Habari za Punde

ZEC yazindua kamati ya maadili ya uchaguzi mkuu 2020

 Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ZEC Mhe. MABRUKI JABU MAKAME kushoto alipokuwa akijiandaa kuzungumza kabla ya kuzindua kamati ya maadili. kamati ya Maadili ya Uchaguzi imeundwa na Wajumbe wanaowakilisha vyama vya Siasa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Mjumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa kwa upande wa Ofisi ya Zanzibar. 


Na Jaala Makame Haji-ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC tarehe 27/6/2020 imezindua kamati ya maadili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 iliyoanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 65(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 4 ya mwaka 2018 ambacho kinaitaka Tume kwa kushauriana na vyama vya siasa, Msajili wa vyama vya siasa na mamlaka ya Serikali kutayarisha Kanuni za maadili ya kuongoza shughuli za vyama na Wadau wengine katika Uchaguzi.

Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kamati hiyo, Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ZEC Mhe. MABRUKI JABU MAKAME aliwaomba wadau wa Uchaguzi ambao wanaunda kamati hiyo kukaa pamoja na kujipangia mipango mizuri kulingana na Sheria zilizopo ili kuona kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 unafanyika kwa mafanikio makubwa.

Mhe. Mabruki alisema kuwa, Tume ya Uchaguzi ina imani kuwa wananchi watayafuata maelekezo ya vyama vyao endepo kila mjumbe wa kamati hiyo atawajibika ipasavyo katika kutekeleza wajibu wake.

Alifahamisha kuwa, kamati hiyo ya maadili ya Uchaguzi ni miongoni mwa kamati sita zilizoundwa na ZEC ili kupata ushauri juu ya masuala mbalimbali katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar THABIT IDAROUS FAINA alizitaja kamati hizo ambazo ni pamoja na kamati ya fedha, ununuzi na usambazaji wa vifaa, kamati ya elimu ya wapiga kura, kamati ya ulinzi, usalama na vyombo vya dola, kamati ya mawasiliano na vyombo vya habari na kamati ya kuratibu shughuli za waangalizi wa uchaguzi.

Mkurugenzi FAINA, alieleza kuwa, miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo ni kuandaa kanuni za Uchaguzi pamoja na kuzisimamia ili kila mdau wa Uchaguzi aweze kupata haki yake ya kushiriki katika uchaguzi uliohuru, wa haki na uwazi.

Aidha Mkurugenzi huyo, alisisitiza kuwa wajumbe wa kamati za ushauri katika uchaguzi Mkuu ni washauri wazuri wa Tume katika kuendesha Uchaguzi unaozingatia misingi ya kidemokrasia kwa kila mwananchi.

Alifafanua kuwa, kamati ya Maadili ya Uchaguzi imeundwa na Wajumbe wanaowakilisha vyama vya Siasa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Mjumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa kwa upande wa Ofisi ya Zanzibar.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hassan Nassir Ali aliwaomba wananchi kuondoa hofu katika kipindi cha Uchaguzi na kuwaomba viongozi wa Vyama vya siasa ambao ni wajumbe wa kamati ya maadili kutii viapo vyao katika kamati hiyo na kufuata yale wanayoelekezwa katika kanuni za maadili ya Uchaguzi.

Naibu Msajili wa vyama vya Siasa kwa upande wa Zanzibar Muhammed Ali Ahmedi aliviasa vyama vya siasa ambavyo vimeshiriki katika kamati hiyo kuwa msitari wa mbele katika kuzisimamia kanuni za maadili ya Uchaguzi, kuzilinda na kuzitangaza kwa wananchi, viongozi wenzao wa vyama vya siasa pamoj na vyombo vya dola.

Nao wajumbe wa kamati hiyo waliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuunda kamati za ushauri kwa madhumuni ya kuweka mustakbali mzuri wa kudumisha amani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

1 comment:

  1. Hatutaki uchaguzi wenye manufaa makubwa, tunataka uchaguzi huru na haki tu

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.