Habari za Punde

Wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Washerehekea Siku ya Kuzaliwa kwa Mhe. Balozi Seif leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwaasa Wafanyakazi kazi wake kuwa na Utii katika majukumu yao wakati walipomfanyia Tafrija ya Kushtukizia ya Siku yake ya Kuzaliwa.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Mitawi akimlisha kipande cha Keki Balozi Seif kama ishara ya kumpongeza kwa kutimia Miaka 78.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi akitoa shukrani kwa niaba ya Viongozi na Wafanyakazi wa Taasisi yake mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
 Baadhi ya Viongozi na Wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakishiriki kwenye tukio hilo la kushtukizia.
Wafanyakazi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kumfanyia tafrija ndogo ya kushtukiza Bosi wao Mhe. Balozi Seif Ali Iddi baada ya kutimiza Miaka 78 ya Siku yake ya kuzaliwa kila ifikapo Tarehe 23 Febuari.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi   amewaasa Watumishi wachanga na wale wanaoendelea na Majukumu  yao kwa sasa katika Taasisi za Umma na zile Binafsi kuzingatia kwa kina suala la Utii kwenye utekelezaji wa Kazi za kuhudumia Jamii mahali popote pale.
Alisema Utii ndio dhana nzito, sahihi na inayobeba ngao kubwa kwa Mtumishi ye yote na matokeo yake hujikuta akipata fursa nyingi zinazomuwezesha kuheshimika sambamba na kupanda daraja katika maeneo yake ya Kazi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa wasia huo kufuatia Uongozi na Wafanyakazi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kumfanyia tafrija ndogo ya kushtukiza baada ya kutimiza Miaka 78 ya Siku yake ya kuzaliwa ifikapo Tarehe 23 Febuari ya kila Mwaka.
Alisema yeye akiwa miongoni mwa Watumishi wa umri mrefu wa kazi usiopungua Miaka Sitini katika nafasi mbali mbali za Utumishi wa Umma ameshuhudia mambo mengi katika mafanikio ya huduma za Kijamii yaliyobebwa na dhana ya Utii uliotukuka.
“ Huwezi kupata mafanikio yoyote katika Taasisi iwe za Umma, Binafsi na hata Familia kama hutakuwa na Utii kwa wale waliokuzunguuka muda wote katika matendo yako ya kila Siku”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif  alieleza kwamba katika umri wake hata akiwa nje ya Utumushi wa Umma ataendelea kutoa busara zake kwa wale wote watakaokuwa tayari kuchota busara hizo muhimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika kipindi chote cha kuiongoza Wizara hiyo ndani ya Muda wa Miaka Tisa na Nusu.
Alisema Ushirikiano huo kwa kiasi kikubwa ndio ulioleta mafanikio makubwa ndani ya Wizara hiyo iliyo inayosimamia Shughuili za Serikali yanayoshuhudiwa na Wananchi walio wengi Mjini na Vijijini.
Akitoa shukrani kwa Niaba ya Uongozi na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Nd. Abdullah Hassan Mitawi alisema Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi ni Tanuri lenye mambo mengi yanayoweza kutumiwa na Watendaji wachanga.
Kaimu Katibu Mkuu Mitawi alisema tanuri hilo lililojaa busara, uzoefu pamoja na hekina  za takriban Miaka Sitini litakuwa chachu ya kuchotwa na Viongozi na Watendaji wachanga katika Utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya kuwatumikia Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizaliwa Mnamo Tarehe 23 Febuari Mwaka 1942 katika Kijiji cha Mgambo Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja na kupata Elimu za Dini na Dunia kama walivyo Watoto wote wa Ukanda wa Mwambao.
Balozi Seif alipata Mafunzo ya Ualimu Beit El Ras na kuanza Kazi ya Kufundisha katika Skuli ya Kinyasini iliyo jirani na Kijiji chake ambapo jitihada zake zilimuwezesha kuteuliwa kuhamia Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania akiwa Afisa wa Kawaida.
Aliendelea na wadhifa huo uliobadilika kila kukicha kutokana na Utii wake katika kazi iliyompandisha daraja na kuwa Balozi kamili wa kuiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi kirefu na Mataifa mbali mbali Duniani.
Balozi Seif Ali Iddi alistaafu Kazi kwa mujibu wa Utumishi wa Umma na kuamua kuingia katika ulingo wa Kisiasa uliomuewesha kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi {CCM} kwa Upande wa Zanzibar.
Ulingo huo wa Kisiasa ulimfungulia njia na kuchaguliwa na Wananchi kuwa Mbunge wa Jimbo lililokuwa la Kitope kwa Tiketi ya Chama cha Mapinduzi {CCM} katika Vipindi Viwili na kupata nafasi ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Tanzania Miaka Mitano ya awali.
Kutokana na Utii aliokuwa nao Balozi Seif  wakati bado akiendelea kuwa Mbunge wa Kitope Awamu ya Pili ulimshawishi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kumteuwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Baadae aliamua kugombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar nafasi iliyompa fursa ya Kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndani ya kipindi cha Miaka na Nusu sasa.
Balozi Seif  Ali Iddi wakati akiyafungua Mafunzo ya Vijana katika Chuo cha Ujasiri Amali cha Wadi ya Mahonda hapo kwenye Tawi la CCM Kitope “B” Mnamo Tarehe 15 Oktoba Mwaka 2018 alitoa kauli ya kutogombea tena nafasi ye yote ameshatangaza Rasmi kujipumzisha na shughuli za Kisiasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.