Habari za Punde

Kutoka Barazani: Hotuba ya maoni ya kamati ya sheria, utawala bora na idara maalum


HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA SHERIA, UTAWALA BORA NA IDARA MAALUM KUHUSIANA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA,
KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021
                                                                       
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, ninachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu kwa kutujaalia uzima na afya njema ambavyo vimetuwezesha kukutana tena katika Baraza hili Tukufu, kwa ajili ya kuendelea na shughuli zetu za kuwatumikia wananchi wetu. Aidha, ninakushukuru wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote kwa kuliongoza Baraza hili kwa ufanisi na nina imani kwamba mtaendelea kuliongoza Baraza hili kwa uadilifu wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuiongoza nchi yetu kwa uadilifu na kuhakikisha kuwa maendeleo makubwa yanapatikana pamoja na kuendelea kudumu kwa amani na utulivu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia, sina budi kumshukuru Waziri wa Katiba na Sheria mheshimiwa Khamis Juma Mwalim pamoja na watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu ndugu George Joseph Kazi. Aidha, Kamati inatoa shukurani zake za dhati kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mheshimiwa Said Hassan Said, Naibu Mwanasheria Mkuu, ndugu Mzee Ali Haji pamoja na watendaji wao kwa mashirikiano mazuri waliyoyatoa kwa Kamati katika kipindi chote bila ya kuwasahau watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa mashirikiano waliyotupatia wakati wa kupitia makadirio ya Bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, aidha, ninachukua fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yetu kwa mashirikiano makubwa wanayonipatia katika kutekeleza majukumu ya Kamati yetu na kuhakikisha kuwa thamani halisi ya fedha inapatikana katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima, naomba kuwatambua Wajumbe hao kwa majina kama ifuatavyo:

1.     
Mhe. Machano Othman Said
Mwenyekiti
2.     
Mhe. Zulfa Mmaka Omara
Makamu Mwenyekiti
3.     
Mhe. Ali Khamis Bakar
Mjumbe
4.     
Mhe. Salma Mussa Bilal
Mjumbe
5.     
Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed
Mjumbe
6.     
Mhe. Suleiman Makame Ali
Mjumbe
7.     
Mhe. Maryam Thani Juma
Mjumbe
8.     
Ndg. Ali Alawy Ali
Katibu, na
9.     
Ndg. Haji Jecha Salim
Katibu

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo sasa naomba nichukue fursa hii adhimu kutekeleza jukumu langu la msingi lililonileta mbele ya Baraza lako Tukufu.

FUNGU G 01: WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria, katika mwaka wa fedha 2020/2021 inategemea kutekeleza Programu kuu tatu (3) na Programu ndogo tano (5) pamoja na mafungu manne (4) yanayojitegemea, licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbali inazozikabili zikiwemo uhaba na ubovu wa baadhi ya ofisi zake kama vile majengo ya Mahakama mbali mbali Unguja na Pemba, uhaba wa vyombo vya usafiri na uhaba wa vitendea kazi katika sehemu mbali mbali katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imeridhishwa sana na utekelezaji wa programu za Wizara ya Katiba na Sheria baada ya kuona kuwa taasisi zinazohusika na utetekelezaji na usimamizi wa masuala ya haki zimepiga hatua kubwa ya kundeleza usimamizi wa haki katika jamii. Aidha, Kamati imeridhishwa sana na utendaji wa Ofisi ya Mufti pamoja na kutoa elimu ya masuala ya dini ya Kiislamu ikiwemo ndoa na talaka katika jamii.

Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena, Kamati yangu inatoa masikitiko yake juu ya ukosefu wa gari kwa ajili ya mheshimiwa Mufti Mkuu wa Zanzibar jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele na Baraza lako hili tukufu kila inapowasilishwa Bajeti ya Wizara hii katika kila mwaka wa fedha. Kamati inaishauri Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kulipa uzito suala hili kwani muda umekuwa mrefu na changamoto hii bado haijapatiwa ufumbuzi.
FUNGU G 02: MAHAKAMA KUU

Mheshimiwa Spika, Mahakama ni miongoni mwa mihimili mikuu ya nchi inayotarajiwa kuimarisha na kuongeza upatikanaji wa haki, kuheshimu utawala wa sheria, kuzingatia haki za msingi za binadamu na ushirikishwaji wa shughuli za kidemokrasia nchini pamoja na kujenga misingi imara ya Utawala Bora.

Mheshimiwa Spika, Kamati inaishauri Serikali kufanya juhudi za kukamilisha jengo la Mahakama kuu Tunguu katika muda uliopangwa. Hata hivyo, bado kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga au kuyafanyia matengenezo baadhi ya majengo ya mahakama ambayo kwa kiasi kikubwa hayalingani na hadhi yake, Mahakama nyingi za Mikoa na Wilaya ziko katika hali mbaya kimiundombinu ikiwemo Mahakama ya Wete na Mkokotoni.

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inashauri uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na Afisi ya Mwanasheria Mkuu kufanya tathmini kwa wahitimu wanaotoka katika Chuo cha Skuli ya Sheria Zanzibar katika kila mwaka ili kuona kama lengo lililokusudiwa linafikiwa au kuna marekebisho yanapaswa kufanywa baada ya kuona uwezo wa wahitimu hao.

FUNGU G 03: AFISI YA MWANASHERIA MKUU

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Afisi ya Mwanasheria Mkuu miongoni mwa majukumu yake ya msingi ni kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na Taasisi zake, kuandaa Miswada, Kanuni na matangazo ya kisheria pamoja na kuiwakilisha Serikali Mahakamani kwenye kesi zote za madai dhidi ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Afisi ya Mwanasheria Mkuu imeweka programu ndogo ya Kutoa Ushauri wa Kisheria, Kutayarisha na Kusimamia Mikataba ya Serikali;programu ambayo kimsingi utekelezaji wake unatimiza lengo kuu la kuanzishwa kwa Afisi hii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, Kamati inatoa shukrani na pongezi za dhati kabisa kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuipitia na kurekebisha sheria mbali mbali nchini ambapo mchango wake ni mkubwa katika kujenga misingi ya demokrasia.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Kamati imeridhishwa na uanzishwaji wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Gombani, Pemba jambo ambalo litawarahisishia wananchi na wakaazi wa Pemba kupata huduma za kisheria kwa wakati na bila ya usumbufu wowote. Vile vile, Kamati yetu imeridhika na utendaji wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusimamia majukumu yake na hivyo tunaomba wazidi kutekeleza majukumu yao ya kuisaidia Serikali ili kuzidi kuimarisha utawala wa haki na sheria.

FUNGU G 04: OFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, miongoni mwa majukumu yake ni kuendesha mashtaka Mahakamani, kutoa ushauri wa kisheria na maelekezo juu ya haki za jinai. Ofisi hii inatarajia kuongeza upatikanaji wa haki, kuheshimu utawala wa sheria, kukuza haki za binadamu na kukuza ushiriki wa kidemokrasia nchini.

Mheshimiwa Spika, vile vile, Kamati inaipongeza kwa dhati Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa juhudi zake za kuiwakilisha Serikali katika kesi za jinai na kupelekea kupungua kwa mrundikano wa kesi Mahakamani hususani kesi za udhalilishaji wa wanawake na watoto ambazo katika kipindi cha hivi karibuni matendo hayo yameongezeka mara dufu.

FUNGU G 05: TUME YA KUREKEBISHA SHERIA

Mheshimiwa Spika, Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar ina jukumu kuu la kuzifanyia mapitio ya sheria nchini ambapo imedhamiria kuzifanyia sheria mbali mbali mabadiliko ili ziende sambamba na mabadiliko ya mazingira na wakati.

Kamati imeridhishwa na utendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kazi nzuri wanazozitekeleza katika kipindi hiki ambapo baadhi ya sheria amabazo ni za muda mrefu na hazikuwahi kufanyiwa mapitio wamezipitia na kuweza kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa ajili ya kupitishwa na kufanywa sheria bora zinazoendana na wakati.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha maoni machache ya Kamati yangu kwa niaba ya Kamati pamoja na kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu kwa kunisikiliza kwa umakini wakati wote wa uwasilishaji wa maoni yetu.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa,ili kufikiwa malengo yaliyopangwa katika utekelezaji wa majukumu yake, Kamati inawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu waichangie na wairidhie Bajeti hii na hatimae waiidhinishie Wizara ya Katiba na Sheria makadirio na makisio ya fedha zote zilizopangwa kutumiwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kamati yangu Naomba Kuunga Mkono Hoja.

Ahsante,
(Mhe. Suleiman Makame Ali )
Mjumbe,
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.