Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ndg. Salum Maulid Salum akihutubia wakati wa ufungaji wa Mafunzo ya Ukarimu na Upishi yaliotolewa na Taasisi ya China National Research Institute of Food &Fermentation Industries, ufungaji wa mafunzo hayo umefanyika katika ukumbi wa Sheikh. Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.
UTOAJI wa mafunzo ya watumishi katika maeneo ya kazi ni
miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba
chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein.
Hayo yameelezwa leo na
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Salum Maulid
Salum wakati akifunga mafunzo ya Upishi
na Ukarimu ya awamu ya tatu hafla liyofanyika huko katika Ukumbi wa Sheikh
Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake
Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa hatua
hiyo inatokana na ombi maalum la Rais
Dk. Shein kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China la kuja kutoa mafunzo
kwa watumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuongeza ufanisi wa
shughuli zao.
Aliongeza kuwa hicho
ni kitendo cha kutekeleza sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011
pamoja na kanuni za Utumishi wa Umma kwa vitendo na kuonesha dhamira yake ya
dhati ya kuwaendeleza kitaaluma wafanyakazi wa taasisi mbali mbali hapa nchini.
“Kwa hakika tuna
wajibu wa kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa busara, mapenzi na
uzalendo wake kwa maendeleo ya wafanyakazi na wananchi wote wa
Zanzibar”,alisema Katibu Mkuu Salum.
Aidha, Katibu Mkuu
huyo aliwataka Washiriki wa Mafunzo hayo kulipa hisani hiyo kwa Rais Dk. Shein
ya kuwaombea mafunzo hayo kwa kuongeza ufanisi katika shughuli zao ili waoneshe
tafauti ya kabla ya mafunzo na uwezo wao baada ya mafunzo hayo.
Alisema kuwa kutokana
na umhimu wa mafunzo hayo pamoja na lengo la kuleta ufanisi na kuwapa washiriki
taaluma ya mambo mbali mbali Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
iliongeza muda wa mafunzo kutoka wiki tatu kama ilivyokuwa mwaka jana hadi
mwezi mmoja.
Alieleza kuwa uamuzi
huo umewapa washiriki wa mafunzo hayo muda mrefu zaidi wa kupata mafunzo kwa
kina na kujifunza mambo mengi kuliko wale waliopata mafnzo hayo kabla.
Pia, alieleza haja ya
mafunzo hayo kufanyika hapa Zanzibar kwani imewajumuisha watendaji wengi kuliko
ingefanyika nchini China ambapo fursa hiyo wasingeliipata wote.
Katibu Mkuu huyo
alitoa shukurani kwa uongozi wa Taasisi ya “China National Research Institute
of Food and Fermentation Industries Corpoation Ltd” kwa kukubali kuongeza muda
wa mafunzo kama ilivyoombwa.
Aliwapongeza washiriki
wa mafunzo hayo kwa kushiriki vyema kwa umakini, kujituma na kuonesha nidhamu
katika kipindi chote cha mafunzo hayo na kuwapongeza kwa mwenendo huo kwani ni
kielelezo cha kutambua umuhimu wa mafunzo na kulinda heshima ya taasisi zao.
Aliwataka washiriki
hao waendelee kuudumisha mwenendo huo ili iwe chachu ya kupata ufanisi zaidi
katika kuimarisha Utumishi wa Umma huku akitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa
Mkufunzi Mwelekezi Mwalimu Abdalla Mohamed kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali ambaye amekuwa kiungo muhimu kati ya wakufunzi na washiriki wa mafunzo.
Aidha, alitoa
shukurani za pekee kwa Uongozi wa Taasisi ya Utalii iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), na
Uongozi wa Hoteli ya Verde kwa kuruhusu kutumika kwa maeneo yao katika
kufanikisha mafunzo hayo.
