Habari za Punde

Wazazi na Walezi Waaswa Kupambana na Cchangamoto za Malezi ya Watoto Nchini.

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi. Mwajuma Magwiza akizungumza na wadau na waandishi wa habari za Watoto na Malezi wakati wa Kongamano kuhusu Ajenda ya kitaifa ya wajibu wa wazazi na walezi katika malezi na matunzo ya familia liliwahusisha wahariri na waandishi wa habari za Watoto na Familia lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
Wazazi na Walezi nchini wameaswa kuzingatia suala la malezi kwa watoto katika familia kwani bado ni changamoto na limekuwa likileta matatizo mbalimbali kwa watoto nchini ikiwemo kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi wao na wengi wao kukimbilia kuishi mitaani.
Hayo yamebainika leo jijini Dar e salaam katika kongamano la kitaifa la waandishi wa habari kuhusu Agenda ya Kitaifa kuhusu wajibu wa wazazi/ walezi katika malezi na matunzo ya Familia liliwakutanisha wahariri na waandishi wa habari zinazohusu Watoto, Malezi na Matunzo ya Familia.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto BI. Mwajuma Magwiza amesema kuwa Kwa mujibu wa utafiti  uliofanywa na Wizara kwa kushirikiana na wadau kwa kipindi cha Disemba 2017 hadi Januari 2018 katika Halmashauri 12 za Ilala, Kinondoni, Temeke, Kigamboni, Ubungo, Arusha, Iringa, Mbeya jiji, Wilaya ya Mbeya, Dodoma, Nyamagana na Ilemela iligundua uwepo wa Jumla ya watoto 6,393 ikiwa watoto wa kike  1,528 na watoto wa kiume  4,865 wanaosihi na kufanya kazi mitaani.
Bi. Mwajuma Magwiza ameongeza kuwa kati yao watoto 1,385 watoto wa kike  410 na watoto wa kiume 975 walitambuliwa wakiishi na kufanya kazi mitaani muda wa usiku uwepo wa watoto hawa maeneo ya mitaani kwa kiasi kikubwa unatokana  na kutowajibika kwa familia katika kumudu majukumu yao ya kutunza na kulea watoto wao.
Aidha Bi. Mwamjuma aliongeza kuwa kulingana na Taarifa ya utafiti wa afya ya mama na mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2015/16 inaonesha kwamba asilimia 25 ya kaya za mijini na asilimia 27 ya kaya za vijijini zina watoto ambao hawaishi na wazazi wao japokuwa mzazi mmoja au wote wawili bado wapo hai, hii inamaana wanaishi katika familia pana au wao wenyewe peke yao hivyo kukosa malezi ya wazazi wa pande zote mbili yaani baba na mama katika makuzi yao.
”Hii inawaathiri sana watoto kisaikolojia na wakati mwengine inasababisha na kuchangia kwa kiasi kikubwa watoto kuamua kuondoka na kwenda maeneo mengine ikiwemo mitaani, kujishughulisha na shughuli hatarishi kwa ajili ya kujipatia mahitaji yao.” alisema Bi. Mwajuma
Ameongeza kuwa kwa kuthamini na kutambua umuhimu wa Familia katika malezi na matunzo ya familia Serikali imendaa  Ajenda hiyo ya Kitaifa ambayo inalenga katika kuhakikisha kuwa wazazi na walezi na jamii kwa ujumla inakumbushwa na kuhimizwa kuwajibika katika kuwapa matunzo na malezi bora watoto kwa kuwajenga katika maadili, elimu ili waweze kufikia ndoto zao na kuwa na taifa bora.
Niwaombe wamiliki wa vyombo vya habari kutenga muda wa kuwa na vipindi mahsusi vya kuwakumbusha na kuwaelimisha wazazi na walezi wajibu wao katika kuwalea, kuwatunza, kuzungumza na kuwapa upendo watoto ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanakuwa salama na kufikia ndoto zao na kuja kuwa wazazi bora wa baadae” alisema Bi. Mwajuma
Akizungumza kwa niaba ya katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mkurugezi Msaidizi sehemu ya Familia kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi. Tausi Mwilima amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa familia inasimama imara na kutimiza wajibu wake katika kutoa malezi chanya Wizara imeandaa Ajenda hii ya Kitaifa ambayo inaweka msisitizo katika maeneo makuu 5 ambayo ni matunzo, ulinzi, mawasiliano, kujenga familia na upendo. Maeneo hayo yakieleweka na kufanyiwa kazi watoto na vijana wetu watakuwa salama katika maeneo mbalimbali na tutaweza kutengeneza kizazi bora na imara chenye watu wenye maadili na uzalendo kwa Taifa letu.

Ameongeza kuwa Katika Kongamano hilo watatoka na mpango kazi wa pamoja wa namna bora ya kutekeleza Ajenda hii kupitia vipindi mbalimbali ambapo Wizara kwa kushirikiana na vyombo vya habari watakubaliana, namna bora ya kutekeleza kampeni ya Familia Imara Taifa Bora itakayotekelezwa kwa pamoja na wadau mbalimbali kupitia vyombo vya habari na njia nyingine zitakazoonekana zinafaa kufikisha hamasa hii kwa jamii ili kuleta matokeo chanya.

“Wizara imejipanga katika kuhakikisha kuwa elimu hii inawafikia wadau mbalimbali makundi maalum ya kimkakati, aidha, kwa leo tumeanza na kundi la wanahabari watakaoshirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa Ajenda hii inatekelezwa na kila mtu vikiwemo vyombo vya habari”.alisisitiza Bi. Tausi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.