MAKAMO
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kasi ya ukuaji uchumi wa Zanzibar
imeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 7.1.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo wakati akifunga Semina ya siku
moja ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC), huko katika ukumbi wa
Taasisi ya Mafunzo wa Benki Kuu ya Tanzania (B.O.T) uliopo katika mtaa wa
Nyamagana jijini Mwanza.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kwamba mafanikio
hayo yamepatikana kutokana na kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya
ya upotevu wa mapato hayo.
Alisema kuwa hali hiyo imeongeza mapato kutoka TZS bilioni
181.1 mwaka 2010 hadi kufikia TZS bilioni 748.9 mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la
mara 4.1 au sawa na asilimia 314 na kuzipongeza taasisi za TRA na ZRB ambazo
zinakusanya mapato.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar Awamu ya Saba imeongeza bajeti yake kwa mara 3.2 kutoka TZS bilioni
444.6 mwaka 2010/2011 hadi TZS trilioni 1.4194 mwaka 2019/2020.
Aliongeza kuwa kutokana na ufanisi huo, hata bajeti za
Wizara mbali mbali nazo zimeongezeka ikiwemo Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya,
Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi.
Sambamba na hayo, Makamo huyo wa CCM Zanzibar alieleza kuwa
huduma za jamii nazo zimimarika kutokana na mambo ya Kisera yaliopangwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara tu baada ya Mapinduzi ya Januari 12,
1964 katika huduma za elimu na afya na kupelekea huduma hizo kutolewa bure.
Rais Dk. Shein alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imetoa umhimu mkubwa katika kuhakikisha Amani na utulivu vinakuwepo
nchini wakati wote ambapo hali hiyo ndiyo iliyowezesha kupiga hatua kubwa za
maendeleo katika nyanja ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yote ya utekelezaji wa Ilani
yametokana na kuwepo kwa amani na utulivu ambayo yametoa nafasi ya kuyaenzi
Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 pamoja na Muungano uliopo.
“Ibara ya 127 ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka
2015-2020 inatuelekeza kuwa CCM itaendelea kuwa muumini wa kweli wa amani na
utulivu na kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kuwa wamoja wenye mashirikiano na
wanaopendana”, alisema Dk. Shein.
Aleleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kazi
ya kuandaa Mwelekeo Mpya wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020-2050 baada ya
kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira 2020.
Alisisitiza kuwa Dira hiyo mpya ya Maendeleo ya Zanzibar
itakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya
2020-2030 na kuandaliwa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya 2020 kwa upande wa
Zanzibar katika kuiletea maendeleo Zanzibar.
Alisema kuwa CCM imeimarika na inakubalika kwani imeweza
kushinda katika chaguzi mbali mbali kwa sababu wananchi wanakikubali hivyo,
aliwataka viongozi hao kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya chama hicho
huku akieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar ushindi wa chama hicho katika
uchaguzi ujao hauepukiki.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa CCM
Taifa, Katibu Mkuu wa CCM pamoja na viongozi wote wa chama hicho kwa upande wa Tanzania
Bara kwa ushindi mkubwa wa asilimia 99.9 wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwataka Wajumbe wote wa
NEC kufanya kazi na wazee na kuziunga mkono jitihada wanazozifanya katika
mabaraza yao katika maeneo wanayoishi sambamba na kuendelea kuwandaa vijana
kuwa wazalendo.
Nae Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Samia Suluhu Hassan akitoa neno la shukurani
alipongeza jitihada za Rais Dk. Shein katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ambazo zimeipelekea Zanzibar kupata mafanikio makubwa.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli alieleza
mafanikio makubwa yaliopatikana katika miaka minne ya uongozi wa chama hicho
ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM kwa kiasi kikubwa na
kuwataka viongozi wa NEC kutumia nafasi waliyonayo katika kuleta mabadiliko ya
Tanzania kiuchumi.
Alieleza juu ya mwelekeo mpya wa Sera za CCM katika miaka
ya 2020-2030 katika kuhakikisha Tanzania inajitegemea kiuchumi kupitia sekta ya
viwanda huku akisisitiza kuwa Tanzania
ni nchi tajiri kutokana na rasilimali nyingi zilizopo.
Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo wa CCM alitumia fursa
hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa ushirikiano mkubwa aliotoa katika
kuhakikisha mafanikio hayo makubwa yanapatikana hapa nchini.
Alieleza mwelekeo mpya wa Sera za CCM katika miaka ya 2020
hadi 2030 na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya 2020 katika kuimarisha sekta ya
viwanda, elimu, maji, mawasiliano, kilimo, uvuvi na ufugaji, madini, utalii
ambapo alieleza jinsi watalii walivyoongezeka kwa Tanzania Bara na Zanzibar kutokanana
vivutio kadhaa vilivyopo.
Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliipongeza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein kwa kununua meli mpya ambapo
alieleza kuwa usafiri huo wa meli utawasaidia wananchi ikiwa ni pamoja na
kusafiri ndani na nje ya nchi.
Pia, Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kutoa tangazo la
kuachiwa kwa ndege ya Tanzania iliyokuwa inashikiliwa nchini Canada na
kuwaeleza wananchi kuwa watatangaziwa siku ya kuwasili ili wakaipoke ambapo
inatarajiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Mwanza.
Mada mbali mbali zilitolewa katika semina hiyo ikiwemo
Mafanikio ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa kipindi cha
miaka mine kwa upande wa Tanzania Bara ambapo ilitolewa na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na kwa Zanzibar ilitolewa na
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment