RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein
akizungumza na Ujumbe wa Madaktari wa Chama
Cha Wapatholojia Tanzania (APT) walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo,(
kulia kwa Rais) Mwenyekiti wa Chama Cha Wapatholijia Tanzania Dkt. Charles
Massambura akiwa na ujumbe wake. wakiwa
Zanzibar kwa ziara ya siku mbili hafla imefanyika leo 1/11/2019 Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameahidi kuendelea kushirikiana na Wapatholojia wote nchini
na kusisitiza haja ya kuwatunza na kuwalea kutokana na umuhimu mkubwa wa fani
yao.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Wajumbe wa Chama cha Wapatholojia Tanzania (APT), ambao wako Zanzibar
kwa ziara maalum ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais Dk. Shein.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alisema kuwa Wapatholojia wana umuhimu mkubwa katika Taifa hili
kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ikiwemo kutoa huduma, kufundisha pamoja na
kufanya tafiti mbali mbali hivyo, ni vyema wakapewa heshima maalum.
Rais Dk. Shein ambaye pia, ni mlezi wa Chama Cha
Wanapatholojia Tanzania (APT), alisema kuwa nia yake ni kuhakikisha chama hicho
kinaendelea kuwa madhubuti na kupelekea vijana wengi kujiunga kwa ajili ya
kufikia lengo lililokusudiwa.
Rais Dk. Shein aliahidi kuendelea na utaratibu huo
wa kuwaalika viongozi hao wa Chama Cha Wapatholojia Tanzania (APT) akiwa mlezi
wa chama hicho na hata pale atakapokuwa si mlezi kwani azma yake ni kuhakikisha
wanachama wa chama hicho wanaendelea kuwa wamoja sambamba na kuendeleza misingi
ya Patholojia.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwekewa
utaratibu maalum wa kuendelea kuwatunza na kuwalea Wapatholojia wa Tanzania
huku akieleza juhudi alizozichukua katika kuhakikisha Wapatholoji hawaharakishwi
kustaafu na badala yake wanaandaliwa mazingira mazuri na Serikali ili waendelee
kutoa huduma kwa jamii.
Alieleza kuwa juhudi hizo ziliweza kuzaa matunda
wakati akiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi
wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati ule Rais Jakaya
Mrisho Kikwete na hivi sasa wataalamu hao wanafanya kazi hadi miaka 65.
Aliongeza kuwa juhudi za makusudi zinaendelea
kuchukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha fani ya Patholojia inaimarika
kwa kiasi kikubwa hapa Zanzibar.
Aidha, alieleza kufarajika kwake kwa kuona vijana wanajiunga
na chama hicho kwani wataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuziba pengo la
wataalamu hao hapo baadae.
Mapema, Rais wa Chama cha Wapatholojia Tanzania (APT)
Dk. Charles Massambura alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa mwaliko wake huo
aliowapa viongozi wa chama hicho wa kuitembelea Zanzibar sambamba na ukarimu
mkubwa walipewa katika ziara hiyo.
Alieleza kuwa wajumbe wote wa Chama hicho waliofanya
ziara yao hapa kuanzia jana 31 Septemba 2019 na kuimalizia leo wamefarajika kwa
kiasi kikubwa kutokana na maendeleo makubwa yaliofikiwa na Zanzibar katika
sekta mbali mbali za maendeleo.
Aliongeza kuwa katika ziara yao hiyo wameweza
kuona mambo mbali mbali ya kimaendeleo ikiwa ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein ikiwemo sekta ya afya, utalii,
miundombinu, uwekezaji pamoja na huduma zote za kijamii.
Aidha, Rais huyo wa chama hicho cha Wapatholojia
alitoa pongezi maalum kwa Rais Dk. Shein kwa kuendelea kushirikiana nao tokea
walipomchagua kuwa mlezi wa chama hicho
mwaka 2014 na kabla ya hapo ambapo alikuwa nao bega kwa bega katika kuhakikisha
chama hicho kinaimarika na kinaleta manufaa kwa Taifa.
Sambamba na hayo, wataalamu hao walieleza
kufarajika kwao na hatua za Serikali zinazochukuliwa chini ya uongozi wa Rais
Dk. Shein za kujenga Hospitali ya kisasa ya Rufaa na kufundisia huko Binguni,
Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja na kupongeza huduma zinazokusudiwa
kutolewa kupitia ramani na michoro waliyoiona
kwa ajili ya ujenzi huo.
Wataalamu hao walimpongeza Dk. Shein kwa mchango
wake mkubwa alioutoa katika kufanikisha mkutano wao wa 10 uliofanyika hapa
Zanzibar Septemba 5 mwaka huu akiwa ni mmoja wa waanzilishi wa Chama hicho
kilichoanzishwa katika mwaka 1991.
Mnamo Septemba 5, 2019 Rais Dk. Shein wakati akifungua mkutano wa 10 wa Jumuiya ya
Wapatholojia Tanzania (APT), uliofanyika hapa Zanzibar aliwapongeza Wapatholojia
hao kwa uwamuzi wao wa kufanya mkutano wao hapa Zanzibar na kuwakaribisha
kuitembelea Zanzibar wakati wowote.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment