Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihakikiwa taarifa zake na Afisa wac Tume ya Uchaguzi Zanzibar(ZEC) Ndg. Salum Abdulrahman Nadhif, alipofika Kituo cha Kujiandikisha Wapiga Kura Skuli ya Msingi Bungi Wilaya ya Katiu Unguja leo.29-2-2020.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amewatoa wasi wasi wananchi
waliokuwa hawajapatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na kuwataka kuwa na
subira kwani kitambulisho hicho ni haki ya kila mwananchi wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo, katika
mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kuhakiki taarifa zake kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika kituo cha kupigia kura cha skuli ya
Msingi Bungi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Rais Dk. Shein akiwa amefuatana na Mama Mwanamwema
Shein katika zoezi hilo, alisema kuwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kina
umuhimu mkubwa kwa mwananchi wa Zanzibari kutokana na kusaidia katika shughuli
mbali mbali na si ya kutumia kwa uchaguzi pekee.
Hivyo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wasiwe na
wasi wasi kwani Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itachukua jukumu lake la
kuhakikisha kila mwenye sifa ya kupata kitambulisho hicho basi anakipata kwa
taratibu na sheria zilizopo.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa zoezi hilo
linakwenda vizuri kutokana na muda na taratibu zilizowekwa ambazo zimekuwa
zikiwasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kuweza kuhakiki taarifa zao kwa ufanisi
mkubwa pale wanapofika vituoni.
Alieleza kuwa kazi zote zina changamoto na hasa
zile zinazowahusu watu wengi sambamba na kuwepo kwa utaalamu mpya, hivyo
aliwataka wananchi waendelee kuwa wastahamilivu na bila ya kukiuka sheria na
kuwahakikishia kuwa kila mwenye haki yake ya kupata Kitambulisho cha Mzanzibari
Mkaazi atakipata.
“zoezi linakwenda vizuri, nimetumia muda mfupi na
wasimamizi na waandishi wanafanya kazi zao vizuri “alisema Rais Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imejiandaa kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao wa Zanzibar mwaka
huu 2020 una kuwa huru na wa haki na wala hakutakuwa na zogo wala khasia
zozote.
Rais Dk. Shein ambaye alifika kituoni hapo mnamo
majira ya saa tatu za asubuhi na kujumuika na wananchi waliojitokeza katika
zoezi hilo, alisisitiza kuwa na kwa wale wote ambao wenye nia ya kuvuruga
uchaguzi kwa njia zozote zile Serikali
itawadhibiti.
Rais Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa
atahakikisha Zanzibar inaendelea kuwa salama na yenye amani katika wakati wote
wa uongozi wake na hata wakati wa kiongozi mwengine ajae.
Alieleza kuwa Serikali ni ya watu wote na si ya
mtu mmoja na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwepo na
anapoondoka yeye atakuja kiongozi mwengine na anaamini atatokana na Chama chake
cha Mapinduzi (CCM) ambacho kitaendelea kushinda kama ilivyo kawaida ya chama
hicho katika uchaguzi ujao.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi
kuendelea kumuombea dua yeye pamoja na kuiombea Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ili makusanyo ya mapato yaendelee kuwa mazuri kwa azma ya kutekeleza
ahadi yake ya kuongeza mshahara kabla ya kumaliza madaraka yake japo kwa asilimia
ndogo.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar ni Tume Huru ambayo imekuwepo muda mrefu tokea kuanzishwa chaguzi hapa
Zanzibar ambayo imekuwa ikifanya
vizuri kutokana na kuendeshwa kwa mujibu
wa Katiba ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Aliongeza kuwa licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya
uongozi kwa kila ufikapo muda uliowekwa lakini bado Tume hiyo ipo vizuri na
haijatetereka na imekuwa ikifanya kazi zake vyema kwa mujibu wa Katiba ya
Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza imani
yake kwa Tume hiyo na kusisitiza kuwa inaimani kubwa kuwa Tume hiyo itafanya
vizuri sana katika uchaguzi mkuu ujao kwani tokea alipoingia madarakani mwaka
2010 Tume hiyo imekuwa ikifanya vizuri. Hivyo, aliwataka wananchi watulie na
wala wasiwe na wasi wasi.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment