Habari za Punde

Matumaini yafifia baada dawa ya remdesivir kugonga mwamba

Kumekuwa na matumaini makubwa kwamba dawa ya remdesivir ingeweza kutibu ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.
Dawa iliyokuwa ikitazamiwa kutibu virusi vya corona inaripotiwa kushindwa kufikia viwango vya ufanisi katika jaribio la kwanza la matibabu.
Kumekuwa na matumaini makubwa kwamba dawa ya remdesivir ingeweza kutibu ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.
Lakini jaribio la dawa hiyo nchini Uchina limeonesha kuwa dawa hiyo haikufanikiwa, kwa mujibu wa waraka uliochapishwa kimakosa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Dawa hiyo haikuboresha hali za wagonjwa au kupunguza kiwango cha virusi katika damu, ulisema waraka huo.
Kampuni ya Marekani inayotengeneza dawa hiyo, Gilead Sciences, imesema kuwa waraka huo ulipotosha uchunguzi wake.
Taarifa juu ya kushindwa kwa jaribio la dawa hiyo ilisambaa baada ya WHO kutuma maelezo katika kanzidata (hofadhi ya kumbukumbu za kimtandao) yake ya kitabibu , na baadae kuondosha data hizo.
WHO imethibitisha kuwa ripoti hiyo ya muswada iliwekwa mtandaoni kimakosa.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa watafiti waliwafanyia uchunguzi wagonjwa 137, wakawapatia dawa 158 na kulinganisha mafanikio na waliosalia 79, ambao walipewa dawa isiyo na kemikali ya placebo.
Baada ya mwezi mmoja, asilimia 13.9 ya wagonjwa waliokuwa wakipokea dawa hiyo walikufa ikilinganishwa na asilimia 12.8 ya wale waliopokea placebo. Jaribio lilisitishwa mapema kwa sababu ya madhara yake.
"Remdesivir haikuhusishwa na faida za kimatibabu wala za uchunguzi wa virusi ,"ulieleza muhtasari wa waraka huo.
Viwango vya hisa vilishuka katika masoko makuu matatu ya hisa nchini Marekani kwa zaidi ya 1% ya faida baada ya taarifa juu ya jaribio hilo kutangazwa.
"Tunaamini kuwa taarifa iliyotumwa ilijumuisha data zisizofaa kuhusu utafiti," msemaji wa kampuni ya Gilead alisema na kuongeza kuwa utafiti ulisitishwa mapema kutokana na kujitokeza kwa watu wachache kushiriki na hivyo takwimu zake hazikuwa na maana.
''Kutokana na hilo, matokeo hayakukamilika ingawa kile kilichojitokeza katika data kinaonesha uwezekano wa faida ya dawa ya remdesivir, hususani miongoni mwa wagonjwa waliotibiwa katika hatua za mapema za ugonjwa," alisema.
Hii haina maana ni mwisho wa safari wa dawa hiyo, hata hivyo majaribio kadhaa yanayoendelea yatatoa picha ya wazi kuhusu matumizi ya dawa hiyo.
Chanzo cha Habari.BBC.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.