Habari za Punde

Mkutano wa Tume ya Uchaguzi na Viongozi wa Vyama Vya Siasa Tanzania

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
MHE.  JAJI WA RUFAA (MST.) SEMISTOCLES KAIJAGE KWENYE MKUTANO WA TUME NA  VYAMA VYA SIASA KATIKA
UKUMBI WA MIKUTANO WA MWL. NYERERE, 
TAREHE 8 APRILI, 2020

           Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
           Waheshimiwa Wajumbe wa Tume,
           Mkurugenzi wa Uchaguzi,
           Msajili wa Vyama vya Siasa,
           Viongozi wa Vyama vya Siasa,
           Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
           Inspekta  Jenerali  wa Polisi,
            Kamishna Mkuu wa Uhamiaji
           Watendaji wa Tume,
           Waandishi wa Habari,
Bwana Asifiwe!!!, Tumsifu Yesu Kristu!!!,  Assalam Aleykum!!!.         
Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, napenda kutumia fursa hii, kuwakaribisha katika mkutano huu muhimu ambao madhumuni yake ni kupeana mrejesho  wa yale tuliyojadiliana katika mkutano wetu wa terehe 23 Machi, 2020. Mkutano huo ulihusu  utekelezaji wa mazoezi ya  uwekaji wazi wa Daftari la Awali na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Awamu ya Pili.
Napenda pia kuwashukuru kwa mwitikio wenu wa kuhudhuria katika mkutano huu, licha ya majukumu mengi mliyonayo. Uwepo wenu ni muhimu  na Tume inauthamini sana.

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa,
Kama nilivyotangulia kusema  mkutano huu umelenga zaidi katika kuleta mrejesho wa yale yaliyojadiliwa katika mkutano uliopita. Mtakumbuka katika mkutano ule, Tume iliahidi kuyafanyia kazi maoni na  mapendekezo yenu kwa kukutana na kushauriana na wadau wengine na pia kuwapa taarifa juu ya mabadiliko yoyote yatakayoweza kutokea kabla ya Uboreshaji wa Daftari wa Awamu ya Pili. 

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa
Baada ya mashauriano  na wadau wakuu, Tume imeona vyema kuendelea na mazoezi hayo mawili kwa kuzingatia tahadhari  za kiafya kama inavyoshauriwa na Wataalam wa masuala hayo.
Tayari  Tume imenunua vifaa kinga vinavyotakiwa  kwa ajili ya kuchukua tahadhari za maambukizi ya ugonjwa wa COVID – 19 unaosababishwa na virusi vya Corona na tayari imetoa maelekezo kwa watendaji wa Uboreshaji kuzingatia miongozo ya afya.

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa,
Kama tulivyowataarifu katika Mkutano wetu uliopita, uwekaji wazi wa Daftari la Awali utafanyika sambamba  na Uboreshaji wa Daftari Awamu ya Pili.  Napenda kuwafahamisha kwamba, mazoezi hayo kama nilivyowataarifu kwenye mkutano uliopita, yataanza rasmi tarehe 17 Aprili, 2020.  Kwa mujibu wa ratiba mtakayopewa, mazoezi hayo yatakamilika tarehe 04 Mei, 2020 kwa Nchi nzima. 

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa,
Mazoezi ya Uwekaji wazi wa Daftari la Awali na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yatafanyika kwa siku tatu (3) tu kwenye kila Mkoa na katika route mbili badala ya route tatu zilizopangwa hapo awali na yatazingatia, wakati wote, tahadhari zinazoshauriwa na Serikali na Wataalam wa afya.

Katika Route ya kwanza  mazoezi haya yatafanyika kuanzia tarehe 17 Aprili  hadi tarehe 19 Aprili, 2020.  Jumla ya mikoa 12 na vituo vya uandikishaji Elfu mbili na tano (2005) vitahusika.  Katika Route hii ya kwanza, Mikoa itakayohusika ni:- Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Simiyu na Mwanza. Mikoa mingine ni; Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora.

Kwa upande wa Route ya pili  mazoezi haya yatafanyika kuanzia tarehe 02 Mei, hadi 04 Mei 2020.  Maeneo yanayohusika ni Tanzania Zanzibar  na mikoa 14 ya Tanzania Bara ambapo vituo vya kuandikisha wapiga kura vipatavyo Elfu mbili na moja (2001) vitahusika. Mikoa ya Tanzania Bara itakayofikiwa kwenye route ya pili ni Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Jumla ya vituo vya kuandikisha Wapiga Kura vitakavyotumika katika Awamu hii ni Elfu nne na sita (4006), badala ya vile Elfu nane na thelathini na moja (8031) tulivyowaeleza hapo awali. Kati ya hivyo, vituo Elfu tatu, mia tisa hamsini na sita (3,956) vitakuwa  Tanzania Bara na vituo Hamsini (50) vitakuwa Tanzania Zanzibar. Leo, Tume itawakabidhi orodha mpya ya vituo hivyo.  Orodha ya vituo vya uandikishaji mliyogawiwa kwenye Mkutano wetu wa tarehe 23/03/2020 haitatumika.



Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa
Uboreshaji huu utafanyika katika kila Kata ambapo kutakuwa na  Mwandishi Msaidizi na BVR Kit Operator ambao watakuwa na orodha ya vituo vyote katika Kata husika.  Watendaji hawa watakuwa na uwezo wa  kuboresha taarifa za Mpiga Kura yeyote  atakayefika kituoni.  Aidha, Mpiga Kura atakayefika kituoni ataandikishwa kulingana na kituo atakachopigia kura siku ya Uchaguzi Mkuu  wa mwaka huu ndani ya  Kata husika.

