Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwapungia mkono Wananchi wa Kijiji cha Kibondemzungu wakati wa hafla ya ufunguzi wa Daraja la Dk.Ali Mohamed Shein Kibondemzungu barabara ya Fuoni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja akipita katika daraja hilo baada ya kulifungua, (kushoto kwa Rais) Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar.Mhe. Dkt, Sira Ubwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zuberi Ali Maulid na (kushoto kwa Rais) Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Ndg. Mustafa Aboud Jumbe.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa ujenzi wa
barabara na daraja la Kibonde Mzungu ni uthibitisho wa Mapinduzi kwani kabla ya
Mapinduzi hapakuwepo madaraja na barabara nzuri kama zinazojengwa hivi sasa
hapa Zanzibar.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla ya ufunguzi wa
Daraja la Kibonde Mzungu, lililopewa jina “Daraja la Dk. Shein”, liliopo Wilaya
ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, hafla iliyofanyika eneo hilo la
Kibonde Mzungu ikiwa ni shamrashamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliongeza kuwa wakati
huo daraja kubwa hapa Zanzibar lilikuwa ni daraja la Tingatinga lililopo Kaskazini
Unguja ambalo halikuwa na sifa wala vigezo kama madaraja na barabara
zinazojengwa hivi sasa ambazo zina ubora kwa wananchi kwa ajili ya usarifi wao na bidhaa zao.
Alisema kuwa baada ya
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kila kitu kilishamiri zikiwemo barabara, nyumba
na mambo mengineyo., “lakini hivi sasa tunachokitaka wenyewe tunajenga, na mimi
nataka nikukumbusheni ujenzi wa daraja hili mara tu baada ya kulitembelea mnamo
mwaka 2017 yalipotokea mafuriko na kuamuru kujengwa”.
“Nilisema tujengeni
daraja kubwa la kisasa hapa, daraja liwepo tena liwe kubwa na zuri na leo
limejengwa na kila mtu analiona”. Alisisitiza Dk. Shein.
Katika hafla hiyo, Rais Dk. Shein alieleza kwa ufupi historia ya
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na kueleza juhudi zilizochukuliwa katika
kuhakikisha wanyonge wa Zanzibar wanakuwa huru sambamba na kuimarika kwa sekta
za maendeleo zikiwemo barabara.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Mapinduzi yataendelea kusemwa kila siku kwani ni jambo ambalo lina maslahi
ya wananchi wote licha ya kuwepo baadhi ya watu ambao hawapendi kuyataja,
kuyazungumza wala kuyasikia.
Alisema kuwa Mapinduzi
yalikuwa ni lazima yafanywe na yatokee kutokana na dhulma zilizokuwepo Zanzibar
kutoka kwa watawala wa Kigeni wa Kisultani na Kiengereza hatua ambayo
ilipelekea kuanza kwa vuguvugu la Mapinduzi na hadi uhuru kupatikana.
Alisema kuwa uchumi wa
Zanzibar ulihodhiwa na Wakoloni hao ikiwemo elimu, afya na sekta nyenginezo na
mnyonge alikuwa hana maana wala hawezi kufanya starehe za aina yoyote na badala
yake kulikuwa na mipaka na mahala pa kushereheka na muda maalum pamoja na saa
maalum za kufanya starehe.
Rais Dk. Shein pia,
alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 nchi zote duniani ziliyatambua hasa
kwa malengo yake ya kujenga umoja wa watu wa Zanzibar, kujenga mshikamano na
maelewano, amani sambamba na kuondosha ubaguzi.
Alisema kuwa hatua
hiyo ilipelekea kutungwa kwa Sheria ya mwanzo ya Rais, Sheria Namba 6, iliyotiwa saini mnamo tarehe 25
Februari mwaka 1964 ambapo katika uongozi wa Rais Karume kila kitu kiliongozwa
kwa sheria na taratibu za nchi.
Alisema kuwa wakoloni
hawakujenga chochote kwani tokea wakati huo Kibonde Mzungu ilikuwepo na Wakoloni
walikuwepo lakini hawakujenga barabara wala daraja kama hilo na badala yake
waliimarisha usafiri katika maeneo ya Mji Mkongwe pamoja na kujenga treni
katika eneo la mjini pekee.
Alisema kuwa ndani ya miaka
56, kumefanywa mambo mengi na Zanzibar sivyo ilivyo leo huku akisisitiza kuwa
kila fedha zitakaporuhusu, zitajengwa barabara hata barabara za juu (Fly-over).
Alisisistiza haja kwa
Serikali kuanza utaratibu wa kujenga barabara za juu (Fly-over) kwani tayari
ameshatoa agizo kwa Wizara hiyo kutafuta jibu la ujenzi wa barabara hiyokuelekea
Kaskazini ili iaze wapi kwani ni lazima Serikali ifanye.
Rais Dk. Shein
aliitaka Wizara hiyo kuhakikisha mjenzi anayejenga barabara ya kutoka katika
daraja hilo mpaka kituo cha Polisi Fuoni akabidhi barabara hiyo mwezi Februari
kama ulivyomkataba na kusisitiza kuwa mkataba huo usivukwe.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliiagiza Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) waunganishe barabara
inayotokea katika daraja hilo hadi eneo la barabara inayoelekea Koani, kwani
wana vifaa vipya, wataalamu wanao huku akisisitiza kuwa ni basi kutoa tenda za
ujenzi wa barabara kwa ile barabara wanayoweza kuifanyia kazi.
