Habari za Punde

SMZ Itaendelea Kuchukua Hatua Kuimarisha Sanaa na Kuendeleza Utamaduni Kwa Kuwaendeleza Wasanii Kuwaongezea Taaluma

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wasanii mbalimba Zanzibar katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha sanaa na kuendeleza utamaduni kwa kuwaendeleza wasanii kwa kuwaongezea taaluma ya kuzifanikisha shughuli zao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Mkutano alioufanya kati yake  na Wasani wa Zanzibar,  huko katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa jitihada maalumu zitachukuliwa kuhakikisha kuwa kazi za sanaa zinatoa fursa kubwa zaidi ya ajira kwa vijana kwa kufanya shughuli zao kisasa na bora zaidi ambazo zitatumia fursa ya soko la utalii.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa katika kuyafikia malengo hayo, Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha nyumba ya sanaa iliyopo Mwanakwerekwe kwa kuijenga upya na kuwa na jengo la kisasa lenye taswira nzuri.

Alieleza kuwa nyumba hiyo itawekwa vifaa vya kisasa pamoja na kuongeza walimu wa fani mbali mbali za sanaa ambapo kukamilika kwa hatua hio kutatoa nafasi muhimu kwa vijana wa Zanzibar kupata sehemu nzuri ya kujifunza ujuzi wa fani mbali mbali.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa sanaa na utamaduni ni nyenzo muhimu za kuitambulisha jamii na ni hazina muhimu ya kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi chengine kwani jamii isiyokuwa na utamaduni, mila, silka, desturi pamoja na sanaa yake inakuwa kama vile haipo.

Rais Dk. Shein alieleza furaha yake kwa kukutana na wasanii hao kutoka Unguja na Pemba na kueleza kuwa jamii ya watu wa Zanzibar kama zilivyo jamii nyengine duniani nayo pia, ina sanaa, tamaduni, mila, silka, desturi zake tangu enzi na dahari zilizoachwa na wazee hivyo, ni lazima zitunzwe, zidumishwe na ziendelezwe.

Alisema kuwa sanaa imeiletea sifa Zanzibar na kuifanya ijulikane miaka mingi iliyopita ambapo historia inaeleza kuwa wasanii wa zamani akiwemo Marehemu Bibi Siti bint Saad tangu miaka ya 1930 aliweza kuitangaza Zanzibar kwa muziki wa taarabu kiasi cha kufika India na Mataifa mengine duniani.

“Sanaa ni uhai wetu, kwa hakika maisha bila ya sanaa  yangekuwa chapwa na kama yanauzwa yangekuwa bure ghali…….kwa mnasaba huo kazi za wasanii ni muhimu na nakuhakikishieni kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana na inatambua umuhimu wa wasanii”, alisema Dk. Shein.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa kuienzi, kuidumisha na kuiendeleza sanaa na utamaduni wa Kizanzibari ikiwa ni utambulisho na urithi wa jamii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imekuwa ikichukua hatua mbali mbali katika kuiimarisha sekta hio.

Alieleza kuwa yapo mengi yaliyofanywa na Serikali kwa ajili ya kuziendeleza sanaa na utamaduni wa Zanzibar kwa vipindi tofauti kwa muda wa miaka 56 ya Mapinduzi ambapo katika kipindi chote hicho kila awamu ya uongozi wa Serikali iliunda Wizara maalum inayoshughulikia mambo ya sanaa na utamaduni na kuteuliwa viongozi wenye sifa wa kuiongoza Wizara hio.

Rais Dk. Shein alisema kuwa tayari zoezi la ugawaji wa mirahaba limefanywa kwa awamu 6 tangu lilipoanza mwaka 2013 ambapo katika mwaka huo TZS milioni 37.0 ziligawiwa na katika mwaka 2019 jumla ya TZS milioni 120.1 ziligawiwa kwa wasanii mbali mbali wakiwemo waliokwishatangulia mbele ya haki.

Hivyo, Rais Dk. Shein aliwahimiza wasanii na wabunifu kujisajili ili waweze kunufaika zaidi kwa kazi zao kupitia utaratibu huo ulioanizishwa na kusimamiwa na Serikali yao ambayo haina ubaguzi na inasimamia suala hilo kwa mujibu wa sheria na haki kwa kila msanii na mbunifu aliyesajiliwa rasmi.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliitaka Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kushirikiana ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali ya kufufua vuguvugu la michezo katika maskuli linasaidia pia, kukuza masuala ya sanaa na utamaduni.

