Habari za Punde

RC Wangabo asisitiza watumishi kutoa elimu ya Corona hadi vijijini baada ya wananchi na vijana wengi kutofuatilia vyombo vya habari

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akipimwa hali yake ya joto la mwili kabla ya kuingia katika ofisi za kituo cha Uhamiaji kilichopo katika mpaka wa Kasesya unaotenganisha nchi ya Tanzania na Zambia,uliopo kata ya Itete, Wilayani Kalambo.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maelekezo kwa maafisa wa uhamiaji pamoja na watumishi wa mpaka wa Kasesya unaotenganisha nchi ya Tanzania na Zambia kuhakikisha wananchi wanaotumia mpaka huo wanazingatia usafi. 
Mkuu wa mkoa wa Rukwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama wakitoka katika geti (nyuma yao) linalotenganisha mpaka wa Tanzania na Zambia baada ya kutembelea mpaka huo na kujiridhisha juu ya udhibiti wa utumiaji wa mpaka huo kwa watanzania na wazambia. 
Afisa Afya wa Wilaya ya kalambo Richard Manuma (Kulia) akitoa maelezo juu ya maandalizia ya hema linalotumika kwaajili ya kuwaweka Karantini siku 14 wasafiri wanaotumia mpaka wa Kasesya unaotenganisha nchi ya Tanzania na Zambia katika Wilaya ya Kalambo mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto).

Na.Abdulrahaman Salim -Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameitaka Kamati ya maafa ya Mkoa kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa, Kata, Tarafa hadi Mkoa huku akisisitiza mkazo wa kutolewa kwa elimu hiyo uelekezwe kwa vijana ambao wengi wao wanaonekana kutofuatilia taarifa za habari pamoja na elimu mbalimbali zinazotolewa na vyombo vya habari juu ya ugonjwa wa Corona.
Amesema kuwa vijana wa kisasa kuanzia mjini mapaka vijijini wamekuwa wagumu kusikiliza taarifa ya habari kwenye redio wala kuangalia taarifa ya habari kwenye runinga zaidi ya kujiendekeza kusikiliza muziki bila ya kujali na kutaka kujua serikali inasema nini juu ya kujikinga na maradhi hayo ya Corona.
“Akitembea kuna vitu viko masikioni humu anasikiliza muziki tu, nini serikali inasema kuhusu janga hili hajui, lakini mambo haya yanazungumwa sana kwenye redio, yanasemwa sana kwenye televisheni zetu, program ziko nyingi lakini vijana na kundi kubwa wanaonekana hawana muda wa kufuatilia, tuwarudishe hili kundi kubwa, lijenge tabia ya kufuatilia nini kinazungumzwa kwenye redio, kila redio inazungumza, ziko redio za ndani ziko redio zenye sura ya kitaifa,” Alisisitiza.
Aliongeza kuwa hii inaweza kuwa vita ya tatu ya dunia isipokuwa adui hatumuoni hivyo hatuna budi kila mmoja kwa nafasi yake akaendeleza kutoa elimu bila ya kuchoka ili kuweza kupambana na adui huyu ambaye haijulikani lini atashindwa.
Ameyaongea hayo wakati alipofanya kikao na kamati ya maafa ya mkoa iliyowajumuisha waganga wakuu wa wilaya wakiongozwa na mganga mkuu wa mkoa, viongozi wa dini na wataalamu wa ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya jamii wa mkoa na taasisi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na kutoa elimu za afya katika mkoa.
Aidha, Alisisitiza ili kuweza kufanikisha kufikisha elimu kwa wananchi wote wa mkoa huo hakuna budi kuwaelimisha viongozi wa ngazi zote wakiwemo wenyeviti wote wa vijiji na mitaa ili watilie mkazo utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika maeneo yao ya kiutawala.
Kuhusu ulinzi wa Mipakani Mh. Wangabo alisema kuwa Mkoa wa Rukwa una vipengo 50 katika ziwa Tanyanyika ambavyo hutumika na wananchi wan hi ya jirani ya Kongo na hivyo kuwataka wananchi kuwa makini na wavuvi wote wanaotoka katika nchi hiyo kuhakikisha wanawarudisha walikotoka na kisha kuripoti kwa vyombo vya usalama na kusisitiza kuwa wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuwa walinzi wa kwanza wa usalama wa nchi yetu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.