Habari za Punde

Uganda Yatazamia Kudhibiti Corona Kwa Kuwazuia Madereva wa Kenya na Tanzania.

 
Rais Museveni amesema kwa sasa usafiri wa malori ya mizigo ni changamoto kubwa kwa nchi yake.

Idadi ya wagonjwa nchini Uganda imeongezeka na kufikia 74. Lakini ongezeko hilo si la raia wa Uganda bali madereva kutoka nchi jirani za Kenya na Tanzania.
Katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona serikali ya Uganda imefunga mipaka yake na kusimamia marufuku ya wananchi kutoka nje.
Hata hivyo, mipaka ya nchi hiyo ipo wazi kwa sekta ya uchukuzi na hutegemea zaidi mizigo kutoka Kenya (kupitia mpaka wa Malaba kutokea bandari ya Mombasa) na Tanzania (kupitia mpaka wa Mutukula kutokea bandari ya Dar es Salaam).
Kwa siku mbili zilizopita, madereva 13 (Watanzania wanane, Wakenya watano) wamegundulika kuwa na virusi hivyo baada ya kuingia Uganda.
Hii leo Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa tayari waziri wake wa afya yupo kwenye mazungumzo na mawaziri wa Afya kutafuta suluhu ya suala hilo la usafiri wa malori ambalo amelitaja kuwa ndio tatizo kubwa zaidi kwa Uganda kwa sasa.
"Tunahitaji mizigo iingie, lakini wakati huohuo hatuihitaji ugonjwa (wa virusi vya corona)," amenukuliwa Museveni katika ukurasa wa Twitter wa runinga ya NBS.
Museveni leo amesema baada ya kushughulika ipasavyo na mipaka ya anga, sasa hatua inayofuata ni kushughulikia pia mipaka ya ardhini na nchi jirani ili kuendelea kuzuia kasi ya maambukizi.
Maafisa waandamizi wa serikali ya Uganda wamekuwa wakinukuliwa wiki hii kuwa wanataka madereva kutoka Kenya na Tanzania kuacha magari mpakani.
Baada ya kuyaacha hapo yatachukuliwa na madereva wa Uganda ambao watayapeleka mpaka mwisho wa safari.
Hii leo Museveni amethibitisha mpango huo akisema mawaziri wa afyawatalijadili hilo.
"Kubadili madereva, Maedreva kutoka Kenya waendeshe mpaka mpakani kisha magari kupulizwa dawa na madereva wengine (wa Uganda) kuyachukua kutokea hapo. Hili pia mawaziri watalijadili," ameema Museveni.
Pia Uganda inataka madereva hao kupimwa kbla ya kutoka katika nchi zao.
Hatua nyengine ambayo Uganda inapanga kuitekeleza kwa sasa ni kuhakikisha wanawapima madereva wote kutoka nchi jirani na kuwaruhusu kuendelea na safari pale tu majibu yatakapotoka na kuonesha hawana maambukizi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uganda Jenerali Jeje Odongo jana Alhamisi amewaambia waandishi wa habari kuwa serikali ilikuwa inapanga kutumia vipimo vya haraka kuwapima madereva hao.
"Vipimo vya haraka vinatumia dakika 10 tu kutoa majibu, lakini changamoto yake ni kuwa kipimo kimoja ni dola 65 na kwa wastani siku moja magari 1,000 huingia Uganda.
Wiki iliyopita rais Museveni aliongeza marufuku ya kutotoka nje kwa siku 21 zaida ana kusema kuwa hatua zote zilizotangazwa ilipotangazwa marufuku ya awali zitaendelea kama kawaida.
Hatua hizo ni pamoja na kuzuia kabisa mikusanyiko ya watu. Nyumba za ibada na taasisi zote za elimu zitaendelea kufungwa.
Watu pekee watakaoruhusiwa kutoka na kuendelea na shughuli zao ni wafanyakazi katika sekta muhimu kama afya, ulinzi na usalama, wafanyakazi wa benki na wanahabari.
Amri ya kutokutoka nje nchini Uganda inasimamiwa na vyombo vya ulinzi
Usafiri wa umma na wa ndege za abiria pia umepigwa marufuku.
Magari ya mizigo pamoja na ndege za mizigo zinaruhusiwa kuendelea na shughuli zake. Hata hivyo marubani na wasidizi wao katika ndege za mizigo watawekwa katika maeneo maalumu chini ya uangalizi wa serikali.
Chanzo cha Habari BBC News.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.