Habari za Punde

WACHANGIAJI DAMU KUZAWADIWA JEZI MPYA ZA SIMBA NA YANGA

Mfanyabiashara Azim Dewj akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuwahamasisha Wananchi na Wanamichezo kuchangia Damu akiwa na wawakilishi wa Taasisi, Mkurugenzi wa tiba MOI Dkt Samuel Swai, Muwakilishi wa GsM Eng Herth Said pamoja na muwakilishi wa kampuni ya Romarid Sports 2010 Ltd wakiwa pamoja katika  mkutano na waandishi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu na kupata jezi mpya leo MOI.


Kuelekea mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga siku ya Jumapili, Taasisi ya tiba ya Mifupa MOI kwa kushirikiana na mfanya biashara Azim Dewj pamoja wadhamini wa Yanga GSM na wadhamini wa Simba kampuni ya Romario Sports 2010 imezindua kampeni ya kuchangia damu ambapo mchangiaji atapatiwa jezi mpya ya timu anayoishabikia.

Kampeni hiyo inayokwenda kwa jina la ‘changia damu okoa maisha upate jezi’ inalenga kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa damu salama kwa majeruhi wa ajali, Watoto wenye vichwa vikubwa , wagonjwa wasiofahamika na wasio na ndugu pamoja na wagonjwa wengine wenye uhitaji.

Mfanyabiashara Azim Dewj amesema hii ni awamu ya pili ya kampeni hii ya uchangiaji damu ambapo awamu ya kwanza mashabiki wa Yanga na Simba waliochangia damu walipata tiketi za kuingia kwenye mechi ya watani hao wa jadi.

“Nawahamasisha mashabiki wa timu za Simba na Yanga kujitokeza kwa wingi MOI kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wahanga wa ajali na wengine wanaohitaji , safari hii ukichangia damu tunakupa jezi mpya ya timu unayoshabikia” alisema mfanyabiashara Azim Dewj.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa tiba MOI Dkt Samuel Swai amesema mahitaji ya damu MOI ni chupa 30 kwa siku ambapo kumekua na changamoto ya upatikanaji wa damu kutokanana na wachangiaji wa hiari kupungua.

Dkt Swai amesema zoezi la uchangiaji damu litakua siku ya Jumamosi tarehe 11/07/2020 katika eneo la kuegesha magari la kitengo cha dharura cha zamani ambapo zoezi litaanza saa tatu asubuhi mpaka saa kumi jioni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.