Habari za Punde

Madiwani 8 Watetea Nafasi Zao na Watatu Wapoteza Nafasi Zao Halmashauri ya Mji wa Handeni Tanga.

Na. Halima  Kamchalla, HANDENI.
MADIWANI 8 kati 11 waliomaliza muda wao katika halmashauri ya mji wa Handeni walitia nia ya kuwania tena nafasi hizo na kufanikiwa kutetea viti vyao kwa kuwashinda watia nia wenzao ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akitoa matokeo ya jumla ya kata zote 12 za halmashauri hiyo Jana katika ofisi ya chama mjini Handeni, Katibu wa CCM wilayani humo Salehe Kikweo alisema kuwa kata 11 za halmashauri hiyo zilikuwa zikiongozwa na madiwani wa CCM huku kata moja ikishikiliwa na mpinzani kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Kikweo alisema kuwa madiwani 9 walioongoza kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita wamefanikiwa kurudi huku madiwani watatu wakishindwa kutetea viti vyao na nafasi zao kuchukuliwa na watia nia wengine ndani ya chama ambao wajumbe waliwachagua wakiamini watafanikiwa kuipeperusha vema bendera ya chama hicho mwezi Octoba kwenye uchaguzi mkuu baada ya mchujo kumalizika ndani ya chama.

"Tunashukuru uchaguzi wa kura za maoni kwa wagombea wetu ndani ya chama umemalizika salama huku waliopata nafasi wengi ni wale waliotetea viti vyao ndani ya halmashauri, tuna jumla ya kata 12 Ccm tulikuwa na madiwani 11 na mmoja wa kata ya Mabanda alikuwa cuf" alifafanua.

Alizitaja kata hizo kuwa ni Chanika, Kwenjugo, Vibaoni, Msasa, Mdoe, Kwamagome, Mlimani, Malezi, Kwediyamba, Konje, Kidereko na Mabada.

Aidha alifafanua kwamba kata ya Chanika ilikuwa na wagombea 7 na kura ziliopigwa ni 103, Chihumpu Abdallah aliibuka na ushindi wa kura 80, kata ya Kwenjugo wagombea 8 kura zimepigwa 110 na Twaha Mgaya alipata ushindi wa kura 39, kata ya Malezi wagombea 7 kura zilizopigwa 107 Shabani Kitombo aliibuka na kura 74, wakati kata ya Mdoe wagombea 16 kura zilipigwa 71 na mshindi ni Mwishashi Ulenge aliyepata kura 19.

Kata ya Kwediyamba wagombea watano na kura zilipigwa 74 mshindi ni Salehe Sebo kura 39, kata ya Kwamagome wagombea wanne kura zilipigwa 182 Mussa Mkombati aliibuka na kura 126 kata ya Msasa wagombea 8 kura zilipigwa 81 na mshindi ni Hoseni Khatibu kura 43, kata ya Kidereko wagombea 11 kura zilipigwa 90 na Godfrey Munga aliibuka na kura 61.

Kikweo alisema kata hizo wagombea wake walioshinda ndio waliotetea viti vyao na kuongeza kuwa kata ambazo zimechukuliwa na watia nia wapya ni Konje ambayo ilikuwa na wagombea 12 na kura zilipigwa 94 ambapo mshindi alikuwa ni Siri Mikael aliyepa kura 39 na diwani aliyeshindwa kutetea kiti chake Manyendi Kigoda akiambulia kura moja.

Kata nyingine ni Vibaoni wagombea 17 kura zilipigwa 76 na Ramadhani Kuyugu aliibuka na kura 35 na aliyeshindwa kutetea kiti chake Athumani Muhando alipata kura moja huku kata ya Mlimani wagombea walikuwa 11 kura 79 ambapo Amiri Mwaliko alipata kura 42 na kumuondoa diwani aliyeshindwa kutetea kiti chake Mwajabu Mhina aliyepata kura 26.

Kata ya Mabada ambayo ilikuwa ikiongozwa na diwani wa CUF Masoud Mhina ilikuwa na wagombea 10 na wapiga kura 101 ambapo Salehe Mwaliko aliongoza kwa kupata kura 43 huku mshindi wa pili aliibuka na kura 19 ambaye ni Eliyasa Mwedi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.