Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi Mdogo Mpya wa India anayefanyia Kazi zake Zanzibar.Mhe. Bhagwant Singh, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo.16/3/2020.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa hatua za India za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar
zina imarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na udugu uliopo kati ya
pande mbili hizo.
Hayo yamesemwa leo na
Rais Dk. Shein wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mdogo Mpya wa
India katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Bhagwant Singh, aliefika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya
kujitambulisha.
Katika maelezo yake Dk.
Shein alisema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na India ambao umeanzishwa na waasisi wa Mataifa hayo akiwemo Hayati Julius
Kambarage Nyerere kwa mashirikiano na waasisi wa India akiwemo Hayati
Jawaharlal Nehru na baadae Hayati Indira Gandhi.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa waasisi hao walishirikiana kwenye nyanja za kimataifa ikiwa ni
pamoja na kupiga vita ukoloni pamoja na ubaguzi wa rangi.
Akielezea juu ya
ushirikiano na uhusiano kati ya India na Zanzibar, Dk. Shein alimueleza Balozi
huyo kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano uliopo hatua ambayo imesaidia
sana kuongeza ushirikiano katika sekta
mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, biashara, miundombinu, kilimo, huduma
za kijamii na nyenginezo.
Kwa upande wa ushirikiano
uliopo katika sekta ya elimu, Dk. Shein alitoa pongezi kwa India kwa kuendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi
kadhaa za masomo kwa Zanzibar nchini humo katika fani mbali mbali.
Akiongezea mazungumzo
hayo katika sekta hiyo ya Elimu, Rais Dk. Shein alieleza haja ya India kuweza
kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa ajili ya kuleta
wakufunzi kwa ajili ya masomo ya Tiba na Kinga ya Meno yanayoendeshwa na Chuo
Kikuu hicho.
Dk. Shein alisema kuwa
India ni nchi ambayo inatambulika duniani kote kutokana na kupiga hatua katika
mafunzo ya masomo ya Sheria na Tiba hivyo, hatua hiyo ya kuleta wakufunzi kuja
kusomesha Chuo Kikuu cha (SUZA) kutasaidia kuimarisha sekta ya afya hapa
nchini.
Aidha, alieleza kuwa
hatua hiyo pia, itapunguza idadi ya wagonjwa kwenda nchini India kwa ajili ya
kufuata matibabu yanayotolewa na Hospitali zake kuu za nchi hiyo na badala yake
huduma hizo zitatolewa na madaktari wazalendo watakao pata mafunzo hayo hapa
hapa nchini katika chuo hicho Kikuu hicho cha (SUZA).
Pia, alipongeza hatua
za mashirikiano zilizofanyika Kati ya Zanzibar na India kwa nchi hiyo
kuikopesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia benki yake ya Exim kiasi
cha Dola za Kimarekani milioni 92 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji
safi na salama katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza hatua zinazoendelea kutokana na makubaliano ya mashirikiano
yaliyofikiwa wakati wa ziara yake nchini humo mnamo Februari mwaka 2014.
Dk. Shein alimuahidi
Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana nae
katika kuhakikisha anaendelea kufanya kazi zake vyema hapa nchini ikiwa ni
miongoni mwa kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya India na
Zanzibar.
Nae Balozi Mdogo Mpya wa
India anaefanya kiazi zake hapa Zanzibar Bhagwant Singh alipongeza uhusiano na ushirikiano wa muda
mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na kuahidi kuwa nchi yake utauendeleza
kwa manufaa ya pande zote mbili.
Balozi Singh alimpongeza
Rais Dk. Shein kwa kasi kubwa ya maendeleo yaliyofikiwa hapa Zanzibar na
kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ili zizidi
kuimarika.
Aliongeza kuwa India
itahakikisha inakamilisha miradi yote ya maendeleo ilioanzishwa kwa
mashirikiano kati yake na Zanzibar sambamba na kuendelea kutoa nafasi za masomo kwa Zanzibar zikiwemo
zile za muda mfupi kwa watendaji wa Serrikali kupitia mpango wa “Indian
Technical and Economic Cooperation Program” (ITEC) na “International Forestic
Science” (IFS).
Aidha, alieleza hatua
za nchi hiyo za kuendelea kusaidia upatikanaji wa vitendelea kazi na kuleta
wakufunzi katika Chuo cha Amali
Vitongoji Pemba ambapo Mpango huo upo katika hatua za mwisho za ujenzi wa
majengo ya chuo hicho.
Sambamba na hayo,
Serikali ya India imeweza kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha elimu ya amali
kwa kufadhili ujenzi wa Chuo cha Amali Kibokwa, Unguja kwa lengo la kutoa ujuzi
kwa akina mama na vijana mradi ambao tayari umeshakamilia na kukabidhiwa kwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka 2019.
Pamoja na hayo, Balozi
Singh, alieleza azma ya nchi hiyo ya kuendelea kushirikiana na nchi za Bara la
Afrika ikiwa ni pamoja na kuendelea kuziunga mkono juhudi za nchi hizo katika
sekta zake za maendeleo ili zizidi kupiga hatua za maendeleo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment