Habari za Punde

Jinsi taifa lenye Waislamu wengi zaidi duniani linavyokumbwa na hofu ya kuenea kwa virusi

Serikali imetoa marufuku ya usafiri kipindi hiki cha Ramadan kuanzia Ijumaa, 24 April
Kwa waislamu, Ramadhan ni kipindi muhimu cha mwaka. Muda wa kufanya sala na kuangazia zaidi familia.                                                                                          
Indonesia nchi ambayo ina Waislamu wengi zaidi duniani ni ada kwa raia wake kurejea vijijini walipokulia katika utamaduni unaofahamika kama mudik.
Licha ya janga la corona, mamilioni ya watu bado wanaendelea na safari zao kama walivyokuwa wamepanga awali.
Serikali imepiga marufuku kusafiri kuanzia Ijumaa, Aprili 24, lakini inahofiwa kwamba wengi tayari wameshaondoka au watasfiri tu katika kipindi cha siku chache zijazo, na kuhatarisha zaidi usambaaji wa virusi hivyo kwenye taifa ambalo ni la nne kwa idadi ya watu duniani.
Kufikia Jumanne, Aprili 21, Indonesia ilikuwa na visa 7,135 vya virusi vya corona na kurekodi vifo 616.
Wataalamu wengi wanaamini kwamba idadi kamili ya waliokufa ni ya juu zaidi ya hiyo kwasababu hadi kufikia sasa virusi vya corona vimesambaa kwa mataifa 34.
Asih sasa hivi yuko mwanzoni mwa miaka ya thelathini na anafanyakazi kama msafishaji mjini Jakarta.
Kwake yeye, ni jambo lisilowezekana eti kutotekeleza utamaduni wa 'mudik' yaani familia kukutana kwasababu hilo litafanya wazazi wake kuwa na huzuni mkubwa. Anapanga kurejea katika kijiji chake katikati ya Java.
"Natamani sana sherehe za Eid nikiwa pamoja na familia yangu. Huwa tunaomba pamoja siku ya Eid na kupika chakula maalum kama vile mchuzi wa kuku. Iwapo nitakosa kwenda nyumbani, itakuwa jambo la huzuni sana kwangu," anasema.
Asih na rafiki yake Sumi wanaishi katika chumba kidogo kwenye jengo la ghorofa nne katikati ya Jakarta. Kutokaribiana na jambo lisiloweza kuepukika.
"Bila shaka ninahofu kwamba naweza kupata maambukizi ya virusi vya corona," Asih amesema. "Ningesalia hapa kama ingewezekana lakini familia yangu yote imeniambia kwamba ni lazima niende nyumbani ama niwe ninataka au la."
Ili kuweza kujilinda yeye mwenyewe wakati wa safari yake ya saa 9 kuelekea kijijini, anasema kwamba atava barakoa na glavu.
Rafiki yake Sumi hana bahati. Amepoteza kazi yake kama yaya na anatafuta mbinu ya kusafiri kwenda kijijini.
"Nataka kuondoka Jakarta na kwenda kijijini kabisa. Sina uwezo wa kuendelea kuishi mjini, siwezi hata kulipa kodi ya nyumba," amesema.
Karibia watu milioni 1 tayari wameshaondoka Jakarta - kitovu cha maambukizi ya virusi vya corona na kurejea vijijini au miji yao ya nyumbani.
Watu wengine milioni moja 1.3 wanakadiriwa kuondoka kwenye mji huo kabla ya sikukuu ya Eid, ambayo huadhimisha kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Wasiwasi mkubwa ni kwamba tukio hilo linaweza kusababisha kusambaa zaidi kwa mlipuko huo maeneo mbalimbali ya vijijini.
Wataalamu wa afya wanaonya kwamba huenda ikawa janga hasa ikizingatiwa kwamba kuna upungufu wa vifaa vya kupimia virusi vya corona na vituo vya afya vyenye kutoa huduma bora katika maeneo ya vijijini.
"Utamaduni wa Mudik unaweza kusababisha kuongezeka kwa idadi ya waliolazwa hospitalini kwa Covid-19 kufikia 200,000," amesema daktari Pandu Riono, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza chuo kikuu cha Indonesia kitivo cha afya.
"Mwezi mtukufu wa Ramadan ulitakiwa kuwa wa furaha lakini baadhi yetu watakuwa hospitali na wengine kufa kwasababu ya hali ambazo kiuhakika tunaweza kuzizuia."
Kufika Julai, maambukizi yanatarajiwa kufikia milioni moja katika eneo la Java, kulingana na utafiti wa hivi karibuni na chuo kikuu cha Indonesia.
Huo ni wakati ambao wengi wanarejea baada ya mwezi wa Ramadhani. Mwaka jana, watu milioni 20 walisafiri makwao katika sikukuu ya Eid.
Kuhamasisha watu kuepuka kusafiri mwaka huu, serikali imeahirisha ile wiki moja ya sikukuu ya Eid hadi mwezi Desemba na imepiga marufuku wafanyakazi wa umma, jeshi na polisi kurejea makwao.
Lakini kupiga marufuku utamaduni wa mudik ni jambo ambalo litakasirisha raia wengi wa Indonesia.
"Sisi tuna ujamaa sana. Watu ambao wamehamia mijini ni wa vijijini, na pia ni wa jamii zao vijijini," anasema Imam Prasodjo, mwanasosholojia wa chuo kikuu cha Indonesia.
Marufuku ya serikali imetolewa kuchelewa na tayari Asih tayari yupo barabarani .
Kwa Sumi, ni wakati wa kujua namna ya kuendelea kuishi, anafahamu fika kwamba pesa zitamwishia iwapo ataendelea kuishi Jakarta.
Rafiki hao wawili wameahidi kuendelea kuwasiiana wakati ambapo Indonesia inaingia katika nyakati hatari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.