Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UNDP Nchini Tanzania.Bi. Christne Musisi alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kuonana na Rais leo, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Miradi ya
Maendeleo (UNDP) limepongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, chini ya
uongozi wa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Pongezi hizo
zimetolewa leo na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Miradi ya Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania Christine Musisi wakati alipokuwa na
mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein.
Katika mazungumzo
hayo, Mwakilishi huyo Mkaazi wa (UNDP), alitoa pongezi hizo kwa Rais Dk. Shein
na Serikali anayoiongoza kutokana na kasi kubwa ya ukuaji uchumi sambamba na hatua
kubwa za maendeleo zilizofikiwa Zanzibar.
Mwakilishi huyo Mkaazi
wa Umoja wa Mataifa alieleza kuwa Katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Shein
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeona mageuzi makubwa ya kiuchumi na
kimaendeleo sambamba na kuimarika kwa utawala Bora.
Aliongeza kuwa Shirika
la Umoja wa Maifa linaloshughulikia Miradi ya Maendeleo (UNDP) litaendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo
ili Zanzibar izidi kupata mafanikio.
Aidha, Mwakilishi huyo
Mkaazi wa (UNDP), alieleza kuwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein Shirika hilo
limeweza kushuhudia mafanikio makubwa ya kiimaendeleo ikiwa ni pamoja na juhudi
za kupamba na umasikini na kukuza uchumi chini ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) ukiwemo (MKUZA II) na kuahidi kuuunga
mkono (MKUZAIII).
Alieleza kuwa huduma
za kijamii zimezidi kuimarika zikiwemo huduma za afya, elimu, maji safi na
salama pamoja na huduma nyenginezo sambamba na juhudi kubwa zilizofanyika
katika kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Hivyo, Kiongozi huyo
alieleza kuwa (UNDP), iko tayari kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia
vipaumbele vyote vilivyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nae Rais Dk. Shein kwa
upande wake alieleza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Miradi
ya Maendeleo (UNDP), ni miongoni mwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) ambalo
limekuwa na mashirikiano na kuweza kuiunga mkono Zanzibar kwa muda mrefu.
Hivyo, Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika hilo na kueleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wanafarajika na juhudi kubwa
inazozichukua Shirika hilo katika kuhakikisha Zanzibar inazidi kupata mafanikio
ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Rais Dk. Shein
aliongeza kuwa uchumi wa Zanzibar umezidi kuimarika kutokana na mashirikiano
makubwa kati ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi
wake bila ya kuwasahau washirika wa Maendeleo kama vile Shirika hilo la Umoja
wa Mataifa (UNDP).
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza juhudi na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha na kukuza uchumi wake ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya
uwekezaji, viwanda sambamba na kuiendeleza na kuiimarisha sekta ya utalii
ambayo inachangia kwa asilimia 27 ya Pato la Taifa la Zanzibar na asilimia 80
ya fedha za kigeni.
Katika mazungumzo
hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa sekta ya utalii imeweza kuimarika kwa kiasi
kikubwa ambapo pia, juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika
kuiendeleza sekta hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hoteli kubwa za kitalii
pamoja na kuviimarisha vivutio vlivyopo.
Kwa upande wa
uwekezaji, Rais Dk. Shein alimueleza Mwakilsihi Mkaazi huyo wa (UNDP) kuwa Mamlaka
ya Ukuzaji wa Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), imekuwa ikifanya kazi kubwa katika
kuhakikisha maeneo huru ya Uchumi yanaimarika na yanafikia yale malengo
yaliyowekwa ambapo kwa upande wa Unguja alieleza kuwa eneo la Fumba tayari
limeanza kutumika kiuwekezaji huku juhudi zikichukuliwa kwa upande wa eneo la
Micheweni huko Pemba.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa huduma za kijamii
zimezidi kuimarika na miradi yote ya maendeleo imeendelea kupata mafanikio na
kueleza kuwa huduma za afya kwa upande wa kupunguza vifo vya akina mama na
watoto vimepungua kwa kiasi kikubwa.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha
Zanzibar inatekeleza azma ya Uchumi Bahari (Blue Economy), ikiwa ni pamoja na kuimarisha
viwanda vidogo vidogo, kukuza sekta ya utalii, uvuvi pamoja na sekta
nyenginezo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment