WITO umetolewa kwa wananchi kupewa moyo kutokana na wengi
wao kufuata maelekezo ya kupambana na maradhi yanayosababishwa na virusi vya
Corona na kwa wale waliokuwa hawajaelewa wametakiwa kuelimishwa juu ya kupambana
na janga hilo.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa wito huo hivi
karibuni huko katika Ikulu ndogo,
Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, wakati alipofanya mazungumzo na Viongozi wa
Mikoa miwili ya Pemba katika ziara yake
ya siku tatu aliyoifanya kisiwani humo.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alieleza kuwa wananchi walio wengi wameonesha muitikio katika
kupambana na maradhi hayo kutokana na kufuata maelekezo yanatotolewa na
wataalamu wa afya pamoja na viongozi wao.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa wananchi wengi hivi sasa wamekuwa wakifaa barkoa, wakitumia maji ya
kutiririka na sababu pamoja na vitakasa mikono na maelekezo mengine ya
kupambana na janga hilo, hivyo ni vyema wakapewa moyo kwa juhudi zao hizo.
Aliongeza kuwa kwa
wale ambao bado hawajaelewa, Rais Dk. Shein aliwataka viongozi wote hapa nchini
kuendelea na juhudi na mikakati yao ya kuwapa elimu ya kupambana na maradhi
hayo kwa njia mbali mbali ili ujumbe huo uweze kuwafikia.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa licha ya juhudi na miongozo inayotolewa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kupiti wataalamu wake wa afya pamoja na viongozi wake bado wapo
wananchi ambao wanakaidi maelekezo hayo hivyo, ni vyema wakaendelea kuepwa
elimu, miongozo na maelekezo juu ya janga hilo.
Hivyo, Rais Dk. Shein
aliwataka viongozi wote hapa nchini kuendelea kuwapa elimu wananchi katika
maeneo mbali mbali hasa vijijini na ikiwa bado elimu haijafika vyema watumiwe
hata wataalamu wa sekta ya afya ili waende kutoa elimu hiyo kwa azma ya
kupambana na maradhi hayo thakili.
Aidha, Rais Dk. Shein
alipongeza mikakati iliyowekwa na viongozi wa serikali pamoja na wataalamu wa sekta
ya afya hapa nchini na kusisitiza haja ya kupewa msukumo kwa wananchi kwani
wapo walioanza kuelewa na wapo ambao bado elimu hiyo haijawafikia ama
imewafikia lakini bado hawajaanza kuifuata.
Mnamo Machi 25, mwaka
huu wakati akitembelea eneo linalotarajiwa kujengwa jengo la Uchunguzi wa Virusi vya maradhi makuu
lililopo ndani ya Taasisi ya Afya huko Binguni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini
Unguja Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kuacha ukaidi na kufuata kikamilifu
maelekezo ya Serikali, ikiwa ni hatua za kuunga mkono juhudi za kukabiliana na
Virusi vinavyosababisha maradhi ya Corona.
Katika maelezo yake siku hiyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika
kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo, Serikali tayari imetowa malekezo kadhaa,
ikiwa njia ya kujikinga na virusi vya ugonjwa huo, hivyo akawataka wananchi
kuacha ukaidi na kutekeleza maelekezo katika kupambana na janga hilo.
Aliongeza kuwa uwepo wa Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona ni
janga na Kimataifa na ni maradhi yasiotaka mzaha wala hayachaguwi aina ya mtu
wa kuamuathiri, hivyo ni vyema wananchi wakaondokana na ukaidi na badala yake
wafuate maelekezo ya Serikali pamoja na wataalamu wa afya.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment