Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar wakati alipotembelea Jengo linalotarajiwa kuwa la Uchunguzi wa Virusi Zanzibar,Wilaya ya Kati Unguja lilioko katika enelo la Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar, (hawapo pichani) na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Afya Zanzibar.Mhe. Hamad Rashid Mohammed na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar.Dkt. Mayasa Salum Ally.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kuacha ukaidi na kufuata
kikamilifu maelekezo ya Serikali, ikiwa ni hatua za kuunga mkono juhudi za
Serikali katika kukabiliana na Virusi vya Ugonjwa wa Corona.
Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipotembelea eneo
linalotarajiwa kujengwa jengo la Uchunguzi wa maradhi makuu, liliomo ndani ya Taasisi ya Utafiti wa Afya, huko Binguni, Wilaya Kati Unguja.
Amesema katika kukabiliana na virusi
vya ugonjwa huo, Serikali tayari imetowa malekezo kadhaa, ikiwa njia ya
kujikinga na virusi vya ugonjwa huo, hivyo akawataka wananchi kuacha ukaidi na
kutekeleza maelekezo ya kudumisha usafi kama inavyoelekezwa.
Alisema Virusi vya Ugonjwa wa Corona
ni janga na Kimataifa na ni maradhi yasiotaka mzaha wala hayachaguwi aina ya
mtu wa kuamuathiri, hivyo ni vyema wananchi wakaondokana na ushindani na
kuzingatia maelekezo ya Serikali.
Alieleza kuwa Serikali imeingia katika
vita dhidi ya adui asieonekana na hivyo ikalazimika kuchukuwa hatua mbali mbali
za dharura ikiwemo kuzuia Kongamano la dini pamoja na kuzifunga skuli zote na
wanafunzi kukosa taaluma.
Shein alisema Serikali haiwezi kuainisha ukubwa
wa gharama inazopoteza kutokana na hatua
ilizochukuwa katika kukabiliana na virusi vya ugonjwa wa Corona, sambamba na
athari za kiuchumi zitokanazo na kuvurugika kwa sekta ya utalii, ambayo huchangia
asilimia themanini ya fedha za kigeni.
Rais Dk. Shein aliwataka wananchi
kuondokana na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi
kuondokana na mikusanyiko, hususan katika eneo la Hospitali kuu ya Mnazi mmoja
pamoja na maeneo ya masoko, kwa kigezo kuwa hatua hiyo inaweza kuwa chanzo cha
kusambaa kwa viusi hivyo, pale itakapotokezea mtu mmoja kuwa navyo.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein
alilisistiza azma ya Serikali ya kujikita katika kufanya uchunguzi wa maradhi mbali
mbali kwa kigezo kuwa hakuna tiba muafaka bila ya kuwepo uchunguzi, hivyo
akabainisha dhamira ya Serikali katika kukamilisha ujenzi wa jengo la kisasa la
Maabara katika eneo hilo la Binguni.
Alisema Serikali imefikia uamuzi wa kukamilisha
jengo hilo mahala hapo kwa kuzingatia mazingira bora yaliopo, ambayo yamejitenga
na pia ni mazuri kwa shughuli hizo.
Aliwahakikishia wananchi kuwa jengo
hilo litakamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo pamoja na kuwekewa vifaa vyote muhimu ili kukidhi
mahitaji na malengo yaliokusudiwa.
Aidha, alisema Serikali itakamilisha
miradi yote ya Maendeleo iliyokwisha anzishwa, ikiwemo ya ujenzi wa Nyumba Kwahani, Michenzani Mall, Barabara, Mahakama
Kuu na mingineyo pamoja na kuanzisha miradi mipya, huku akibainisha kuwa endapo
kutatokezea upungufu wa fedha itaangalia namna ya kukamilisha miradi hiyo.
Mapema, Waziri wa Afya Hamad Rashid
Mohamed, amesema Wizara hiyo imejiandaa kikamilifu kushirikiana na Serikali ya
Watu wa China katika dhana ya kukuza
utalaamu ili kuleta ufanisi wa maabara
itakayojengwa.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment