Habari za Punde

Uzinduzi wa Huduma Mpya ya Kutuma Fedha Kati ya Ezypesa na Simbanking Kati ya Zantel na Benki ya CRDB.

Afisa Mkuu wa Benki ya CRDB Bank.Ndg.Fredrick Nshekanabo akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Huduma Mpya ya kutuma fedha kati ya Ezypesa na Simbanking kupitia Simu ya Mkono ya Zantel na Benki ya CRDB Tanzania,hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al Bahri Mbweni Zanzibar.

Ndugu Mohamed Khamis Baucha, Mkuu wa Kampuni ya Zantel Zanzibar,
Viongozi na wafanyakazi wa Zantel,
Wafanyakazi wenzangu wa Benki ya CRDB,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Asalam Aleykhum,

Ndugu Mgeni Rasmi,
Awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kipekee kabisa kutoa shukrani zangu za dhati kwako, kwa kukubali kujumuika nasi katika hafla hii fupi ya uzinduzi huduma ya kutuma pesa kidigitali kutumia simu ya mkononi kati ya Eazypesa na SimBanking ya CRDB bank. Asante sana
Kipee kabisa nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi wa kampuni ya ZANTEL kwa kushirikiana nasi katika kufanikisha jambo hili. Asanteni sana!
 Pia niwashukuru na kuwakaribisha viongozi mbalimbali wa Serikali na wageni wote ambao wamejumuika nasi katika hafla hii. Karibuni sana!

Ndugu Mgeni Rasmi,
Dira ya Benki yetu ya CRDB inalenga katika kutoa huduma bunifu na zenye kukidhi mahitaji ya wateja wetu, popote walipo.
Siku zote, tunaamini katika kuongeza njia mbadala za kutolea huduma zetu ili tuweze kuwafikia wananchi wengi zaidi. Kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma zetu, tumesaidia kuingiza wananchi wengi zaidi katika mfumo rasmi wa malipo, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na nchi nzima kwa ujumla.
Ndugu Mgeni Rasmi,
Tukiongozwa na kauli mbiu isemayo “Benki inayomsikiliza Mteja”, mwaka 2011, tuliingiza sokoni mfumo wa utoaji huduma kupitia simu za mkononi ujulikanao kama “Simbanking”. Kupitia huduma hii mteja anaweza kufanya yafuatayo:
·        Kupata taarifa fupi za akaunti yake,
·        Kuangalia salio,
·        Kufanya malipo ya Ankara (Luku, Dstv, Azam TV, n.k)
·        Kununua muda wa maongezi
·        Kupata mkopo wa haraka wa mshahara (Salary Advance)
·        Kuhamisha pesa kwenda benki nyingine na mitandao ya simu
·        Kufanya malipo ya serikali kupitia mfumo wa kielektroniki wa Serikali (GePG)

Ndugu Mgeni Rasmi,
Huduma hii ya SimBanking inapatikana kwa kwa njia mbili:
·        Kwanza kupiga *150*03# na kufuata maelekezo
·        Pili kupitia “SimBankingApp” inayoweza kupakuliwa kupitia mtandao wa intaneti.

Ndugu Mgeni Rasmi,  
Huduma ya SimBanking ambayo mpaka sasa inatumiwa na zaidi ya wateja milioni mbili, inalenga kuwapa wateja wetu urahisi “convenience” wa kufanya miamala yao popote walipo na kwa wakati wautakao, ndio maana tumekuwa tukitumia kauli mbiu ya “Ulipo Tupo”.

Ndugu Mgeni Rasmi,
Takwimu zinaonyesha ni asilimia 60 ya watanzania ndio wameunganishwa na mfumo wa kifedha kupitia simu za mkononi, wakati ni asilimia 17 tu ya watanzania ndio wanaotumia huduma za kibenki. Hii inaonyesha kuwa njia rahisi zaidi ya kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi, ni kupitia simu zao za mikononi.
Hivyo basi, kuungana kwa Benki ya CRDB na Kampuni ya Zantel kupitia huduma hizi za SimBanking na Eazypesa, ni sehemu ya mkakati huo.

Ndugu Mgeni Rasmi,
Benki ya CRDB ina furaha kuanza kushirikiana na kampuni ya simu ya Zantel na kuzindua rasmi upatikanaji wa huduma za Eazypesa kupitia mfumo wa SimBanking. Muunganiko huu pia, utawapa wateja wa benki ya CRDB wenye kutumia mtandao wa Zantel, uwezo wa kuzifikia akunti zao kupitia simu zao za mikononi, hivyo kuwaondolea ulazima wa kutembelea matawi yetu pindi wanapohitaji huduma. Kwa kiasi kikubwa, muunganiko huu utasaidia kufikisha huduma za kifedha kwa watanzania wengi zaidi na kwa urahisi zaidi.
Kwa kuanzia, huduma zifuatazo zitapatikana:

·        Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya CRDB kwenda Eazy-Pesa
·        Kuhamisha fedha kutoka Easzypesa kwenda akaunti yoyote ya CRDB
·        Kununua muda wa maongezi kupitia Simbanking

Tutaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma hizi ili kuondoa kabisa ulazima wa wateja wetu kutembelea mabenki hivyo kuwapa muda wa kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali na ujenzi wa taifa.

Ndugu Mgeni Rasmi, wageni waalikwa.
Nimalize kwa kuwashukuru wote kwa kufika na kuungana nasi kwenye hafla hii ya uzinduzi. Pia nitoe rai kwenu waandishi wa habari kuwaelimisha na kuwafikishia ujumbe wateja wetu na watanzania kwa ujumla juu ya upatikanaji wa huduma hii.
Aidha, naomba niwakaribishe watanzania wote kuendelea kufurahia huduma za Benki ya CRDB kupitia mtandao wetu uliosambaa nchi nzima bara na visiwani. Nimalize kwa kusema “ULIPO TUPO” tupo tayari kukuhudumia.
Asanteni kwa kunisikilia

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.