Habari za Punde

AfDB imeipatia Tanzania Mkopo wa Masharti Nafuu US Dola Milioni 495.59


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (kushoto), akisaini Mikataba mitano yenye thamani ya Dola za Marekani 495.59 na Mwakilishi  Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Alex Mubiru (kulia) katika hafla iliyofanyika Benki Kuu Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (kushoto), akibadilishana nakala ya Mkataba na Mwakilishi  Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Alex Mubiru (kulia) katika hafla iliyofanyika Benki Kuu Jijini Dar es Salaam, Tanzania na AfDB zimesaini mikataba mitano yenye thamani ya Dola za Marekani 495.59.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, akiwa  katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano (Ujenzi), Mhandisi Elius Mwakalinga (wa pili kushoto), Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika(AfDB), Alex Mubiru( wa pili kulia), Afisa Mtendaji Mkuu Tanroad, Patrick Mfugale na watendaji wa Mamlaka Viwanja vya Ndege na Tanroad mara baada ya utiaji saini wa mikataba ya Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege wa Kimaifa wa Msalato Jijini Dodoma, Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo-Pangani-Tanga uliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam.


Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO                                                                                        
Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), zimesaini mikataba mitano ya mkopo wa masharti nafuu ya Dola za Marekani milioni 495.59 ambayo ni sawa na TZS trilioni 1.14 zitakazowezesha kutekeleza ujenzi wa miradi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato Jijini Dodoma, Dola za Marekani  milioni 271.63, ujenzi wa barabara ya Bagamoyo-Holoholo-Lungalunga–Malindi km.120.8 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 168.76 na Dola 55.2 kwa ajili ya Programu ya utawala bora na kuendeleza Sekta Binafsi.

Katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema kuwa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo Afrika zimekuwa na mahusiano mazuri ambayo yamewezesha kutolewa kwa mkopo huo wenye masharti nafuu.

“Kama tunavyojua sekta ya miundombinu ndiyo sekta muhimu ambayo inaweza kuinua biashara na kukuza uchumi kwa hiyo katika kulitambua hilo Benki ya Maendeleo Afrika imekubali kutupatia mkopo huu, ambao utatumika katika utekelezaji wa kuboresha miundombinu kwa ujenzi wa Uwanja mkubwa wa Ndege Msalato Jijini Dodoma utawezesha kumudu ndege kubwa za kimataifa kutua”, alisema Doto James.

Alisema kuwa kupitia mikataba hiyo AfDB itaipatia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mikopo ya masharti nafuu  ya dola za Marekani milioni 198.63 kupitia dirisha la African Davelopment Bank ( ADB Window), dola Marekani milioni 246.96 kupitia African Development Fund (ADF Window) na dola milioni 50 kupitia mfuko wa Serikali ya China unaosimamiwa na AfDB.

Aliongeza kuwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege Msalato na ujenzi wa barabara ya Bagamoyo-Pangani kwa kiwango cha lami itaisaidia Serikali kuziba pengo la miundombinu na kuchochea kasi ya maendeleo ya Uchumi kwa jamii ya watanzania.

Aidha kupitia AfDB miundombinu ya barabara mbalimbali imeshatekelezwa na zinaendelea kutekelezwa zikiwemo za Tabora-Koga-Mpanda Km 342.9, Mbinga-Mbamba bay Km. 66, mradi wa awamu ya pili ya mabasi yaendayo kasi Km. 20.3, Kabingo-Kasulu-Manyovu Km. 260, barabara ya kuzunguka Jiji la Dodoma Km.110.2 huku upande wa Zanzibar AfDB inafadhili barabara za Bububu-Mahonda-Mkokotoni Km.31 na barabara za kuunganisha vijiji vya Zanzibari Km.21, kwa hiyo benki hii ni wadau wakubwa wa maendeleo Tanzania

Pia Alibainisha kuwa kuna barabara nyingi za ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo Afrika zimekamilika na kutumiwa na wananchi kufanya biashara na kukuza uchumi wao zikiwemo za Arusha-Namanga km. 105, Singida-Babati-Minjiru km. 223.5, Iringa Dodoma km.260, Tunduru-Mangaka-Mtambaswala km.202.5, Namtumbo-Tunduru km.193 Dodoma-Babati km.188.1 na Arusha bypass km.42.4 pamoja na upanuzi wa barabara ya Sakina-Tengeru km 14.1 kwa njia nne kwa hiyo ushirikiano huu umewezesha kuimarisha ujenzi wa miundombinu hiyo ili kumarisha sekta ya usafirishaji.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika AfDB nchini Tanzania, Bw. Alex Mubiru, alisema kuwa mikataba hiyo inayotoa dola za Marekani 495.6 zitafikisha dola za Marekani bilioni 2.38 ambapo kati ya hiyo dola za Marekani bilioni 1.47 zimewekezwa kwenye miradi ya miundombinu.

“Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Msalato utachukua takribani miaka minne ambapo inakadiliwa kuwa na uwezo wa kubaba ndege 50, 000 kwa mwaka, abiria 1.5 na utakuwa uwanja mkubwa wa kimataifa Jijini Dodoma utakatumiwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani kote wafanyabiashara na watalii”, Alisema Alex Mubiri.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanroad, Mhandisi Patrick Mfugale alisema kuwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato Jijini Dodoma utakuwa na uwezo wa Kutosha kubeba ndege kubwa kwani utakuwa na urefu wa kilomita 3.6 na upana wa mita 60.

“Uwanja huu wa Msalato Jijini Dodoma utakuwa mkubwa wa kuhudumia ndege kubwa aina ya Dreamliner 17, na kama ni aina ya Airbus ni ndege 380, magari  ya kawaida 472, na mabasi ya abiria 72, na ukimalizika utahudumia abiria mililioni 1.5 kwa mwaka”, alisema Mhandisi Mfugale.

Lakini pia ujenzi wa daraja la mto pangani utasaidia wananchi wa Tanga kufanya biashara zao bila usumbufu ambapo daraja hilo litakuwa na nguzo nane, huku barabara ikiwa na km 105 barabra kuu na km. 25 barabara unganishi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.