Habari za Punde

Mam Asha mgeni rasmi maadhimisho ya miaka 16 ya Kikundi cha Mazoezi cha Kata Presha

 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya kuasisiwa kwa Kikundi cha mazoezi cha Katapresha kutimia Miaka 16 hapo katika Ukumbi wa Kiwanja cha Kufurahishia Watoto Kariakoo.
 Baadhi ya Wana kikundi cha Katapresha wakijivinjari katika sherehe za Maadhimisho ya Kikundi chao kutimiaka Miaka 16 tokea kuundwa kwake.
 Msanii maarufu wa Kikundi cha Zanzibar One Mordern Taarab Nassor Hussein akiimba wimbo maalum wa kutimia Miaka 16 tokea kuundwa kwa kwa Kikundi cha mazoezi cha Katapresha
 Msanii maarufu wa Kikundi cha Zanzibar One Mordern Taarab Nassor Hussein akiimba wimbo maalum wa kutimia Miaka 16 tokea kuundwa kwa kwa Kikundi cha mazoezi cha Katapresha
 Mama Asha akikata keki maalum kuashirika kutimia kwa sherehe za maadhimisho ya kuasisiwa kwa Kikundi cha mazoezi cha Katapresha kutimia Miaka 16
 Mama Asha akimlisha Keki Mke wa Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar Mama Asha Jecha miongoni mwa Viongozi wa Kikundi hicho kwenye sherehe zao za kutimia Miaka 16.
Mama Asha akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kikundi cha Mazoezi cha Katapresha mara baada ya kukata Keti ikiwa ni ishara ya kukamilika kwa sherehe za maadhimisho ya kuasisiwa kwa Kikundi hicho.
Picha na – OMPR – ZNZ
Na Othman Khamis, OMPR
Jamii bado inaendelea kukumbushwa umuhimu wa kujenga Utamaduni wa kufanya mazoezi kila siku au hata Wiki mara moja ili kujenga Afya itakayochangia kuepuka maradhi mbali mbali mwilini.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alitoa kumbusho hilo wakati wa hafla maalum ya kusherehekea maadhimisho ya Kikundi cha Mazoezi cha Kata Presha tokea kuasisiwa kwake Miaka 16 iliyopita.
Hafla hiyo iliyoshirikisha baadhi ya wanachama wa Vikundi vyengine vya Mazoezi hapa Nchini ilifanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya kufurahisisha Watoto Kariakoo na kuambatana na Muziki laini wa Kikundi cha Zanzibar One Mordern Taarab.
Mama Asha alisema mazoezi ni kitu muhimu kwa Mwanaadamu kinachopaswa kudumishwa kila mara dhana yenye  muendelezo wa kuunga mkono Sera ya Serikali katika kusisitiza Watu kufanya mazoezi ili kupunguza gharama kubwa za uagiziaji wa Dawa unaohitaji fedha nyingi.
Aliwataka wanakikundi hicho cha Katapresha kuwa na wajibu wa kuwa na muda wa kujitathmini kitendo kitakachowapa fursa ya kuzijuwa changamoto zinazowakabili na hatimae kuzitafutia ufumbuzi unaostahiki.
Mama Asha alisema katika tathmini hizo ni vyema pia wakaanzisha Saccos kwa lengo la kupata msukumo wa namna ya kumsadidia Mwanachama pale anapopatwa na matatizo kama maradhi.
Katika kuunga mkono hatua hiyo muhimu Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Rais wa Zanzibar alijitolea kukisaidia Kikundi hicho cha Katapresha jumla ya shilingi Milioni Moja zitakazohamasisha uanzishwaji wa Saccos ya Kikundi hicho.
Mapema akisoma Risala ya Wanakikundi cha Mazoezi cha Katapresha Mwalimu Msaidizi wa Kikunid hicho Ahmad Yussuf Mwalimu alisema Kikundi hicho kilichoanzishwa Mwaka 2013 na kupata usajili rasmi kinatoa huduma za kimazoezi bila ya kujali rangi, dini au itikadi zozote zile.
Ahmad alisema lengo la kuanzishwa kwake kimeelekeza katika kujenga Umoja miongoni mwao na wanamichezo wengine, kuelimisha Jamii umuhimu wa mazoezi katika kukabilaiana na maradhi hasa shindikizo la Damu linalosumbua Wananchi walio wengi hapa Nchini.
Mwalimu Msaidizi huyo wa Kikundi cha mazoezi cha Katapresha alitoa wito kwa Taasisi na Mashirika tofauti Nchini kuhamasisha mazoezi mbali ya kupunguza maradhi lakini pia itatoa nafasi kwa Vijana kujiepusha na vitendo viovu.
Hata hivyo Ahmad alisema Wanamichezo wa Kikundi hicho bado wanakumbwa na changamoto ya eneo la kufanyia mazoezi hasa kipindi ambacho sehemu wanayoitumia ikiwa imepangiwa shughuli nyengine za Kijamii
Alieleza kwamba Kikundi chao hivi sasa kimekuwa na ongezeko kubwa la Wanachama kutoka 20 hadi kufikia 98 kiwango ambacho kwa njia ye yote ile lazima wapate eneo kubwa zaidi ili kukidhi nafasi ya kutosha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.