STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13.10.2019
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Maafisa Wadhamini wanadhima
kubwa ya kuwasimamia wale wote wanaovunja misingi ya kukuza uchumi hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, huko katika
ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta na
Makonyo Wawi wakati alipokutana na Watendaji na Viongozi Wakuu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na viongozi wa vikosi vya SMZ na SMT wanaofanya
kazi zao kisiwani Pemba.
Rais
Dk. Shein alieleza kuwa, kwa mwaka jana kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar
ilifikia asilimia 7.1 na matarajio ni kukua kwa uchumi huo mwaka hadi mwaka kutokana
na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Alisema
kuwa mapato yanakusanywa kwa ufanisi mzuri na kinachokusanywa ndicho
kinachotumika na hakuna tatizo la matumizi ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa hivi sasa.
Alieleza
kuwa kuhusiana na mapato Rais Dk. Shein alisema kuwa wakati anaigia madarakani
mwaka 2010 Serikali ilikuwa ikikusanya TZS Bilioni 13.5 kwa mwezi ambapo kwa
hivi sasa Zanzibar inakusanya TZS Bilioni 65.7 kwa mwezi.
Aliongeza
kuwa mambo mengi yanayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
yanatekelezwa kutokana na fedha zake wenyewe ambapo licha ya kukusanywa kiasi
hicho cha fedha lakini bado hakitoshi, hivyo juhudi zaidi zinahitajika.
Alieleza
kuwa mbali ya juhudi hizo za Seriakli lakini bado wapo wafanyabiashara wanaokwepa
kulipa kodi na kusisitiza kuwa Serikali zote duniani zinakwenda kwa kukusanywa
kodi.
Alitumia
fursa hiyo kusisitiza haja ya kulipa kodi sambamba na kutoa risiti kwani bila
ya kutoa ama kuchukua risiti mapato makubwa ya Serikali yanapotea.
Kuhusiana
na suala zima la mfumko wa bei, Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar uko chini
ambapo wakati anaingia madarakani ulikuwa asilimi 18 na kila siku unashuka na
hadi hivi leo uko chini ya tarakimu moja huku bei ya bidhaa hivi sasa imepungua
sana.
Licha
ya baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bidhaa bei pamoja na kufanya magendo
lakini hata hivyo, juhudi zinaendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuhakikisha
wananchi wa Zanzibar wanaishi vizuri.
Aidha,
Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa kuna kila sababu ya wananchi wa Zanzibar
kutibiwa bure sambamba na kupewa huduma zote za uchunguzi wa afya na kuitaka
Wizara ya Afya kusimamia kwa wale wote watakaofanya hadaa washtakiwe kwa
kuhujumu uchumi.
Rais
Dk. Shein alieleza juhudi za makusudi zitakazochukuliwa na Serikali katika
kuhakikisha Wilaya ya Micheweni inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji safi
na salama huku akieleza kuwa hadi mwishoni mwa mwaka huu katika Mji wa Zanzibar
na vitongoji vyake ukiwemo Mji Mkongwe tatizo la maji litakuwa historia.
Sambamba
na hayo, Rais Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao haja kuwasikiliza watu
wanaokwenda maofisini mwao kufuata huduma na kwamwe wasikatae kuwasikiliza
kwani moja kati ya sifa ya kiongozi ni kuwasikiliza wananchi na ndipo
watakapofanya vyema kazi zao.
Pia,
alieleza haja kwa Maafisa Wadhamini kusimamia nidhamu sambamba na uhujumu wa
mali ya umma ikiwa ni pamoja na kutumia vyema fedha za Serikali kwa taratibu
zilizowekwa.
Dk.
Shein alisisitiza haja ya kupambana na rushwa katika utendaji wao wa kazi na
kusisitiza haja ya kushikamana na kuwapongeza viongozi hao kwa kuendelea
kushirikiana vyema katika utendaji wao wa kazi.
Sambamba
na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa viongozi hao kusimamia vyema vitendo
vinavyopelekea kuporomoka kwa maadili, malezi na inswafu ya maisha.
Pamoja
na hayo, Rais Dk. Shein alieleza mikakati iliyowekwa na Serikali katika
kuhakikisha inatekeleza vyema shughuli zake ikiwa ni pamoja na kupunguza safari
za viongozi, semina na mikutano, posho za vikao vya kazi sambamba na kufanya
mikutano na semina hizo katika kumbi za Wizara za Serikali badala ya kufanywa
kwenye kumbi za hoteli binafsi.
Pia,
alitumia fursa hiyo akuwashukuru viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mapokezi makubwa
waliyomfanyia siku aliyowasili kisiwani humo.
Rais
Dk. Shein alimpongeza Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mmanga
Mjengo Mjawiri kwa kufanikisha vyema Maonyesho ya Siku ya Chakula Duniani
yanayoendeleo huko Chamanangwe Kisiwani Pemba.
Vile
vile, Rais Dk. Shein alieleza matarajio yake kwa mikutano yake aliyoifanya na Wazee
wa CCM wa Wilaya zote Kisiwa humo.
Rais
Dk. Shein alieleza kufurahishwa na hali ya amani na utulivu iliyopo kisiwani
Pemba na kutoa pongezi kwa viongozi wote wenye majukumu ya kuisimamia hali hiyo
huko Kiswani Pemba.
Alisema
kuwa CCM inaidhibiti vizuri hali ya siasa hapa nchini kwani uchumi ni siasa hivyo,
chama hicho kusimamia vyema siasa nchini kwani utulivu unategemea mahitaji ya
wananchi na kuwataka viongozi kuyaeleza hayo kwa wananchi.
Mapema
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi
Haji Gavu alimkaribisha Rais Dk.Shein kuzungumza na viongozi hao.
Nae
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum
za SMZ Haji Omar Kheir alimpongeza Rais Dk. Shein kwa uwamuzi wake huo wa
kuzungumza na watendaji pamoja na viongozi hao na kuahidi kutekeleza yale yote
aliyowaagiza kwa niaba ya viongozi wote.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment