Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Jumuiya ya Wasomi wa Kitanzania wanaosoma Nchini China { CAAT} hapo Hyat Regence Jijini Dar es salaam.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa  Jumuiya ya Wasomi wa Kitanzania wanaosoma Nchini China { CAAT}hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa hoteli ya Hyyat Regence Jijini Dar es salaam.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wataalamu Nchini wana jukumu na dhima kubwa ya kuzitumia Taaluma  walizonazo katika kuzibadilisha bidhaa zinazozalishwa Nchini kupitia mchakato wa Viwanda ili ziwe na thamani kubwa itakayosaidia kuinua Uchumi wa Taifa.
Alisema Elimu, Sayansi na Teknolojia waliojifunza Wataalamu hao iwe ndani au nje ya Nchi hawanabudi kuitumia kwa vitendo ili fursa zilizopo katika Sekta ya Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Mali asili zitumiwe vyema wakati Taifa likielekea kwenye Uchumi wa Kati ifikapo Mwaka 2025.
Akiufungua Mkutano wa pamoja baina ya Wataalamu wa Tanzania na China ulioandaliwa na Jumuiya ya Wasomi wa Kitanzania waliosoma China { China Alumni Association of  Tanzania – CAAT} na kufanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya Hyat  Regence  Jijini Dar es salaam Balozi Seif Ali Iddi alisema Wataalamu hao wanapaswa kushirikiana na wenzao wa China katika kufanikisha jambo hilo.
Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya Utalii, Ardhi yenye rutba inayofaa  kwa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi mazao ambayo yanaweza kusafirishwa China  au mahali pengine popote Duniani na kupata thamani kama yatafanyiwa mchakato wa Kitaalamu.
Balozi Seif  alieleza kwamba katika harakati zao  Wataalamu hao ni vyema wakahakikisha kuwa wanachakachua bidhaa hizo kwa uweledi mkubwa wakilenga zaidi kuwasaidia wajasiri Amali wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Alifahamisha kwamba wapo Wananchi wengi waliojikita katika ujasiri Amali kupitia mpango wa kujikwamua na ukali wa maisha wakisubiri kwa hamu Taaluma yao iweze kuwasaidia katika kuboresha bidhaa zao na kufikia kiwango kinachoweza kuuzwa katika soko la Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Wanajumuiya hiyo ya Wasomi  wa Kitanzania waliosoma China kutokubali kutumiwa kisiasa kama baadhi ya Jumuiya nyengine  kama hizo zinazojaribu kuweka matabaka kwa baadhi ya Wanachama wake.
Alisema Alumni hizo wakati mwengine kwa utashi wa kukubali kuburuzwa huamua kuangalia utofauti wa Chama kimoja cha Kisiasa dhidi ya Chama au vyama vyengine jambo ambalo linakwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa Jumuiya kama hizo.
Balozi Seif aliwaeleza wana Alumni hao kwamba Serikali inalikemea vikali jambo kama hilo. Hivyo aliwataka Wanachama hao wa CAAT akiwa kama Mlezi wao wajitambue na kuzingatia Katiba ya Jumuiya yao kama inavyojielekeza.
“ Msikubali kuyumbishwa kisiasa wala kubabaishwa na Mtu au Kikundi chochote kile. Serikali yenu iko pamoja nanyi usiku na mchana katika kuhakikisha mnafikia malengo yenu mliojiwekea”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia nyanja za Uchumi kati ya China na Tanzania  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Jamuhuri wa Watu wa China imefanya mambo mengi ndani ya Ardhi ya Tanzania ikiwemo Ujenzi wa Viwanda pamoja na Miundombinu mbali mbali isiyohesabika.
Alisema hii inathibitisha wazi kwamba Uhusiano wa Tanzania na China unajidhihirisha kupitia nyanja mbali mbali za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii kwa kushuhudiwa kwa misaada iliyotolewa na China kupitia Serikali zote mbili Nchini Tanzania, ile ya Jamuhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif  alifahamisha kwamba pamoja na uwepo wa uhusiano huu wa muda mrefu sasa unaokisiwa  na wanahistoria wanaothibitisha kuwa Wachina waliingia Mwambao wa Tanzania kabla ya ujio wa Watu wa Bara la Ulaya, lakini kwa sasa umekuja zaidi na sura mpya.
Kitendo cha kuwatumia Vijana wa Kizazi Kipya waliosoma China na Kuunda chombo chao kinaleta faraja kubwa kwa Serikali kwa vile sio  tu kumbukumbu nzuri bali pia ni kielelezo thabiti cha Uhusiano mwema baina ya Mataifa haya Mawili.
“  Jumuiya hii ambayo ni daraja thabiti la uhusiano wetu inadhihirisha kuwa urafiki wetu ni urafiki wa kweli. Ahsanteni sana Vijana wetu kwa kuja na wazo hili”. Alisema Balozi Seif.
Kwa upande wa Sekta ya Elimu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alisema Tanzania imepata fursa nyingi za kudhaminiwa Wananchi wake hususani Vijana  kwa kupata nafasi za kusoma Nchini China jambo ambalo linawapa maarifa yanayowawezesha kuwa na uweledi katika Fani mbali mbali.
