RAIYE MKUBWA - WVUSM – PEMBA.
Kama inavyoeleweka kwamba kila ifikapo tarehe 12/08 ya
kila mwaka ni siku ya kimataifa ya Vijana, siku ambayo mataifa mbali mbali
ulimwenguni huadhimisha kwa lengo la kutambua na kutathmini juhudi na michango
inayotolewa na vijana katika maendeleo ya jamii, taifa na Dunia kwa ujumla.
Umoja wa Vijana wa CCM wakishirikiana na vijana wa baraza la vijana
wilaya ya chake chake wameadhimisha siku ya wiki ya vijana duniani kwa
kujitolea kufanya usafi katika hospitali ya Rufaa ya Changuo iliyopo Vitongoji
wilaya ya Chake chake Mkoa wa kusini Pemba.
Akizungumza na vijana hao Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo Ndg.
Kassim Ali Omar amewataka Vijana kuitumia fursa ya wiki ya vijana kwa kuitilia
maanani kaulimbiu ambayo inalenga kudumisha amani na utulivu hususan katika
kipindi hiki cha matayarisho ya uchaguzi mkuu wa taifa.
Afisa kassim, ametoa wito kwa vijana kuwa na moyo wa kujiendeleza
kielimu na kushiriki kikamilifu katika kutafuta mafunzo ya vitu mbali mbali ili
kufanya mambo kwa uweledi wa hali ya juu.
Aidha, amewataka Vijana kusoma elimu ya nadharia na vitendo ili kufanya ujasiriamali hivyo kuweza kujiajiri wenyewe kutokana na ujuzi
wataoupata kwalengo la kukuza mfuko wa
mapato yao pamoja na maendeleo ya taifa
kwa ujumla.
‘’Jambo la msingi tukitia maanani siku hii tujitahidi kujiendeleza
kielimu kusoma elimu ya nadharia na
vitendo ambayo ndani yake inaingiza masuala ya ujasiriamali na kuwapelekea
vijana kujiajiri wenyewe’’. Alisema
Pia amewapongeza sana vijana kwa kujielewa na kujitokeza kwa wingi
katika utiaji nia na uchukuaji fomu za kugombania uongozi wa nafasi mbali mbali
kwani kumeonesha muamko mkubwa uliopatikana kwa Vijana ukilinganisha na miaka
mengine ya uchaguzi na kuwaomba vijana baada ya uchaguzi wayapokee matokeo kwa
njia ya amani
Afisa huyo, amewataka vijana waitumie nafasi hii kuwashawishi vijana
wengine waweze kufanya matendo mazuri ili kuepukana na vishawishi kama utumiaji
wa madawa ya kulevywa na kuvuta bangi waepukane nayo kwani yanavunja heshma
katika jamii
‘’Vijana tuna nafasi kubwa katika jamii katika suala la kushawishi na
kuhamasisha wengine waweze kufuata matendo mema, kwani kuna mambo mengi ya
madawa tusaidie wenzetu waepukanenayo kwani hayo’yanavunja heshma na hadhi ya
jamii’ alisema
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Chakechake ndg. Ashloo Masoud Khamis amempongeza
Mhe. Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti Wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed
Sheni Pamoja na Dkt John Magufuli kwa Kuwathamini vijana na kuwapa nafasi
katika uongozi na kuwashirikisha katika mambo mbali mbali ndani ya serikali.
Vile vile, Ashloo amewaasa vijana
kufanya mambo mazuri katika siku yao kwa kufanya kazi nzuri hata baada ya
maadhimisho haya ili kuionesha jamii inayoiangalia ni kitu gani wanafanya.