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa,
Kwa upande wa uwekaji wazi wa Daftari la Awali, Orodha ya wapiga kura itabandikwa katika kila kituo kilichotumika kuandikisha Wapiga Kura Awamu ya Kwanza.
Mpiga Kura ambaye atakuwa amehakiki taarifa zake na kuhitaji kufanyiwa marekebisho ama Mpiga Kura anayehitaji kumwekea pingamizi Mpiga Kura mwingine, atatakiwa kwenda kwenye kituo cha Kata husika kilichopangwa.
Zoezi hili la uwekaji wazi daftari litawahusu Wapiga Kura wote, wakiwemo wale walioandikishwa mwaka 2015 na wale walioandikishwa katika awamu ya kwanza ya Uboreshaji.


Aidha, utaratibu wa kuweka pingamizi kwa aliyeandikishwa utafanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 24 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kifungu cha 30(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa.  Mtu yeyote ambaye jina lake lipo kwenye Daftari la Awali la Mpiga Kura anaweza kuweka pingamizi dhidi ya kuendelea kuwepo kwa jina lake mwenyewe au jina la mtu mwingine yeyote iwapo mtu huyo atakuwa amepoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari au amefariki.
Vilevile, pingamizi la Uandikishwaji linaweza pia kuwekwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Afisa Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi.

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa,
Mpiga Kura anayetaka kuweka pingamizi atatakiwa kufika kituoni na kujaza fomu maalum ambayo inafahamika kama Fomu Na. 3B ambayo, pamoja na mambo mengine, itamtaka atoe sababu za kuweka pingamizi hilo.
Mweka Pingamizi anatakiwa kuwasilisha pingamizi ndani ya siku saba (7) kuanzia siku ya mwisho ya Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali katika eneo husika. Pingamizi hilo litafanyiwa kazi na Afisa Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi ndani ya siku saba (7) na kisha kutolewa uamuzi.
Uamuzi huo unaweza kukatiwa Rufaa katika Mahakama ya Wilaya na Mahakama hiyo inatakiwa kutoa uamuzi ndani ya siku 14 tangu tarehe ya Rufaa kupokelewa Mahakamani. Uamuzi wa mahakama hiyo ni wa mwisho.
Kimsingi, uwekaji wazi wa Daftari kama ilivyo kwa Uboreshaji wa Daftari utazingatia Sheria za Uchaguzi na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hizo.

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa,
Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha tena njia zitakazo tumika katika uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kama ifuatavyo:-

Kwanza, ni kwa Wapiga Kura wenyewe kufika katika vituo walivyojiandikisha na kuhakiki taarifa zao katika orodha itakayokuwa imebandikwa katika vituo hivyo.

Pili,  ni kwa kutumia Mfumo wa Voters’ Interaction Systems  (VIS), ambapo Mpiga kura kupitia simu yake ya kiganjani atapiga namba *152*00# na  kufuata maelekezo yatakayo mwezesha kuhakiki  taarifa zake. Huduma hii ni ya bure.

Vilevile, kwa kupitia Tovuti ya Tume (www.nec.go.tz), Mpiga kura atahakiki taarifa zake katika sehemu iliyoandikwa “uhakiki” na kuendelea kufuata maelekezo.

Tatu,  ni kupitia kituo cha Huduma kwa Wapiga Kura (Call centre) ambapo wananchi watapiga simu bure kupitia namba ya simu ya kituo ambayo ni 0800782100 na kupata usaidizi katika kuhakiki taarifa zao.

Tume imeweka njia zote hizo ili kuwapa urahisi Wapiga Kura wote kuhakiki taarifa zao.

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa
Kama mnavyofahamu, Tume hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu. Nitoe rai kwenu viongozi wa  Vyama vya Siasa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu za Uboreshaji na Uwekaji wazi wa Daftari la Awali.

Nawasisitiza  wananchi  waliojiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura mwaka 2015 na wale waliojiandikisha katika Uboreshaji wa Daftari Awamu ya Kwanza kujitokeza kwa wingi kuhakiki taarifa zao pindi Daftari litakapowekwa  wazi katika maeneo yao na watumie njia nyingine za uhakiki zilizoelezwa hapo juu. Pia watumie nafasi hiyo kuwawekea pingamizi wananchi wasio na sifa za kuwemo kwenye Daftari la Wapiga Kura.

Aidha, niwaombe wananchi hususan wale wenye sifa ya kujiandikisha kama Wapiga Kura wapya wasisubiri kujitokeza siku ya mwisho ya zoezi,  na hivyo kusababisha msongamano, bali wafike vituoni mara tu zoezi litakapowafikia; na watunze kadi zao.

Vilevile, ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuzingatia tahadhari za kiafya zilizowekwa katika vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID - 19 katika kipindi chote cha zoezi hili muhimu.

Ndugu Viongozi wa Vyama  vya  Siasa
Katika kuhitimisha, napenda  kuwashukuru tena kwa kuitikia wito wetu na kuhudhuria mkutano huu; na zaidi kwa ushirikiano wenu wa siku zote.

Baada ya kusema maneno hayo, sasa naomba kutamka kwamba mkutano wetu umefunguliwa rasmi.
  
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.