Aidha, aliitaka Wizara ya Elimu kuviendeleza vipaji kwa kuwapa fursa watoto kucheza katika vipindi maalum vinavyotengwa kwa michezo ndani ya wiki ya masomo.

Pia, alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa ya kuwepo kwa watumiaji wa vifaa vya muziki na filamu ili waweze kukuza biashara zao na wasiogope kuleta biashara hizo kwani hazitooza na badala yake zitapamba maduka.

Aliitaka Wizara hiyo kufanya mpango wa kuwaendeleza wasanii kwa azma ya kuonesha kuwa wanawathamini na wako pamoja nao kwa uzima na maradhi huku akiitaka Wizara hiyo kuzifanyia kazi changamoto zote 20 zilitotolewa na wasanii hao ndani ya mwezi mmoja na baadae kumueleza Rais walipofikia.

Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), kwa kubuni kipindi maalum cha “Vuna Vipaji” ambacho kimesaidia vijana kujitokeza na kuonesha uwezo wao wa kuigiza.

Kadhalika, aliwataka wasanii kuendelea bila ya kuchoka kuendeleza sanaa na utamaduni wa Kizanzibari pamoja na kuonesha katika sanaa zao athari za kuiga na wasikubali kuziacha kwa namna yoyote ile sanaa, utamaduni, mila na desturi zao na ni vyema wakazitetea wakati wote.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wasanii kutokana na kuwa mwaka huu wa 2020 Tanzania inakabiliwa na uchaguzi mkuu wakaandaa kazi za sanaa zenye kuhamasisha wananchi kuitumia haki yao ya kuwachagua viongozi kwa amani na utulivu kwani hakuna mbadala wa amani.

Nae Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Karume alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kukutana na wasanii hao wa Zanzibar jambo ambalo limeonesha namna anavyowajali pamoja na kuzithamini kazi zao.

Alieleza jinsi Wizara inavyochukua juhudi za kuwaendeleza wasanii wa Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na kuiendeleza lugha ya Kiswahili ili kiendelee kuwa lugha ya Taifa huku akisisitiza kuwa Wizara hiyo itahakikisha inafanya juhudi za kutekeleza haki za wasanii kupitia Mirabaha inayotokana na kazi zao.

Nao wasanii katika risala yao iliyosomwa na Mwanakombo Mwadini ilimpongeza Rais Dk. Shein kwa uongozi wake kwa kuimarisha miundombinu, utawala bora, kudumisha amani, kuinua hali za wananchi, kuinua sekta za elimu, kilimo, afya, mawasiliano, ajira na nyenginezo bila ya kuisahau sekta ya utamaduni, ubunifu na sanaa.

“Wasanii kwa pamoja tunakushukuru na kukupongeza kwa kuinua hali za wasanii na sanaa kwa ujumla hakika Mheshimiwa Rais wewe ni miongoni mwa wasanii nguli na ni mwenye kuipenda Sanaa, Pia tunakupongeza kwa kutengeneza ukumbi wa kufanyia mikutano yetu pamoja na studio ya kisasa ya kurikodia kazi zetu” walisema wasanii.

Wasanii hao walitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa uongozi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuonesha dhahiri kwa vitendo kwamba inathamini shughuli za sanaa na kuwa bega kwa bega huku Wasanii hao wakitumia fursa hiyo kueleza changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Rais Dk. Shein pia, alipata fursa ya kuwasikiliza wasanii mbali mbali katika mkutano huo ambao walieleza mafanikio na changamoto wanazozikabili huku wakipongeza hatua yake ya kwenda kukutana nao.

Katika mkutano huo pia, wasanii kutoka vikundi mbali mbali vya Unguja na Pemba walitumia fursa hiyo kuonesha kazi zao ikiwemo michezo ya kuigiza pamoja na ngoma ya Kibati yenye asili ya kisiwa cha Pemba, mkutano huo ambao pia, uliwajumuisha wasaanii wakongwe wa fani zote kutoka Unguja na Pemba.

Rais Dk. Shein kwa kuonesha jinsi anavyowajali na kuwathamani wasanii hao pamoja na wabunifu mbali mbali waliohudhuria katika mkutano huo pia, aliwaandalia chakula maalum cha mchana hapo katika viwanja vya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni Jijiji Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.