Habari za Punde

Wanasayansi wa Uingereza Wanataka Chanjo Yao Kufanyiwa Majaribio Kenya

Mkuu wa shirika la Afya Duniani Dkt Tedros Adhanom Ghebreyes amesema kwamba bara la Afrika halitakuwa uwanja wa majaribio ya chanjo ya corona
Watafiti kutoka nchini Uingereza wanafikiria kufanyia majaribio chanjo ya virusi vya corona nchini Kenya ambapo kulingana na wao mlipuko wa ugonjwa huo unaongezeka.
Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya Shirika la Afya duniani kuyaonya mataifa ya Ulaya kwamba bara la Afrika sio uwanja wa majaribio ya chanjo.
Mkuu wa Shirika hilo Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus alilaani kauli alizoziita za "kibaguzi" kutoka kwa madaktari wawili wa Ufaransa ambao walitaka chanjo ya virusi vya corona kufanyiwa majaribio barani Afrika.

"Afrika sio na haitakuwa uwanja wa majaribio ya chanjo yoyote," alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Hatahivyo wanasayansi hao kutoka Chuo kikuu cha Oxford wanadaiwa kufikiria wazo hilo iwapo hawatopata matokeo ya haraka nchini Uingereza.
Chanjo hiyo inajulikana kutoa antobody yenye nguvu, lakini hilo halimaanishi kwamba inaweza kuwa kinga.
''Tutalazimika kuhitaji chanjo chungu nzima , kuna nyingi zinazofanyiwa majaribio hivyobasi tutahitaji dozi nyingi na tutarajie mjadala mkubwa kuhusu ni mataifa gani ama ni kundi lipi la watu linalohitaji chanjo hiyo kwanza'', alisema mwandishi wa BBC wa maswala ya tiba Fergus Walsh.
Alikuwa akizungumza katika runinga ya BBC News ambapo mtangazaji Sophie Raworth alimtaka kutoa mtazamo wake kuhusu ufanisi wa chanjo hiyo.
Walsh alijibu akisema kuna umuhimu kuwa makini na ahadi zinazotolewa kutokana na kile alichokitaja kuwa hamu ya chanjo hiyo kufanya kazi.
Hatahivyo, kulingana na Walsh, kundi hilo la Oxford lina rekodi nzuri ya kipindi cha miaka 30 iliopita ambapo limefanikiwa kutengeneza chanjo zilizofanikiwa dhidi ya aina nyengine ya virusi vya corona kama vile MERS, ambayo imefanikiwa katika majaribio yaliofanyiwa katika miili ya binadamu.
Hatahivyo kuna maswali kuhusu uamuzi wa kufanyia majaribio chanjo hiyo nchini Kenya licha ya wagonjwa wachache wa virusi hivyo kuripotiwa nchini humo.
Kufikia Alhamisi tarehe 23 Aprili, kulikuwa na wagonjwa 320 walioripotiwa katika taifa hilo la Afrika mashariki.
Mapema siku ya Alhamisi, majaribio ya kwanza katika mwili wa mwanadamu barani Ulaya yalianza Oxford katika kile ambacho vyombo vya habari vya Uingereza vimetaja kuwa wakati muhimu.
Watu wawili waliojitolea, wote wakiwa wanasayansi walichomwa sindano ya chanjo na ndio watu wa kwanza kati ya zaidi ya watu 800 walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 55 ambao walichaguliwa kufanyiwa utafiti huo.
Mtu wa kwanza kujitolea alitambulika kuwa mwanasayansi kwa jina Elisa Granato aliye katika idara ya wanyama katika chuo kikuu cha Oxford.
''Mimi ni mwanasayansi na nataka kusaidia sayansi, kwa uwezo wangu wote na kwasababu sifanyi utafiti wa virusi, nilihisi hii ndio jinsi ninavyoweza kusaidia katika utafiti huu. Ndio maana niko hapa na nafurahia'', alimwambia Walsh.
Nusu ya kundi hilo litapokea chanjo ya Covid 19 huku nusu nynegine ikipokea chanjo ya udhibiti ambayo inalinda dhidi ya ugonjwa wa menenitis lakini matokeo yake hayatajulikana kwa miezi kadhaa.
Katika mjadala kwenye runinga ya ufaransa ya channel LCI, Dkt Camille Locht, mkuu wa utafiti kutoka shirika la utafiti wa afya la Inserm alikuwa akiongelea juu ya majaribio ya chanjo barani Ulaya na Australia.
Dkt Jean-Paul Mira,mkuu wa kitengo cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Cochin ya jijini Paris, kisha akasema: "Nichokoze kitu, siyo kwamba tunatakiwa kufanya utafiti huu Afrika, ambako hakuna barakoa, hakuna matibabu wala huduma ya nusu kaputi?
Huku hayo yakijiri, dawa iliyokuwa ikitazamiwa kutibu virusi vya corona inaripotiwa kushindwa kufikia viwango vya ufanisi katika jaribio la kwanza la matibabu.
Kumekuwa na matumaini makubwa kwamba dawa ya remdesivir ingeweza kutibu ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.
Lakini jaribio la dawa hiyo nchini Uchina limeonesha kuwa dawa hiyo haikufanikiwa, kwa mujibu wa waraka uliochapishwa kimakosa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Dawa hiyo haikuboresha hali za wagonjwa au kupunguza kiwango cha virusi katika damu, ulisema waraka huo.
Kampuni ya Marekani inayotengeneza dawa hiyo, Gilead Sciences, imesema kuwa waraka huo ulipotosha uchunguzi wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.