Alisisitiza kuwa
kwamwe haiwezekani Serikali kununua vifaa vya Bilioni 14 halafu kukaanza
kutolewa tenda za ujenzi wa barabara zinazowezwa kujengwa na Idara hiyo na kuitaka
kujenga wenyewe barabara za Pemba na Unguja na pale zitakapotaka kujengwa
barabara kubwa waendelee kutoa tenda lakini kwa ile wanayoweza wafanye wenyewe na
waepuke kupigwa changa la macho.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alikubali Daraja hilo kuitwa jina lake na kupokea heshima hiyo na
kumpongeza Wazari, katibu Mkuu na wafanyakazi wote wa Wizara hiyo kwa
kushirikiana na mkandarasi wa ujenzi huo.
Dk. Shein alieleza
haja ya kutiwa taa za barabarani katika eneo hilo kuanzia eneo la Jumbi bango
la Mkoa hadi kituo cha Polisi cha Fuoni jambo ambalo limeungwa mkono na Wizara
husika na kusema kuwa hayo ni maendeleo kwani barabara kutiwa taa na kujengwa
mitaro pembezoni ni jambo muhimu.
Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano
na Usafirishaji Dk. Sira Ubwa Mamboya
alisema kuwa ilikuwa ni changamoto kubwa sana hasa wakati wa mvua na maji
yalikuwa yanajaa katika eneo hilo na kusababisha madhara ambapo kwa sasa tatizo
hilo limeondoka na litakuwa ni historia na wananchi hivi sasa wanapita usiku na
mchana.
Katika maelezo Waziri
huyo alisema kuwa ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na
kumpongeza Rais Dk. Shein kwa miongozo yake na kumuhakikishia kuwa watafanya
kazi kwa kadri ya uwezo wao katika kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo
hasa katika sekta ya usafiri.
Waziri Sira
aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa Mfuko wa Barabara kwa juhudi
kubwa zilizochukuliwa katika kuhakikisha daraja hilo linajengwa na barabara
hiyo nayo inajengwa na kupitika tena kwa kiwango kizuri na kuwapongeza wale
wote waliofanikisha ujenzi huo huku
akiwaomba wananchi wote wa Unguja na Pemba kuzitunza barabara kwani zinagharimu
fedha nyingi katika ujenzi wake.
Alisema kuwa barabara
zinagharimu fedha nyingi hasa pale zinapoharibika kwa bahati mbaya ama pale zinapoharibiwa
kwa makusudi hivyo aliwataka wananchi kuzitunza vizuri.
Sambamba na hayo,
Waziri Dk. Sira alisisitiza haja ya kuyaenzi, kuyalinda na kuyadumisha
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kwani ndio dira ya maendeleo..
Hata hivyo, Waziri Dk.
Sira alimuomba Rais Dk. Shein kuwa daraja hilo liitwe kwa jina lake Rais Dk.
Shein ili iwe kumbukumbu ya wananchi kutokana na juhudi zake alizozichukua
katika kuhakikisha tatizo la eneo hilo linapatiwa ufumbuzi.
Mapema Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa
ujenzi wa Daraja la Kibonde Mzungu ni miongoni mwa jitihada zinazochukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaondolea wananchi changamoto mbali
mbali za usafiri wananchi wa Unguja na Pemba.
Alisema kuwa ujenzi
huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020
kama ilivyoelekezwa kwenye ukurasa wa 138 Sura ya 88 kilichoeleza kuwa “Serikali
itaendelea na kazi ya utunzaji na matengenezo ya barabara zilizokwisha kujengwa
na kufanya marekebisho katika maeneo yanayotuama maji ya mvua na kuathiri ubora
wa barabara hizo”.
Katibu Mkuu huyo
alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya uamuzi wa kulijenga
daraja katika eneo hilo la Kibonde Mzungu kutokana na athari zilizokuwa
zinajitokeza kila wakati wa mvua kwa kutuwama kwa maji mengi ambayo yalipelekea
kufungika barabara na kushindwa kutumika.
Aidha, alisema kuwa
kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya maamuzi ya
kulitafutia ufumbuzi wa kudumu sehemu ya Kibonde Mzungu kwa kujenga Daraja
kubwa ambalo litaweza kuondoa changamoto iliyokuwepo.
Aliongeza kuwa ujenzi
wa daraja hilo ni sehemu ya ujenzi wa barabara ya
Mkunazini-Kariakoo-Magomeni-Fuoni-Tunguu yenye urefu wa kilomita 16.76 ambao
ujenzi wake unakwenda awamu kwa awamu ambapo pia, ni barabara ambazo zimo
katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020.
Alisema kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
mnamo tarehe 31 Agosti, 2018 ilitiliana saini Mkataba wa ujenzi wa daraja hilo
na Kampuni ya Mwananchi Engineering Construction Company (MECCO) kwa ajili ya
ujenzi huo.
Kwa maelezo ya Katibu
Mkuu huyo alisema kuwa mradi huo hadi kukamilika kwake umegharimu jumla ya TZS
Bilioni 4.319 fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina uliochini ya Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar.
Pia, Katibu Mkuu huyo
alisema kuwa Wizara hiyo inaendelea na ujenzi wa barabara kutoka Kibonde Mzungu
hadi Fuoni Polisi yenye urefu wa mita 1.2 kazi ambayo inafanywa na Kampuni hiyo
ya MECCO na inatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2020.
Rais wa
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment