Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kutembelea Vivutio Vya Utalii wa Ndani Zanzibar.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud akiwakabidhi Mwakilishi wa Baraza la Vijana la Wilaya ya kati Baskeli na Vifaa vya kazi huko Kiboje Wilaya ya kati katika Ufungaji wa Tamasha la Utalii wa ndani kwa kutumia Baskeli Mkoa wa Kusini Unguja.
Na Mwashungi  Tahir     Maelezo  Zanzibar.                                                                 
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud ameitaka jamii kutembelea vivutio vya utalii ili  kuelewa vivutio vya kitalii viliopo Zanzibar na kuachana na  dhana ya utalii kwa wageni .
Akizungumza hayo na Washiriki wa Tamasha la Utalii wa Baiskeli  huko Shehia ya  Kiboje Mkoa wa Kusini Unguja wakati alipokuwa akifunga tamasha hilo na kuitaka jamii , vijana kutembelea sehemu zenye mambo mbalimbali katika Mkoa huo.
Amesema Wazanzibar wengi wanahisi utalii uko sehemu ya Forodhani , na kuwataka waachana  na dhana hiyo, kwa kufahamu kwamba utalii uko Zanzibar nzima  na una  sehemu  nyingi za vivutio takribani vingi sana ikiwemo Mkoa wa Kusini Unguja.
“Watalii wengi wanaona utalii upo Forodhani tu, hapana, utalii uko Zanzibar Nzima na kuna vivutio vingi katika sehemu mbali mbali za Zanzibar”, Alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Hata hivyo amesema wazaliwa wa Nchi hii wawe wa mwanzo katika kukuza utalii wa ndani na kuutangaza Utalii kwa wote na ili uwe endelevu kwa lengo la kuuimarisha.
Aidha aliwataka Wazanzibar kuweka mashirikiano na umoja  kwa lengo la kuuweka utalii wa ndani na utalii kwa wote katika Mkoa huo.
Pia alisema katika Mkoa wa Kusini Unguja tushatekeleza kwa vitendo  dhana  hiyo ya Utalii kwa  kufanya matembezi katika maeneo mbali mbali ya kitalii yenye vivutio vyote vya Kitalii  na kuwapatia fursa vijana kuweza kujua mambo yaliyomo .
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja  Idrissa Kitwana  Mustafa amesema rasilimali zilizopo ndani ya Mkoa huo  zitawafanya vijana kuzitumia kwa kupitia ujasiriamali  na mambo mengine ya kujiendeleza kwa kupitia vivutio hivyo vya utalii.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kati  Hamida Mussa Khamis  amesema lengo kuu la Tamasha hilo ni kuunga mkono Jitihada za Serikali ya Mapinduzi katika Sekta ya Utalii wa ndani na Utalii kwa wote kwa kufanya kwa vitendo.
Pia amesema ndani ya tamasha hilo vijana wameweza kujifunza na kuelimika kwa mambo mengi ambayo walikuwa hawayajui.
Nao washiriki wamevutika sana kwa matembezi hayo na kuahidi mwakani watajitokeza zaidi.
Zaidi ya vivutio vya utalii wa ndani na Utalii kwa wote 13 vimeweza kutembelewa na washiriki kukabidhiwa vyeti na Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika tena  ifikapo Ijumaa ya mwisho January 2021 ndani ya Mkoa huo .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.