Habari za Punde

Waziri Mkui wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Atembelea Hospital ya Wilaya ya Kibaha Iliyotengwa Kuwahudumia Wagonjwa wa CORONA.

Waziri Mkuu, Kaasim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  (wa tatu kulia) wakati alipokagua hospitali ya wilaya ya kibaha iliyopo eneo la Lulanzi  ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahuduma kwa wagonjwa wa Coroma, Machi 28, 2020.  Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo  na wa pili kushoto ni  Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Bakari. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua wodi za hospitali ya wilaya ya Kibaha  iliyopo eneo la Lulanzi  ambayo imetengwa  kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Corona Mchi 28, 2020. Kushto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilio.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili kuwahudumia watu watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) na amesema ameridhishwa na maandalizi.

Aliyasema hayo jana (Jumamosi, Machi 28, 2020) wakati akizungumza na wananchi wilayani Kibaha, Pwani baada ya kukagua hospitali ya wilaya ya Kibaha ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu watakaogundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabilia na COVID-19, ambapo kwa sasa watu wote wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandari lazima wapimwe na wakigundulika wanamaambukizi wanawekwa kwenye maeneo maalumu kwa muda wa siku 14.

“Tunazingatia sana wale wanaotoka kwenye nchi ambazo zimeathirika sana wakiingia hapa Tanzania tunawazuia kwanza, tunawapima na tunafuatilia historia yake anatoka wapi na tunaangalia katika siku 14 amepita kwenye nchi zipi.”

Waziri Mkuu alisema wawaweka kwenye maeneo maalumu ili kuweza kuwapima kila siku na kujirishika kama hawana maambukizi kwani mtu anaweza kupimwa leo akaonekana yuko vizuri lakini ana maambukizi ambayo bado hayaonekani kwenye vipimo. Kama katika kipindi cha siku 14 mtu atabainika hana maambukizi anaruhusiwa kwenda kujiunga na familia.
Pia, alisisitiza wananchi waendelee kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuzuia mikusanyiko na kwa wale wanaosafiri kwenye usafiri wa umma wasibanane kila mtu akae kwenye kiti.

Waziri Mkuu alisema wananchi wanapokwenda kufuata huduma kwenye masoko wahakikishe wanapeana nafasi baina ya mtu mmoja na mwingine na kabla hawajaingia katika maduka wanawe mikono kwa sabuni na maji tiririka ili kujikinga na maambukizi ya corona.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kuwachukulia hatua watu wote wanaopotosha kuhusu taarifa za ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). “Aliyetangaza kuwa shule zinafunguliwa tumeshamkamata na atachukuliwa hatua.”

Hivyo aliwataka wananchi wajihadhari na taarifa zinazotolewa na watu ambao si wasemaji rasmi. Alisema taarifa kuhusu virusi vya corona itatolewa na Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Msemaji wa Serikali.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, MACHI 29, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.