Habari za Punde

Watu 'Bilioni Moja' Huenda Wakaambukizwa Kote Duniani - Yasema IRC

Shirika la ICRC linaamini kwamba tayari raia wengi wanakufa kwa ugonjwa wa Covid-19 ingawa sio hospitalini.
Watu bilioni moja huenda wakaambukizwa virusi vya corona kote duniani na mambo pengine yabadilike, nchi zisizojiweza zinahitaji usaidizi wa haraka, Shirika la kutoa msaada limeonya.
Kamati ya Shirika la Kimataifa la Kutoa Misaada (IRC) limesema kwamba msaada wa kifedha na kibinadamu vinahitajika kusaidia kupunguza kasi ya usambaaji wa virusi vya corona.
Shirika hilo limesema nchi zinazokabiliwa na vita kama Afghanistan na Syria zinahitaji msaada wa dharura wa kifedha kuzuia mlipuko wa ugonjwa wa corona.
"Muda uliosalia kuimarisha hali ni mchache mno," Shirika hilo limeonya.
Kumekuwa na zaidi ya watu milioni 3 walioambukizwa ugonjwa wa Covid-19 kote duniani huku zaidi ya vifo 200,000 vikithibitishwa, kulingana na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins Marekani.
Ripoti ya shirika hilo, ambayo inazingatia data za Shirika la Afya Duniani (WHO) na chuo cha Imperial College London, ilikadiria kwamba kunaweza kuwa na maambukizi kati ya milioni 500 na bilioni 1 kote duniani.
Pia imesema kwamba huenda idadi ya vifo ikawa ni milioni 3 katika nchi zinazokumbwa na migogoro na zisizokuwa na uthabiti.
"Idadi hiyo inastahili kutufungua macho," amesema mkuu wa shirika la IRC, David Miliband.
"Maafa ya janga hili bado hayajashuhudiwa sana katika nchi zilizoathirika na vita," ameongeza. "Cha msingi sasa ni kwa wafadhili kutenga pesa kwa nchi zinazokumbwa na vita.
"Serikali zinastahili kushirikiana kuondoa kizuizi chochote dhidi ya msaada wa kibinadamu."
Maelezo haya yanatokana na data za mara kwa mara kutoka Chuo kikuu cha Johns Hopkins na huenda yasiangazie hali halisi ya mambo yalivyo katika kila nchi.
Chanzo: Chuo kikuu cha Johns Hopkins (Baltimore, Marekani), maafisa wa eneo
Takwimu zilizowekwa mara ya mwisho 28 Aprili 2020, 19:07 GMT +1
Shirika hilo lenye makao yake Marekani ambalo hutoa msaada wa kibinadamu kote duniani, limesema kwamba mambo mengine kama ukubwa wa nyumba, idadi ya watu, kiwango cha huduma za afya na migogoro ya awali huenda vikaongeza hatari ya kutokea kwa mlipuko wa virusi vya corona kwa nchi zinazoendelea.
Idadi rasmi ya walioambukizwa ama kufa kwa virusi vya corona katika nchi zinazoendelea ni ya chini lakini kuna uwezekano mkubwa idadi hiyo kiuhalisia ikawa ni ya juu.
Caroline Seguin, anayesimamia miradi ya kimatibabu nchini Yemen kupitia shirika la kimatababu lisilokuwa na mipaka, anasema shirika hilo linaamini kwamba tayari raia wamekufa kwa ugonjwa wa Covid-19 ingawa sio hospitalini.
"Tunaamini kwamba maambukizi ya ndani kwa ndani yanaendelea lakini kiwango cha wanao pimbwa kiko chini sana," ameiambia BBC.
Bi Seguin amesema Yemen, ambayo iliangaziwa katika ripoti iliyotolewa na shirika la IRC, imeonyeshwa kama nchi iliyo katika hatari zaidi ya kuathirika vibaya na virusi vya corona na kuongeza kwamba tayari nchi hiyo imeathirika vibaya na milipuko mingine ya hivi karibuni kama kuhara na ukambi/surua.
"Mfumo wa afya umeshindwa kabisa kufanyakazi… na bila shaka wizara ya afya haiwezi kukabiliana na virusi vya corona," amesema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.