Habari za Punde

WADAU WATAKIWA KUTOA MCHANGO UTAKAOBORESHA UTENDAJI KAZI NA KULETA TIJA KATIKA UTUMISHI WA UMMA


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na wadau wa Tija katika Ukumbi wa HAZINA Ndogo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa wadau hao kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wenye lengo la kujadili uboreshaji wa utendaji kazi katika Utumishi wa Umma ili kuongeza Tija.


Baadhi ya wadau wa Tija wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) katika Ukumbi wa HAZINA Ndogo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa wadau hao kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wenye lengo la kujadili uboreshaji wa utendaji kazi katika Utumishi wa Umma ili kuongeza Tija.

Na.James K. Mwanamyoto. 
Wadau wa tija katika Utumishi wa Umma pamoja na wanazuoni  wametakiwa kujadili na kuishauri Serikali juu ya namna bora ya kuboresha utendaji kazi na kuongeza Tija Serikalini.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma leo, na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akifungua mkutano wa wadau  kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wenye lengo la kujadili uboreshaji wa utendaji kazi katika Utumishi wa Umma ili kuongeza Tija.

Dkt. Mwanjelwa amesema, mchango wa wadau hao utasaidia kuishauri Serikali  namna ya  kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wa umma na  kuongeza tija ambayo itasaidia katika kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wa maendeleo na huduma zenye kiwango stahiki zinazotakiwa kutolewa na Taasisi za Umma.

“Nawasihi mjikite zaidi katika kuchambua na kutafakari kwa kina juu ya namna ya kuwa na misingi imara na vigezo vitakavyosaidia katika kuboresha zaidi utendaji kazi Serikalini na kuongeza Tija”, amesisitiza Dkt. Mwanjelwa.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, ongezeko la pato la taifa lolote duniani ndio msingi na chanzo cha kuboresha mishahara na masilahi ya watumishi, kuboresha maisha na kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo wadau wanapaswa kuishauri vema Serikali kuongeza wigo wa mapato na hatimaye iweze kuboresha masilahi ya watumishi wa umma.

Mkutano huu wa siku mbili wa wadau wa kujadili uboreshaji wa utendaji kazi katika Utumishi wa Umma ili kuongeza Tija umeratibiwa na Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kuiwezesha Serikali kupata mchango na ushauri katika kuboresha utendaji kazi na Tija ndani ya Utumishi wa Umma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.