Habari za Punde

Diwani wa Kata ya Chanika Atetea Kiti Chake Kwa Kishindo.

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.
Aliyekuwa Diwani wa kata ya Chanika kwa miaka mitano iliyopita Ndg.Chihumpu Abdallah Juma leo ametetea kiti chake kwa kuibuka na ushindi wa kura 80 kati ya kura 102 zilizopigwa na Wajumbe wa Kamati Kuu ya Kata hiyo, ambapo jumla ya wajumbe 103 walipiga kura na moja kuharibika.

Awali akinadi sera na kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika kugombea Udiwani wa kata hiyo katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Octoba, Chihumpu alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano aliyokuwa madarakani aliweza kutekeleza ilani ya Chama kwa asilimia zisizopungua 95.

Chihumpu alieleza kwamba kama kuna eneo ambalo halijafanyiwa utekelezaji ni asilimia chache hivyo kuomba ridhaa ya kupatiwa nafasi hiyo ili kukamilisha pale palipobaki kwa kushirikiana na serikali kuu.

"Wajumbe nyie wenyewe ni mashahidi, mnaona maendeleo yaliyopo ambayo yamekuja ndani ya kipindi cha miaka mitano mliponipa ridhaa ya kuwa diwani ndani ya kata yetu, kila eneo utekelezaji umefanyika hivyo basi nipeni tena ruhusa ya kuongoza miaka mingine mitano ili kumalizia pale palipobaki" alisema Chihumpu.

Aidha alitoa wito kwa wajumbe hao kutoa taarifa za wahalifu endapo sehemu yoyote ya kutolea huduma za jamii kutakuwa na michezo michafu kwa wahudumu kuomba fedha kwa wananchi waliotakiwa kupata huduma bure ambapo kauli hiyo aliitoa baada ya mjumbe mmoja kumuhoji kuhusu huduma ya afya kwa mama mjamzito ambayo imedaiwa kutolewa huku wakina mama hao kutozwa fedha za matibabu.

"Pale hospitalini, kama kuna daktari au muhudumu wa afya anamchaji mama mjamzito pesa ni kosa, tupeane taarifa kwa hili, Rais wetu ametoa kipaumbele kwa wananchi masikini kupata haki yao ya msingi, kama kuna mtu anakwenda kinyume tutamshuhulikia" alibainisha.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wilayani Waliogombea nafasi hiyo katika kata hiyo jumla walikuwa saba ambao aliwataja kuwa ni Ramadhani Majoho kura 2, Sonyo Selemani kura 4, Abdallah Kidato kura 1, Asina Dhahabu kura 6, Abdi Mwinjuma kura 6 na Chihumpu Abdallah kura 80.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.