Habari za Punde

Balozi Seif akagua ujenzi wa barabara nne za Unguja

Harakati za ujenzi wa Bara bara ya Kilomita Nne kutoka Kinduni hadi Kitope iliyo ndani ya Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa kaskazini Unguja
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Makamanda wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Bara bara Nne zilizomo ndani ya Kisiwa cha Unguja
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd, Shomari akimpatia maelezo Balozi Seif wakati wizara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akielezea kuridhika kwake na jitihada za Wahandisi Wazalendo jinsi wanavyosimamia vyema ujenzi wa Miundombinu ya Bara bara Nchini.
  Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na kumpongeza Mwakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya MECCO Bwana Bujeti kwa Uzalendo wake wa kutekeleza kazi za Ujenzi bila ya kusimamiwa.
 Baadhi ya Wananchi katika maeneo mbali mbali wakifuatilia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa Bara bara Nne za Kisiwa cha Unguja
  Mhandisi wa Bara bara za ndani kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Ali Omar akimthibitishia Balozi Seif  kukamilika kwa wakati Miradi ya Bara bara  iliyo chini ya Tawala za Mikoa.
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wenzake na Wananchi wakiishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa umakini wake wa kuimarisha miradi ya MawasIliano ya Bara bara Nchini.
Picha na – OMPR – ZNZ. 
Na Othman Khamis, OMPR
Wakati Serikali Kuu ikiendeleza dhima ya kuimarisha Miundombinu ya Mawasiliano ya Bara bara Nchini kwa kutumia gharama kubwa Wananchi wana wajibu wa kuzingatia matumizi bora ya Rasilmali hiyo muhimu katika mwenendo wa Uchumi wa Taifa pamoja na Ustawi wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara mahsusi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bara bara Nne zinazojengwa katika kiwango cha Lami chini ya usimamizi wa Mfuko wa Bara bara Zanzibar pamoja na Benki ya Kiarabu inayosimamia Maendeleo ya Kiuchumi Barani Afrika {Badea}.
Bara bara hizo ni pamoja na ile iliyoanzia Kinduni hadi Kitope yenye urefu wa Kilomita Nne, Mwera Mambo sasa hadi Mashine ya Maji Meli Tano ikiwa na urefu wa Kilomita 3.4, Fuoni Polisi hadi Kibonde Mzungu Daraja la Dr. Shein Kilomita 1.2 pamoja na  ile  iliyoanzia Mtaa wa Jumbi hadi Koani Kilomita 6.3.
Balozi Seif  alielezea kuridhika kwake na kazi kubwa inayofanywa na Wahandisi Wazalendo katika kuweka miundombinu safi na imara ya Bara bara jambo ambalo litaleta faraja kubwa kwake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein wakati wa mapumziko yao baada ya Utumishi wa Umma.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashauri Wahandisi hao wakati wanapokabidhiwa jukumu la kuimarisha Miundombinu ya Ujenzi wakazingatia vyema mbinu na mikakati ya kisasa katika ujenzi huo kutokana na uhaba wa Rasilmali ya Mchanga unaovikabili Visiwa vya Zanzibar hivi sasa.
“ Wahandisi na Wananchi lazima waelewe kwamba Zanzibar kwa sasa ina upungufu mkubwa wa Mchanga, hivyo katika miradi wanayoianzisha  ni vyema wakazingatia changamoto hiyo ili wasijekwama katika kazi yao”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Wizara inayosimamia masuala ya Ujenzi pamoja na ile ya Fedha kuhakikisha kwamba suala la malipo linafanyika kabla ya kukabidhiwa Miradi husika kwani haitopendeleza kuona mradi unamalizika na kukabidhiwa ukiwa bado unakabiliwa na deni.
Balozi Seif alitoa onyo kwa  Vijana wanaoendesha vyombo vya Moto kwa mwendo wa kasi kuacha mara moja tabia hiyo mbaya na isiyostahiki kwa Mila na Utamaduni wa asili kwa vile  unagharimu maisha ya Wananchitu kadhaa hususan Wazee na Watoto wasio na hatia yoyote.
Alibainisha kwamba uimarishaji wa Miundombinu unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wahisani, Mataifa Rafiki na hata zile Taasisi za Kimataifa unazingatia Zaidi na kwa kina kuwarahisishia usafiri Wananchi wake katika harakati zao za kujitafutia Riziki.
Wakitoa ufafanuzi wa kazi zinazoendelea za Ujenzi wa Miundombinu hiyo ya Bara bara Wahandisi wasimamizi wa Miradi hiyo walisema yapo matumaini makubwa ya Miradi hiyo ya Bara bara kukamilika katika kipindi kilichowekwa kwa mujibu wa Mitaba yake.
Walisema hatua hiyo imekuja kutokana na Ushirikiano mkubwa wanaoupata wa Wananchi katika sehemu zinazopita Miradi hiyo ya Bara bara sambamba na ujenzi wa haraka wa Madajara kutokana na hali bora ya Hewa iliyopo hivi sasa wakati harakati za ujenzi zikiendelea.
Hata hivyo Wahandisi wasimalizi hao wa Miradi ya Bara bara walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba baadhi ya miradi hiyo ilichelewa kwenda na wakati uliopangwa kutokana na changamoto ya uhaba wa Mchanga pamoja na Maambukizi ya Ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona ambao ulisitisha harakati za usafirishaji wa baadhi za Vifaa na zana za Ujenzi.
Kwa upande wao Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Hassan Khatib Hassan na yule ya Mkoa wa Kusini Unguja Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud kwa niaya ya Wananchi wa Mikoa hiyo wameipongeza na kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa umakini wake wa kupambana na changamoto zinazowakabili Wananchi.
Walisema Ujenzi wa Miundombinu ya Bara bara kwa kiasi kikubwa umesaidia kurahisisha harakati zao za Mawasiliano kwa kusafirisha bidhaa zao, kufuata huduma za Afya hasa kwa Akina mama Wajawazito sambamba na mahitaji yao ya wakati wa burudani.
Wakuu hao wa Mikoa pamoja na mambo mengine kupitia Kamati zao za Ulinzi na Usalama katika hatua za awali wameshaweka Mikakati ya kulitafutia ufumbuzi tatizo la mwendo kasi katika bara  bara tofauti ambapo Askari wa usalama Bara barani watawekwa kuratibu mwenendo wa matumizi wa Bara bara hizo.
Nao Wananchi wa maeneo yaliyobahatika kupitishwa bara barahizo wameelezea kufarajika kwao na hatua ya Serikali kuona umuhimu mkubwa wa kuwapatia huduma hiyo ya mawasiliano ya Bara bara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.