MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa ndugu Thuwayba Edington Kisasi(kushoto), akikabidhi mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa huo ndugu Mariam Shomari( wa pili kutoka kulia), iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa huo Mhe.Angelina Adam Malembeka.
Na.Mwandishi Wete -Zanzibar.
UMOJA wa Wanawake wa Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi(UWT) kimewataka wanachama wa jumuiya hiyo kuwaruhusu viongozi kutoa michango mbalimbali katika kuchangia maendeleo ya ujenzi wa majengo ya jumuiya kwa mujibu wa utaratibu.
Imesema si viongozi tu bali hata wanachama wowote wanaruhusiwa kutoa michango hiyo ili mradi wapitie katika utaratibu ambao umewekwa ili kutoa sitofahamu.
Kauli hiyo ameitoa Makamu wa Mwenyekiti UWT Taifa, Thuwayba Kisasi,wakati akipokea mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za jumuiya hiyo katika mkoa wa Kaskazini Unguja wenye thamani ya sh.milioni tatu ambao imetolewa na Mbunge wa viti maalum wa mkoa huo Angelina Malembeka.
Makamu huyo wa UWT alisema hazuiliwi mwanachama yeyote wa jumuiya hiyo katika kuchangia maendeleo ya UWT kwa dhamira ya kuijenga jumuiya ili mradi wa kamati za utekelezaji za jumiya na Chama kifahamu suala hilo.
"Chama si wanachama tu bali pia majengo ya kisasa kutokana na kuwa chama hichi kinahadhi yake hivyo lazima jumuiya hii iwe na majengo ya hadhi yake hivyo ninampongeza Mbunge kutoa mchango huu kwa ajili ya kukijenga chama hivyo ametoa fursa kwa wengine kutoa mchango wao,"alisema Makamu Mwenyekiti huyo
Aliongeza kuwa kinachotakiwa kwa kipindi hichi ni kuongeza kasi ya kuzitatua changamoto za wananchi kama CCM ilivyoelekeza ili kukipatia ushindi chama katika uchaguzi mkuu na kwamba si muda wa kurumbana.
Alisema kinachotakiwa wanajumuiya wa UWT kutambua ni muda wa kukijenga chama na jumuiya kwa pamoja na kuachana na tofauti zilizopo kati yao na kwamba hali hiyo ya mivutano haipendezi.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Kaskazini Unguja,Angelina Malembeka alisema mchango huo ameutoa kutokana na kuunga mkono chama katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa vitendo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya UWT ya kisasa.
Alisema UWT mkoa wa Kaskazini imejenga jengo la ofisi yake lakini imeishia hatua ya mwanzo na kwamba mchango wake huo utasaidia kuendeleza ujenzi huo ambao umesimama kwa muda.
"Nimefanya haya kwa ajili ya kukijenga chama pamoja na UWT na mchango huu wa mifuko ya saruji ina thamani ya sh.milioni tatu na kwamba ninatekeleza ilani kwa vitendo kwa kuhakikisha UWT mkoa ina kuwa na jengo lake la kisasa,"alisema
No comments:
Post a Comment