Habari za Punde

KAMATI YA WAZIRI MPINA YABAINI MADUDU UJENZI WA MAABARA TAFIRI ATOA MAAGIZO MAZITO

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Petra Construction Co. Limited, Basem Abughalyoun (katikati) inayojenga Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kunduchi Dar es Salaam mara baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa ujenzi wa mradi huo. Kulia ni Mkurugenzi wa Uvuvi, Magesa Bulayi.
WAZIRI  wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (kushoto) akisisitiza jambo kwa Mkurugenzi wa Uvuvi, Magesa Bulayi (kulia) mara baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa ujenzi wa maabara ya Taasisi ya Uvuvi Kunduchi Dar es Salaam (katikati) Mkurugenzi wa Kampuni ya Petra Construction Co. Limited, Basem Abughalyoun inayojenga maabara

WAZIRI  wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina (katikati) akikagua baadhi ya miundombinu ya Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI. Dkt. Ismael Kimerei.  Kushoto ni Mwakilishi wa Petra Construction Limited, Nicholaus Mlay.

Na Mwandishi Wetu
KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kuchunguza Mradi wa Ujenzi wa Maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Kituo cha Dar es Saalaam imebaini ukikukwaji mkubwa wa Sheria pamoja na usimamizi dhaifu katika mradi huo na kuilazimu Serikali kufanya maamuzi magumu kutokana na kasoro zilizobainika. 

Hivyo Waziri Mpina amemuagiza Katibu Mkuu Uvuvi kutengua uteuzi wa Meneja wa Mradi wa Swiofish, Flora Luhanga kwa kushindwa kusimamia mradi huo huku akiagiza mkataba wa mshauri elekezi Kampuni ya Y&P Architect Limited kurejewa upya kwa kubadili kiasi cha fedha kilichowekwa kwenye mkataba kuwa sh. Milioni 600 badala ya sh. Bilioni 1.2 iliyopo kwenye mkataba wa sasa pamoja na kurejesha fedha za ziada alizolipwa kiasi cha shilingi milioni 352. 

Aidha ameagiza Mkandarasi Kampuni ya Petra Construction Limited akatwe fedha zote kwa mkupuo kwa malipo yanayofuata kiasi cha shilingi milioni 568 kwa kushindwa kuhuisha dhamana yake ya malipo ya awali na dhamana ya utekelezaji wa mradi na kutakiwa kulipa sh. Milioni 2.6 kila siku kutokana na kushindwa kukamilisha mradi kwa mujibu wa mkataba kuanzia Aprili, 21, 2020. 

Pia ametaka kiasi kitakachookolewa katika mradi huo cha zaidi ya shilingi milioni 500 kipangiwe matumizi mengine ya ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa majengo na miundombinu mingine muhimu ya Makao makuu ya TAFIRI. 

Akiwasilisha ripoti hiyo ya Kamati ya uchunguzi mbele ya Waziri Mpina, Kunduchi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uvuvi, Magesa Bulayi alisema kamati hiyo imebaini ukiukwaji mkubwa wa Sheria na Kanuni katika kumpata Mkandarasi Kampuni ya Petra Construction Company Limited na Mshauri Elekezi Kampuni ya Y&P Architect Limited. 

Alisema Kamati hiyo iliyoundwa na Waziri Mpina ilihusisha watalaamu wabobezi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) 

Hivyo Bulayi alisema Kamati ilibaini pia Kampuni ya Petra Construction Company Limited ilipewa kazi ya ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 2.6 huku ikiwa haina uwezo wa kifedha jambo ambalo limesababisha ujenzi wa mradi huo kusuasua na kukamilika asilimia 65 tu ambapo kwa mujibu wa mkataba mradi huo ulitakiwa kuwa umekamilika Aprili 20, 2020. 

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa dhamana ya malipo ya awali na dhamana ya utekelezaji wa mradi zenye thamani ya shilingi milioni 598 zimeisha muda wake tangu Machi 30, 2020 na Kampuni ya Petra Construction Company Limited haijahuisha dhamana hizo. 

