Katibu wa Mufti Zanzibar Shekh Khalid Ali Mfaume akitoa maelekezo kwa Walimu Wakuu wa vyuo vya Quran na Viongozi wa Taasisi za kidini wa Wilaya ya Mjini, Ofisini kwake Mazizini, baada ya vyuo vya Quran na Madrasa kufunguliwa .
Mkuu wa Fatwa wa Ofisi ya Mufti Zanzibar Shekh Nouman Jongo akitoa nasaha kwa Walimu Wakuu wa vyuo vya Quran na Viongozi wa Taasisi za kidini wa Wilaya ya Mjini huko katika Ukumbi wa Ofisi ya Mufti Mazizini.
Kiongozi wa Jumuiya ya kuhifadhisha Quran Zanzibar Maalim Suleiman Omar Baramia akipokea Mashine ya Printa kutoka kwa Katibu wa Mufti Zanzibar Shekh Khalid Ali Mfaume ili isaidie kazi zao, huko katika Ukumbi wa Ofisi ya Mufti Mazizini Unguja
Baadhi ya Walimu Wakuu wa Vyuo vya Quran na Viongozi wa Taasisi za kidini wa Wilaya ya Mjini Unguja wakifuatilia nasaha zilizokuwa zikitolewa na Maafisa Waandamizi wa Ofisi ya Mufti Zanzibar, Ofisini kwao Mazizini Unguja .
PICHA ZOTE NA YUSSUF SIMAI MAELEZO ZANZIBAR .
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar
Katibu wa Mufti Zanzibar Shekh Khalid Ali Mfaume amewataka Viongozi na Walimu Wakuu wa Vyuo vya Quran kufuata maelekezo ya Wataalamu wa Afya ili kuepukana na maambukizi ya maradhi ya Corona baada ya kufunguliwa Vyuo vya Quran .
Aliyasema hayo Ofisini kwake Mazizini wakati akizungumza na Walimu Wakuu wa vyuo vya Quran na Viongozi wa Taasisi za kidini wa Wilaya ya Mjini
Amesema si vyema Walimu na Viongozi wa vyuo vya Quran kupuuza maelekezo ya wataalamu wa afya kwani Corona bado ipo ingawa maambukizi yamepungua kwa kiasi kikubwa .
Alifahamisha kuwa madrasa nyingi za Zanzibar hazina nafasi ya kutosha kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi katika madarasa ya kusomea hali inayoweza kuchangia kutokea maambukizi ya maradhi ya Corona .
Amewataka Viongozi wa Vyuo vya Quran kuweka vitakasa mikono au maji na sabuni ili wanafunzi wanapoingia na kutoka waweze kunawa pamoja na kuandaa utaratibu mzuri wa kukaa wakati wa masomo yao .
Alieleza kuwa Ofisi ya Mufti ililazimika kuchelewa kufungua Vyuo vya Qurani ili kuangalia mwenendo mzima wa maradhi ya Corona ambayo yanaambukiza kwa haraka hasa panapo kuwa na mkusanyiko wa watu wengi .
Katibu wa Mufti aliwashauri Viongozi wa Vyuo kuwa na subra linapotokezea tatizo ni vyema Waislamu kukaa pamoja na kulitafutia ufumbuzi kwa pamoja .
Mkuu wa Fatwa kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar Shekh Nouman Jongo aliwataka viongozi wa dini kufuata maadili ya kazi zao kwani ni sehemu ya Wazazi na Walezi wa Watoto.
‘Inasikitisha na inatia aibu kwa Mwalimu wa Madrasa kufanya vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi wake,”alisema Shekh Nouman Jongo.
Amesema vitendo hivyo vinaondosha heshima ya Walimu na Viongozi wa Dini ya Kiislamu na kuwajengea hofu Wazazi wanaopeleka Watoto wao Vyuoni.
Aliwashauri Walimu na Viongozi hao kuwa kigezo cha vitendo vyema ili kujenga imani katika jamii .
Katika Mkutano huo Ofisi ya Mufti imetoa Printa sabini kwa Madrasa mbali mbali pamoja na Misahafu inayotarajiwa kusambazwa Zanzibar nzima .
No comments:
Post a Comment