Habari za Punde

ZFDA IMEFANYA KIKAO NA WAFANYABISHARA

Na Miza Kona Maelezo Zanzibar   25/10/2019
Mkuu wa Kitengo cha Uchambuzi wa Athari zitokanazo na Chakula kutoka Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) Aisha Suleiman amewataka wafanyabiashara kufanya maombi na kuambatanisha nyaraka muhimu zinazotambulisha biashara pale wanapokusudia kuingiza au kutoa bidhaa zao nchini kwa lengo la kufanyiwa ukaguzi.
Akizungumza na Wafanyabiashara, Wamiliki wa Mashirika ya Ndege, Wasafirishaji na wafanyakazi kutoka viwanja vya ndege huko Ofisni kwake Mombasa Mjini Unguja katika kikao cha Kujadili Utaratibu wa Uingizaji na Utoaji wa Bidhaa Kupitia Uwanja wa Ndege amesema biashara yoyote haiwezi kusajiliwa bila ya kufanya ya kufanyiwa ukaguzi na kuhakikiwa.
Amesema lengo la kufanya ukaguzi ni kujua uhalisia na ubora wa bidhaa inayoingia na kutoka nchini  na kuhakikisha kwamba haina madhara na salama kwa mtumiaji.
Aidha amefahamisha kuwa mfanyabiashara anatakiwa kufanya usajili wa biashara kwa kufanyiwa ukaguzi wa bidhaa na sehemu ya kuhifadhia bidhaa yake ili kuweza kupata kibali cha biashara baada ya kukamilisha utaraibu uliowekwa na wakala wa Chakula na Dawa.
Ameeleza ni vyema kwa wafanyabiashara kufuata muongozo uliowekwa na Wakala wa Chakula ili kuepuka kupata hasara katika uingizaji au utoaji wa bidhaa pindipo linapotokea la kuzuia biashara.
Mkuu huyo amewasisitiza wafanyabiashara hao kujiepusha na  bidhaa zenye vifungashio vyenye maelezo yasiyofahamika ili kuepukana na madhara ya kiafya kwa binadamu.
Nao wafanyabiashara hao wameshauri Wakala wa Chakula na Dawa kutoa taarifa ya ukaguzi wa bidhaa mapema  kwa wafanyabiashara ili kuweza kushirikiana kwa pamoja na kuepuka gharama kubwa.
Aidha wamesisitiza kusimamiwa na kufuatwa vyema muongozo huo ili kuepuka changamoto zilizopo na kuweza kuimarika kwa soko la biashara na kuingiza  bidhaa bila ya usumbufu  .  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.