Kwa niaba ya uongozi
na watendaji wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Katibu Salum
aliahidi kuendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuwapatia mafunzo ya muda
mrefu na muda mfupi watumishi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa
majukumu yao.
Katibu Mkuu huyo pia,
alitumia fursa hiyo kutoa shukurani maalum kwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa
na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Xie Xiaowu pamoja
na wafanyakazi wake kwa juhudi zao katika kuimarisha uhusiano uliopo baina ya
China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Sambamba na hayo, Katibu
Mkuu huyo alitoa shukurani kwa uongozi na wakufunzi kutoka Jamhuri ya Watu wa
China kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa hapa nchini na kuahidi
kuendeleza ushirikinao kwa manufaa ya wananchi wa pande mbili hizo.
“Naomba wakufunzi wetu
muichukulie Zanzibar kuwa ni nchi yenu ya pili na msisite kurudi tena, fursa
nyengine ya kufanya hivyo itakapojitokeza”,alisisitiza Katibu Mkuu Salum.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya “China National Research Institute of Food and Fermentation
Industries Corporation Ltd” Bwana Dong Jianhui alitoa shukurani Ofisi ya Rais
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuratibu na kuandaa mafunzo hayo na
kuzishirikisha taasisi nyengine za Serikali pamoja na Binafsi katika mafunzo
hayo muhimu.
Aliwapongeza waahitimu
wote 45 na kueleza kuwa mafunzo hayo yaliyojumuisha kada mbali mbali
zilizojikita na ukarimu na upishi zimeweza kuwajenga vyema na kupata mafunzo
yakiwemo ya vitendo ambayo yatawasaidia katika kufanikisha shughuli zao za
kazi.
Alisisitiza kuwa
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia taasisi ya “ China National
Research Institute of Food and Fermentation Industries Corporation Ltd”
itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na kujenga
uhusiano mzuri.
Mapema Mkuu wa Kitengo
cha Uchumi na Biashara wa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China aliyepo
Zanzibar Bibi Shen Qi alieleza kuwa
hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.
Alieleza kuwa
kufanyika kwa mafunzo hayo ni njia moja wapo ya kuendeleza uhusiano mwema
uliopo na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Watu wa China itaendelea kuziunga mkono
nchi zote marafiki zikiwemo zinazoendelea katika kuhakikisha zinafikia malengo
waliyoyaweka.
Nao washiriki wa mafunzo
hayo katika hotuba yao walitoa pongezi za dhati kwa Rais Dk. Shein kwa
kufikiria kwa kina na kuiomba Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuwaletea
mafunzo hayo ya Ukarimu na Mapishi hapa Zanzibar.
Washiriki hao
walieleza jinsi walivyofaidika na mafunzo hayo ya mwezi mmoja ambapo
walijifunza kwa nadharia na vitendo mambo mbali mbali kupitia kwa wakufunzi wao
yakiwemo kumpokea mgeni, kutayarisha chakula na vinyaji, kuhudumia wageni
mashuhuri (VIP Services), kumuongoza mgeni wakati wa kumpokea, maamkizi na
matumizi sahihi ya lugha katika mazingira tofauti pamoja na mafunzo mengineyo mengineyo.
Sambamba na hayo,
washiriki hao walionesha igizo la kuvutia katika miongoni mwa mafunzo yao
waliyoyasoma ndani ya mwezi mmoja kutoka kwa wakufunzi wao.
Wakati huo huo, washiriki hao
walishiriki katika chakula maalum cha mchana kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ajili ya wahitimu hao huko katika hoteli ya Verde, Mtoni Mjini
Zanzibar.
Mafunzo hayo yaliofungwa
leo yalianza Septemba 11, 2019 ambayo yaliwashirikisha watendaji 45 kutoka
Taasisi za Serikali na Binafsi wakiwemo kutoka Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Baraza la Mapinduzi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
Chuo Cha Utalii Maruhubi, Uwanja wa Ndege na Hoteli ya Verde.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment