Habari za Punde

Makala: Majiko Sanifu yanavyosaidia kuhifadhi mazingira

 MMOJA ya akinamama wanaotumia majiko sanifu kwa kupikia, akipanga kuni katika jiko hilo ili kuweza kupikia, jiko ambalo ni rafiki mkubwa wa mazingira.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)

MMOJA ya watumiaji wa majiko sanifu katika kupikia, aliyejulikana kwa jina la Asha Khamis akiongeza kuni katika jiko hilo, wakati alipokuwa akipika wali jiko sanifu ni rafiki mkubwa wa mazingira kwa kutokutumia kuni nyingi.(PICHA NA ABDI SULEIMAN

 JIKO la mawe matatu ambalo hutumia kuni nyingi na kuharibu mazingira kama linavyoonekana katika picha, katika siku za hivi karibuni limekuwa likitoweka kutokana na uwepo wa majiko sanifu yan ayotumia kuni kidogo na rafiki wa mazingira.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
 BAADHI ya mizigo ya kuni ikiwa chini kwenye uwanja wa nyumba baada ya kurudi kukata bondeni, kwa ajili ya kutumia kwa kupikia.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
 BAADHI ya kuni ambazo hutumika kwa ajili ya bekari za mikate, zikiwa zimekusanywa nje ya bekari hiyo kwa ajili ya matumizi.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)

BAADHI ya majiko sanifu yakiwa tayari yameshatengenezwa kwa ajili ya kutumika majumbani, ambapo jiko moja huzwa kati ya shilingi 5000.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)

NA ABDI SULEIMAN.

NI MAJIRA ya saa 7:30 za mchana, nikiwa katika kijiji cha kambini Kichokochwe, huku jua kikali kikiwaka mithili ya hakujanyesha mvua.
Hapa nakutana Asha Omar Hamdan (46) mama wa watoto wanne, kwa sasa anatumia jiko sanifu katika shughuli zake kupikia nyumbani, baada ya kupata maradhi katika utumia jiko la mawe matatu.
“Hebu tizama nilivyoathirika kutokana na jiko, hili la mawe matatu moto wake mkali sana wakati unapipikia, macho yamepiga wekundu na mwili kazi kuwasha kila wakati”alisema.
Asha alisema hakua na lakufanya kwani hata wazazi wake wametumia jiko la mawe matatu kupikia, lakini baada ya kuona hali kwake imekua ngumu, amelazimika kutafuta jiko sanifu katika matumizi yake ya nyumbani.
Jiko sanifu la kuni mbili ni katika majiko bora ya kupikia, jiko halitowi moshi wala moto wake hauathiri mili kutokana na kutoka sehemu moja na sio kama jiko la mawe matatu.
Amesema uzuri wa jiko sanifu linatumia kuni kidogo, halichafuwi sufuria pia linaivisha haraka chakula kama kuchemsha chai dakika nane (8) baada ya moto kushika, huku jiko la mawe matatu ndani ya dakika 10.
Ali Khamis Ahemde (56) ni mume wa biasha, anasema baada ya biasha kulalamika kwa muda mrefu na kutumia dawa mbali mbali, kwa kutibu muwasho na kupona ndipo alipoamua kutumia jiko sanifu katika matumizi yake ya kupikia.
Alisema uwepo wa jiko hilo limeweza hata kumpunguzia mzigo mkubwa wa kwenda kutafuta kunia, ndani ya mwezi mmoja alikuwa anakwenda mara mbili kutafuta kunia.
Ikumbukwe kuwa kabla ya kuwepo kwa majiko sanifu, misitu ilikuwa katika hali mbaya sana, kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni za kupikia, ambapo zaidi ya hekta  1000 zinapote kila mwaka, kwa mujibu wa mkuu wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Pemba Said Juma.
WANAOPIKIA MAJIKO SANIFU WANAYAPI WAO.
Fatma Shaame Hamad mkaazi wa kambini Wilaya ya Wete, amesema majiko sanifu ni majiko mazuri na rafiki mkubwa wa misitu, majiko haya hutumia kuni moja au mbili au tatu katika matumizi yake ni tofauti na majiko ya mawe matatu ambayo yanatumia kuni nyingi.
“Hebu tizama hili jiko linavowaka hapa nimetia kuni 12, kila upande kuni nne kama ingekuwa jiko sanifu jee, nimeshamaliza kupika dakika nane tu kama unachemsha samaki, kuni chache tu na unamaliza haraka sana kupika”amesema”
Ashura Mzee Haji mkazi wa kiungoni, miaka mitatu sasa bado anatumia jiko sanifu katika shughuli zake za kupikia, huku akiwa na matumizi madogo ya kuni.
“Mimi nimeshazowea kutumia majiko haya tena, yanaivishamara moja chakula, wala halichafui sufuria kwa moshi kama majiko yale ya mawe matatu ambayo yanatumia kuni nyingi” alisema Ashura.
Kuni tunazoenda kutafuta kwa sasa zinatusaidia sana, kabla ya jiko hili sanifu kila baada ya siku nne tukatafute kuni, sasa hivi tunafika wiki mbili hatuendi kutafuta tena kunia.
Kombo Khamis Ali mkaazi wa shengejuu, majiko sanifu yamempunguzia usumbufu wa kwenda kutafuta kuni, muda mwingi sasa anafanya shughuli zake kutokana na jiko hilo kutumia kuni kidogo.
“Ilikuwa tunatumia zaid ya masaa mawili kwenda kutafuta kuni, kila wiki tunarudi tena mbondeni kukata kuni, inafika wakati tunafukuzana na watu wa misitu, kama kuni ndogo ndogo hakuna unakata japo mti mbichi unaenda kuuwandika ukikauka unatumia”aliongeza.
   WATENGENEZAJI WA MAJIKO SANIFU WANASEMAJE
Salama Khalfan Khamis mtengenezaji wa majiko sanifu kijiji cha Sahengejuu, alisema kwa sasa soko la majiko yameshuka, kutokana na wananchi wengi kupata elimu ya kutengeneza wenyewe.
Amesema kuwa jiko hilo moja huuzwa kati ya shilingi shilingi elfu 5000, kwati haya ya mawe matatu mtu hutengeneza tu, lakini jiko sanifu ni bora zaidi hata kupikia kuliko la mawe matatu, sanifu sufuria linakaa bila ya hofu wakati hili jengine mtumiaji anapawa kuliweka kwa uwangalifu sufuria.
Majiko sanifu yanafaida nyingi, hutumia kuni kidogo, huhifadhi mazingira katika suala la ukataji wa miti, gari moja ya Ng’ombe hupakia koroja tatu, koroja moja huwa na vigogo 20, ambapo ukichanja kwa shoka korja moja kwa jiko sanifu unatumia mwezi mmoja na nusu, kwa jiko la mawe matatu ni wiki tatu.
Mwajuma Hamad Hamad anasema ugumu wa utengenezaji wa jiko hilo, ni upatikanaji wa udogo tu, ambao hulazimika kuufata sehemu za mbali na hutumia gari za Ng’ombe katika kubebea.
“Hili jiko halina tabu sana katika utengenezaji panahitajika udongo, unaochanganywa na maji, bati la kuwekewa kiwango cha jiko kulingana na bei dogo shilingi elfu 5000 na kubwa 8000, wala halitumii muda mrefu kutengeneza ikiwa mahitaji yamekamilika ni dakika 10 hadi 15 kwa jiko moja, baadae linachomwa na moto ili kuwa imara zaidi”amesema.
Kwa sasa changamoto kubwa ni upatikanaji wa udongo tu, kwa sasa udongo waliokuwa wakitumia umechanganyika na maji chumvi.
Katika kukabiliana na ukataji wa miti, tumelazimika kupanda miti mingi ya jamii na imekuwa  misitu mzuri, yote ni kutokana na makubaliano kama tukiendelea kuharibu misitu kwa ukataji wa kuni mwisho kutakua na jangwa.
            VIONGOZI WA ASASI ZA KIRAIA WANASEMAJE
Mkurugenzi Mtendaji wa Community Forest Pemba, Mbarouk Mussa Omar amesema, sababu iliyopelekea kuwa na mradi wa kutengeneza majiko sanifu na banifu, kutokana na uharibifu wa mazingira, kwa upoteaji wa rasilimali ya misitu imekuwa ni kubwa.
Sababu nyengine muda ni mkubwa ambao wanaoutumia akinamama, baba na vijana kwa ajili ya kutafuta kuni na misitu ya asili imeshapotea, huku nguvu nyingi na muda mkubwa unatumika katika utafutaji wa kuni.
Amesema sabubu ya tatu ni misitu mingi ya asili Kisiwani Pemba, imeshapotea na haya majiko ni marafiki mkubwa wa mazingira na  misitu itaweza kurudi katika haiba yake.
“majiko sanifu yanatumia kuni chache, kwa mfano kuni mbili, tatu hata moja na unaweza kupikia nyungu zako zote na moshi pia hautoki, tafauti na kutumia majiko ya mafya matatu yanayotumia kuni nyingi”amesema.
“Majiko haya pande zote unaweza kutia kuni na sio rafiki kimazingira, moshi mwingi unatoka hupelekea kuathiri hata macho kutoka meupe na kuwa mekundu”ameongeza.
Tuliyalenga maeneo 18 lakini baada ya kuonekana elimu inahitajika zaidi, juu ya matumizi ya majiko sanifu tumefkia maeneo 36, sisi hatukurudi nyuma lengo letu kuyafanya mazingira kuwa salama.
“Tuliweza kutengeneza majiko sanifu 1738, katika utekelezaji wa mradi kuna maeneo tayari wananchi wameenza kupanda miti ya matunda kuhifadhi uharibifu na kuepuka mabadiliko tabia nchi”alifafanua Mbarouk.
 Jumuiya ya Sanaa, Elimu ya Ukimwi na Mazingira (JISEUMA) kisiwa Panza, imesema majiko sanifu ni rafiki wa mazingira na yanasaidia kurudisha haiba ya misitu ambayo imepotea kwa kiasi kikubwa.
“Miti mingi imepotea huku kisiwani kwetu ilifika hadi makaburi yalifikwa na maji ya chumvi, kutokana wananchi kukata miti ya mikoko kwa wingi kwa shuhuli za kijamii, ikiwemo kupikia au kujengea n ahata kwa ajili ya mkaa”alisema.
Katibu wa jumuiya hiyo Juma Ali Mati amesema wamelazimika kupanda miti zaidi  ya 50000, katika maeneo mbali mbali ili kurudisha haiba ya asili ya kisiwa, sasa wananchi wanatumia majiko hayo kwa shughuli zao za kupikia, licha yaw engine bado kuendelea kutumia majiko ya mafia matatu.
Kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) lengo namba 15, lnazungumzia kulinda, kuanzisha na kuboresha matumizi endelevu ya mifumo ya ikolojia, kwa kufanya menejiment ya misitu kukabili majanga.
“Hekta Milioni 13 za misitu hutoweka kila mwaka, huku watu Milioni 1.6 hutegemea misitu kwa maisha yao ikiwemo wenyeji wa misitu Milioni 70” kwa mujibu wa SDGs lengo namba 15.
Kwa mujibu wa hutuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha za Wizara ya Kilimo Maliasili na Uvuvu Zanzibar, mwaka wa fedha 2018/2029 Waziri Rasshidi Ali Juma, alisema takwimu zinazonyeha ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya kuni, kutoka mita za jazo 19,532,25 mwaka 2016, hadi kufikia mita za ujazo 23,114 mwaka 2017.
Hii inatokana na wananchi wengi wa Unguja  na Pemba kuelekeza nguvu zao katika matumizi ya majiko ya mawe matatu, bekari za mikate kuendelea kutumia kuni.
      VIONGOZI WA SERIKALI WANASEMAJE JUU YA MAJIKO SANIFU
Mwalim Khamis Mwalim, Mkuu wa Idara ya Mazingira Pemba, amesema matumizi ya majiko sanifu yana umuhimu mkubwa hususan katika Kisiwa cha Pemba, imetokana na uwepo wa ukataji wa miti hovyo, wakat kipindi cha nyuma sehemu nyingi miti iliharibiwa kutokana na sababu ya upatikanaji wa nishati ya kupikia.
“Majiko sanifu yanatumia kuni kidogo, miti mingene inabakia kwa kuendelea kuhifadhi mazingira, kwa sasa hali ya kimazingira ilivyo, mwamko ni mkubwa wa upandaji wa miti hususana miti ya kisasa, kama mivinje na miti ya asili inaendelea kupitia vikundi vingi vya uhifadhi wa mzingira”amesema.
Moshi ni mchanganyiko wa gesi mbali mbali mtu anapovuta moshi kwa muda mrefu, maradhi mbali mbali ikiwemo muwasho, macho kuwa wekundu yote ni kutokana na utumiaji wa majiko ya mawe matatu.
Wakati umefika sasa kwa wananchi kutumia majiko sanifu, ili kupunguza matumizi ya muda mrefu kwenda kutafuta kuni, ungeweza kufanya shuhuli nyengine, pamoja na kulinda afya zao.
Mkuu wa Idara ya Misiru na Malia Asili zisizorejesheka Pemba, Said Juma Said amesema majiko sanifu yana umuhimu mkubwa sana kwa wananchi wa kisiwa cha Pemba, katika suala la la uhifadhi wa mazingira inatokana na wananchi miaka mingi wakitumia majiko ya  mawe matatu
Majiko hayo yanatumia kuni nyingi, hivyo ukataji wa misitu umekuwa ni mkubwa sana kwa kuni za kupikia, kuwepo kwa majiko sanifu yamesaidia kuhifadhi mazingira kwa kutumia kuni kidogo na kuwepo matumizi endelevu ya misitu.
“Majiko haya yanasaidia uhifadhi wa misitu na kuwa endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo”alisema.
Majiko mkombozi ni miongoni mwa majiko sanifu, mkombozi zaidi yamejengwa kwenye taasisi za ulinzi, pamoja na skuli zenye mabweni ya kulalia wanafunzi kutokana taasisi hizo kutumia kuni kwa wingi, wakati jiko mkombozi hatumii kuni sana.
Mpaka sasa kuna vijiji vimenufaika na majiko sanifu kama vile Makangale, Mjini Wingwi, Tumbe, Wingwi Mtemani, Kiuyu kwa manda, Gando, Kambini, Kiungoni, Kengeja, Wambaa, Makoongwe, ambapo zaidi ya majiko 200 yameshagawiwa katika vijiji hivyo.
Kwa mujibu wa mkuu wa idara ya misitu na Malili zisizorejesheka Pemba, imesema zaidi ya majiko sanifu 5000 watu wanatumia kwa sasa, baada ya kupatiwa elimu mbali mbali juu ya matumizi ya majiko hayo, huku Mkoa wa Kaskazini Pemba ukiongoza kwa matumizi ya majiko sanifu.
Kwa mujibu wa utafiti wa Woody Biomass wa mwaka 2013, uliofanywa na Wizara ya Kilimo Mali asili zanzibar, kupitia idara ya Misitu na Rasilimali,  imesema eneo la Zanzibar ni karibu  2 653 km 2 (Unguja 1 583 km 2 na Pemba 1 070 km 2 ).
Kwa mujibu wa sensa ya watu na wenyeji wa Zanzibar ni 1 303 569 (sensa ya kitaifa 2012) na kiwango cha ukuaji wa sensa ya wastani wa asilimia 2.8%  ni saizi ya familia ya watu 5 kwa mmoja, rasilimali za misitu inachukuwa  jukumu muhimu katika maisha ya kila siku ya watu kupata nishati kupikia, ujenzi wa mbao, utalii, lishe, vyanzo vya maji, malazi ya wanyama wa porini na milango ya maeneo ya ufugaji samaki.
“Mmahitaji misitu Zanzibar ni  ya kisheria chini ya kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Usimamizi na Uhifadhi wa Misitu no. 10 ya 1996. Msitu wa Zanzibar”ulisema utafiti huo.
Kiasi cha kuni nchini Zanzibar kinaendelea kupungua wakati idadi ya miti ikiongezeka, kiasi cha   8 633 290 m3 (mita qub) wakati Unguja ni 5 523 536 m3 na kwa Pemba  ni 3 109 754 m3  kwa mwaka 1997,  wakati mwaka 2013 Unguja kulikuwa 5 782 500 m3  na  Pemba ilikuwa 4 488 300 m3 .
Mratib wa kitengo cha elimu ya afya Pemba Dr Hamad Hamad Simba asema kuwa moja ya kemikali hatari iliyomo ndani ya moshi ni carbonda oxaid, nchi za Ulaya hutumika sana kama sumu ikiambatana na kemikali nyingine.
Amesema unapowasha moto wa kuni pele moshi unapotoka ule wa kwanza wenyewe vipande vidogo vidogo vinavyopaa angani, vinaathari kubwa ndani ya mwili unapovuta hewa hewa unaweza kupata magonjwa mbali mbali ikiwemo muwasho machoni, maradhi ya moyo, kutiririka mafua, kifua na kiharusi.
Alisema wataalamu wanatafautiana lakini wapo wanaosema karibu watu elfu 30,000, hufariki duniani kila mwaka kutokana na moshi wa jikoni, huku waathirika zaidi ni mama wajawazito, watoto wadogo, watoto wachanga na wazee.
HITIMISHO.
Sasa wakati umefika kwa jamii kujikita zaid katika matumizi ya majiko sanifu yanayotumia kuni chake chake za kupikia, kwa mautumia ya majumbani pamoja na bekari za mikate kutumia nishati mbala ikiwemo nishati ya umeme, ili kupunguza wimbi kubwa la ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni, taasisi na idara husika wakati umefika kuendelea kuelimisha jamii na viongozi wa bekari za mikate, kila kukicha miti inapotea itafika wakati Kisiwa cha pemba kitakuwa ni jangwa kwa ukataji wa miti kwa ajili ya kuni.
EMAIL:abdi suleiman33@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.