Kamati pia ilibaini makosa ya ukokotoaji wa urejeshaji wa malipo ya awali ambapo hadi kufikia hati namba 4 ya malipo kiasi kilichokuwa kimelipwa kwa Serikali ni sh. Milioni 54 tu badala ya sh. Milioni 135. 

Bulayi alisema Kamati pia ilibaini kwamba mkandarasi Kampuni ya Petra Construction Company Limited aliahidi kwa mdomo kuokoa zaidi ya milioni 500 katika mradi huo jambo ambalo halikuwahi kuelezwa mahali popote wala kuanishwa maeneo ambayo fedha hizo zitaokolewa. 

Aidha Kamati ilitilia mashaka bei ya mzabuni mfano sh 800, 000 za unit price ya kabati la kupachika iliongezewa 0 kwa wino wa bluu katika nakala halisi ya makadirio ya ujenzi (BOQ) na kusomeka sh. 8, 000, 000 kinyume cha sheria za ununuzi. 

Pia Kamati ilibaini Mshauri Mwekelezi Kampuni ya Y&P Architect Limited iliyopewa kazi ya usanifu na usimamizi wa miradi ya Maabara ya TAFIRI Dar es Salaam, Ujenzi wa nyumba za Watumishi wa MPRU Tanga na Jengo la Utawala Mafia yenye thamani ya sh. Bilioni 4.5 lakini gharama ya Mtaalamu Mshauri huyo ni sh. Bilioni 1.2 sawa na asilimia 27.4. 

Kamati ilibaini kuwa gharama hizo ni kubwa ikilinganishwa na viwango vya ukomo vilivyowekwa na Bodi ya Wahandisi pamoja na Bodi ya Usanifu wa Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) ambapo gharama za Mshauri elekezi zinaanzia wastani wa asilimia 12.45 hadi asilimia 13.75 ya gharama za mradi lakini Kampuni ya Y&P ilipewa kwa asilimia 27.4 tofauti na kiwango kinachoruhusiwa. 

Bulayi alisema Kamati ya uchunguzi imeona gharama alizostahili kupewa Y&P ni sh. Milioni 601 badala ya sh. Bilioni 1.2 hivyo gharama ya mkataba ulioingiwa ni zaidi ya sh. Milioni 654 ikilinganishwa na mwongozo wa bodi. 

Kamati ilibaini gharama hizo ni kubwa ikilinganishwa na hali ya soko na kutolea mifano miradi ya ujenzi wa Soko la Ndugai, Stendi, Kituo cha kuegesha malori Nala na Kituo cha mapumziko Chinangali na Barabara za Mzunguko Dodoma chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia wenye thamani ya sh. Bilioni 87.7 lakini gharama ya usanifu na usimamizi ni sh. Bilioni 1.5 tu sawa na asilimia 1.7 ya gharama ya mradi. 
Pia Kamati imebaini ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake za Mwaka 2013 pia imeonesha kutozingatiwa kwa masharti yaliyowekwa katika zabuni na mikataba ambapo baadhi ya watumishi wanahusishwa na ukiukukwaji huo. 

Kufuatia ripoti hiyo, Waziri Mpina ameagiza uchunguzi zaidi wa vyombo vya dola ufanyike ili kujua ni kwa jinsi gani ukiukwaji huo mkubwa ulifanyika na kuonya kuwa fedha za umma haziwezi tena kutumika vibaya katika miradi inayotekelezwa kwenye wizara yake. 

Kwa upande wao Mwakilishi wa Mkandarasi wa Kampuni ya Petra Construction Limited, Vallency Assenga alisema sababu za kuchelewa kujenga mradi huo ni mvua zinazoendelea pamoja na mlipuko wa Corona huku Mwakilishi wa Mshauri Mwelekezi Kampuni ya Y&P Architect, Anna Shayo alidai kuwa tayari alishamkumbusha kwa barua mkandarasi kuhuisha dhamana yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.