Habari za Punde

Waridi wa BBC: Mwanamke Aliyefukuzwa na Mume Wake Akiwa na Mtoto wa Wiki Moja

                Justina Syokau alifukuzwa na mume wake akiwa namtoto wa wiki moja
Justina Syokau amesifika sana kwa kibao chake kijulikanacho kama 'Twendy Twendy' ni mzaliwa wa Kaunti ya Machakos Kenya.
Justina alizaliwa katika mazingira ya wazazi waliokuwa ni muumini hasa wa dini hivyo basi mzizi wa malezi yake ya kikiristo ni tangu akiwa mtoto.
Justina Syokua alifungukia BBC Swahili na kusema kuwa ameyaonja maisha matamu ya ndoa na vilevile uchungu wa ndoa.
Justina Syokau alifunga ndoa na mwanamume ambaye alikuwa amemuwinda kimapenzi kwa muda mrefu, yule mwanamume hatimaye alifaulu kumshawishi kuwa yeye ndiye atakua mchumba wake wa maisha. Na Juni, 2012, walifunga pingu za maisha katika ndoa iliyojaa mbembwe na bashasha, asijue kuwa ndoa hiyo itakuwa ya muda mfupi tu na iliyojaa pandashuka chungu nzima.
Justina ambaye makao yake ni nchini Kenya, amekuwa muimbaji tangu siku zake za utotoni japo alianza kurekodi baada ya ndoa yake kuporomoka. Justina anaelezea kuwa ndoa yake ilianza kuingia dosari ghafla baada ya kufunga ndoa na barafu yake ya moyo. Baada ya fungate yao walirejea nyumbani akiwa na matumaini ya kupata kila aina ya raha lakini hali ilibadilika. Kulingana na Justina, mama yake mume wake pamoja na mashemeji zake waliokuwa wanaishi nao waliyafanya maisha yao kuwa magumu sana
''Mara tu baada ya ndoa mume wangu alianza kunizaba makofi, na kunitusi, kitu kidogo kingefanyika alianza kunirushia ngumi'' anasema Justina
Kwa hio hali hio ilimpa uwoga na hofu kuu lakini akaamua kuvumilia akiwa na matumaini kwamba mume wake huenda akabadilika.
Cha kusikitisha zaidi ni kwamba kadiri siku zilivyosonga mbele kiza kinene kiliendelea kutanda.
'' Wakati mwengine mume wangu alikuwa anasafiri kwa siku nyingi nisijue aliko, alikuwa ananiacha bila chakula wala pesa, cha ajabu ni kwamba alifuata maagizo ya mama yake kuliko ya kwangu, kwa kweli sikuwa na sauti katika ndoa yangu'' Justina anakumbuka.
Justina anasema kuwa mara nyingi mama mkwe wake alimzonga na wakati mwengine kumtusi hata machoni mwa mume wake lakini kilicho mshangaza, mumewe hakuna hatua zozote alizozichukua kumlinda.
Wakati ulipowadia kwa Justina kujifungua mtoto wao wa kwanza, alitakiwa kuwa na mfanyakazi wa kumsaidia kazi za nyumbani, kwasababu alihitaji kupona, Justina alijifungua kwa njia ya upasuaji.
Kulingana na Justina mambo yalibadilika mno aliporejea kutoka hospitalini na mtoto wake.
Mume wake pamoja na mkwewe walimbadilikia mno na kumtaka Justina afungashe virago. Justina anasema kuwa yule mjakazi aliyekuwa ametolewa kijijini kwao, aligeuka na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake.
'' Haikuwa siri, walikuwa wanapigiana simu na kucheza cheza kama wapenzi machoni mwangu,'' Justina anakumbuka.
Cha ajabu ni kuwa baada ya Justina kurejea kutoka hospitalini, mume wake alimuamrisha kufunga kuchukua kila kilicho chake na kuondoka, jambo ambalo Justina ilimchukua muda kulikubali na kujiuliza maswali mengi,
''Nikiondoka kwa mume wangu, watu watasema nini kuhusu kuvunjika kwa ndoa yangu?
'' Kama mkristo sikutaka watu kunisema kama mwanamke aliyeshindwa kutunza ndoa yake kwa hio niliona ni kheri nivumilie kuliko kuondoka '' Justina anasimulia .
Uhusiano kati ya yaya na mume wake ulikuwa sasa haufichiki kiasi kwamba mume wake alikuwa anashiriki ngono naye katika kitanda chao cha ndoa, isitoshe Justina anadai kuwa sio siku mmoja wala mbili, amewahi kuona ujumbe wa mapenzi kati yao kwenye simu ya mume wake.
Haikuwa muda kabla ya yule mjakazi kuanza kumuandama Justina, kwa kumsingizia kwamba amemrushia maneno machafu, kulingana na Justina yote hayo yalikuwa ya kusingiziwa tu mbele ya mume wake.
Justina anakumbuka jinsi alivyopewa kichapo cha mbwa na mume wake na kutupwa nje bila chochote zaidi ya nguo zake na za mtoto wake aliyekuwa mchanga .
Anasema hakuwa na mtu yeyote wa kumgeukia, na kwa miezi kadhaa ilibidi yeye na mtoto wake ambaye alikuwa na wiki moja tu kuishi mitaani bila sehemu maalum ya kulala wala wala kula .

'' Hakukuwa na sehemu ya kulala, na nilikuwa na tafuta chakula kwenye pipa, hakukuwa na mtu yeyote wa kunisaidia katika kipindi hicho kigumu maishani mwangu'' aliongezea Justina.
Justina anakumbuka kuwa alikutana na msamaria mwema akiwa mtaani na alimpa nauli ambayo ilimuwezesha kurejea alikozaliwa kijijini Machakos lakini pia kule kijijini hakupokelewa vyema kwani baadhi ya watu wa vijijini huwa na mtizamo tofauti kuhusiana na wanawake wanaotoka kwenye ndoa zao.
Kwa hio hakukaribishwa nyumbani kwao na muda mfupi baadae akaamua kuondoka kwenda kutafuta makaazi kwa rafiki yake mmoja waliokuwa wanashiriki naye kwenye kanisa moja.
'' Nilianza maisha mapya na kuamua kuingilia uimbaji wangu, nilirekodi nyimbo zangu na kuanza kuziuza mitaani na kwengineno huku nikiwa nimebeba mtoto wangu mgongoni ''anasema Justina.
Licha ya mengi yaliyofanyika maishani mwake , Justina Syokao amejizatiti kufanikisha ndoto yake ya uimbaji na pia ujumbe wale kwa wanawake ni kuwa, kwa kwenye mahusiano ambayo yanawaumiza hisia zao na kuwakosesha usingizi, wawe ni wenye kufanya maamuzi badala ya kuendelea kuteseka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.