Alisema miongoni mwa fani hizo yakiwemo Mafunzo ya Muda mfupi na Mrefu yalihusisha ngazi za Elimu katika viwango vya Shahada ya kwanza, shahada ya Uzamili pamoja na ile Shahada ya Uzamivu.
“ Mfano mzuri nyinyi Wana CAAT mnaopata nafasi za udhamini wa Masomo kutoka Serikali ya China kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu kwa kila Mwaka”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Balozi wake Nchini Tanzania Bwana Wang Ke kwa kukubali kwake kuwa sehemu ya Jumuiya hiyo ya Wasomi wa Kitanzania waliosoma China {CAAT}.
Balozi Seif aliendelea kuiomba Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kuzidi kuyashawishi Makampuni na Taasisi zake kuja kuwekeza miradi yao Nchini Tanzania iliyokwisha amua kuwa miongoni mwa Mataifa  yanayoelekea kwenye Uchumi wa Viwanda.
Aidha Balozi Seif  alitoa ombi Maalum kwa Wanajumuiya hao kutoa fursa kwa Watanzania na Wanadiplomasia kama Mabalozi na Maafisa wao walioishi Nchini China kupewa nafasi ya uhuru wa kujiunga na Jumuiya hiyo ili weze kuishi kwa muda mrefu zaidi.
Alisema hatua hiyo muhimu kwa upande mwengine inaweza kusaidia mawazo mchanganyiko yatayotokana na wale walioishi China na kuyaelewa mazingira halisi ya Taifa hilo la Bara la Asia.
Akitoa Taarifa ya Mkutano huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasomi wa Kitanzania waliosoma China Dr.Liggle Vumilia alisema Uhusiano wa China na Tanzania unaendelea kubakia kuwa wa Kihistoria  kwa vile Wataalamu na Wasomi wote walikuwa bado hawajazaliwa.
Dr. Vumilia alisema Wataalamu wa Kizazi Kipya wataendelea kukumbuka mchango mkubwa uliotolewa na Waasisi wa Uhusiano huo wa Kihistoria uliosimamiwa kwa pamoja na Marehemu Mao Tse Tung wa China  na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania ambao ulileta ustawi na Kisiasa.
Alisema alisema kazi ya Wasomo inayowakabili hivi sasa ni kuuendeleza Uhusiano huo katika mabadiliko ya Kiuchumi na kuacha tabia ya kulalamika wakati tayari wameshapata  mwanga wa Elimu itakayowaongoza kuleta mabadiliko hayo.
Mwenyekiti huyo wa Wasomi wa Kitanzania waliosoma China alifahamisha kwamba Kundi hilo lina kazi ya kuibua Miradi ya Kiuchumi ndani ya Jamii itakayosaidia kuanzisha Viwanda Vidogo vidogo vya uzalishaji wa Mboga mboga, Makaa ya mawe pamoja na bidhaa za Baharini.
Ameiomba Serikali kwa sasa kuwapatia soko Tanzania na China ili watoe huduma zao katika kusambaza bidhaa zao wazozalisha kupitia vikundi walivyovianzisha sehemu mbali mbali Nchini.
Akitoa salamu Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania Bibi Wang Ke alisema Urafiki wa Kihistoria wa China na Tanzania hauna mjadala kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia Uhusiano huo.
 Balozi Wang alisema katika kustawisha Urafiki huo Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China inaendelea kujitolea kusaini Mikataba  mipya itakayosaidia kizazi cha sasa katika muelekeo wa kuwajengea mazingira bora ya Kiuchumi.
Alisema jumla ya Mikataba 173 ilitiwa saini kwa Mataifa yasiyopungua 75 na Taasisi tofauti za Mabara ya Asia, Pasific  na Afrika ikiwemo Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Wang Ke alitolea mfano mikataba iliyotiwa saini hivi karibuni kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia ziara ya hivi karibu ya Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Kassim.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kuufungua Mkutano wa pamoja baina ya Wataalamu wa Tanzania na China ulioandaliwa na Jumuiya ya Wasomi wa Kitanzania waliosoma China Balozi Mstaafu wa Tanzania Nchini China Balozi Abdulrahman Shimbo alisema China imechagua Mataifa Manneya Afrika kusambaza Viwanda.
Balozi Shimbo alisema akitekeleza utumishi wake wa Kidiplomasia Nchini China Serikali ya China iliichagua Tanzania Nchi Rafiki ili kuingia miongoni mwa Mataifa hayo Manne baada ya kutangaza rasmi kwamba Taifa hilolinalochukuwa nafasi ya Pili kwa Viwanda Duniani kupeleka  ujuzi wake kusaidia Nchi rafiki.
Katika Mkutano  huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizindua Mtandao wa Wanawake Wasomi wa Kitanzania waliosoma na wanaoendelea kusoma Nchini china ulioenda sambamba na Uzinduzi wa Saccos ya Jumuiya hiyo.
Saccos hiyo itasaidia kuwaunganisha Wanajumuiya kwa kuweka Mitaji itayotoa faida ambayo baada ya Miaka Mitatu wanachama wake wamelenga kuanzisha Benki yao itayowasaidia na kutoa mitaji kwa Wananchi wengine wakiwa na mtazamo wa kufungua Tawi Nchini China katika Malengo ya Baadae.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.