‘’Nianze kuwaasa vijana mufanye kazi nzuri kwa hili tulilolikusudia
kwani jamii inatuangalia na tunajuilikana nini tunafanya lakini pia tuwahongere
Raisi wa Serikali zote mbili kwa kwa kuwapenda Vijana na kuwapa kipaombele’’
alieleza
Aidha, katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM wilaya ya Chake Chake Ndg Thamra
Bakari Yusuf, amewaomba Vijana kuwa mstari wa mbele katika kupambana na mambo
maovu yanayofanywa na vijana wengine ili kuikomboa jamii na mambo machafu, na
kuwaelimisha kwamba Zanzibar yetu ni Moja na inahitaji amani na utulivu na sio
machafuko.
Akitoa neno la shukrani Daktari dhamana wa Hospitali ya Changuo, Dkt. Sharifu
Khatibu amewapongez Vijana waliotumia Muda wao wa siku ya Vijana kwa kuichagua
Hospitali ya Changuo kuifanyia Usafi ingawa kuna shughuli nyingi za kufanya
katika jamii lakini wakaamua kuwagusa wagonjwa katika Hospitali hii.
‘………….. niwashukuru sana kwa kutumia muda wenu kuja kufanya usafi katika
hospitali hii na kuacha maeneo mengine kama mashuleni na kuona umuhimu wa
kuwagusa wagojwa….’’ Alieleza
Afisa Vijana wilaya ya Chake chake Bi Stara Khamis Salim amewaomba
Vijana kujua kwamba hii ni siku yao adhimu hivyo kuitumia kwa kuwa pamoja na
kudumisha amani na utulivu kama walivyoamua kuungana kwa pamoja vijana wote ndani
ya wilaya yao kufanya kitu ambacho ni cha kuonekana wameitumikia vipi siku ya
vijana duniani.
Kwa upande wao Vijana wameipokea vizuri siku ya vijana na kutoa wito kwa
vijana wengine kwamba wawe na moyo wa kujitolea ili kuleta maendeleo katika
jamii yao.
Matron wa Vijana wilaya ya Chake chake Ndg. Zuhura Salim Mahmoud
ameeleza kuwa vijana wamehamasika na siku hii kwani wamepata kujitoa kwa wingi
na kutimiza hamu yao waliokuwa wakiitamani kwa muda mrefu hivyo wameweza
kutekeleza moja kati ya malengo yao.
Pia amewaomba vijana wengine waweze kujiunga kwenye vikundi vyao vya
michezo na sanaa ili waweze kuhamasika na kujichangamsha pia kusogeza mbele
maendeleo ya chama kwani wanapojitolea kinachoonekana ni Vijana na Chama cha
Mapinduzi.
‘Vijana wanaweza kuhamasika kupitia makundi yetu ya sanaa na ya
kimaendeleo kama haya ya kujitolea ndio nafasi yetu ya kuonekana vijana….’’
Hata hivyo, Hamadi Khamis Ali Katibu wa Vijana tawi la vitongoji Ametoa
wito kwa Vijana wengine ambao hawakushiriki katika zoezi hili kuwa na moyo wa
kujitolea na kushiriki katika matukio ya kijamii kwani vijana ndio nguvu ya
taifa, na kuwaomba vijana wenzake wadumishe amani na utulivu.
Juma Jongo Juma ambaye Ni mjumbe wa baraza la vijana tawi la vitongoji amewataka
vijana wengine kujiunga na Umoja huo kwani watapata faida tofautitofauti katika
zoezi hilo, kama vile kujichangamsha mwili hivo kuboresha afya zao, kuboresha
usafi mazingira ya Hospital na pia
wameweza kujitangaza ndani na nje ya nchi kwani hii ni siku ya kimataifa.
‘……wenyewe tumepata kujichangamsha kiafya, kuboresha usafi kwenye hospitali
zetu pia kutambulikana vijana kuwepo ndani ya nchi…….’’
Kwa mwaka huu wa 2020 kauli mbiu ya siku ya kimataifa ya vijana ni
‘youth engagement for global action’ ujumbe ambao unalengo la kuimarisha na
ushirikishwaji wa vijana wenye tija katika ngazi ya kijamii, kitaifa na
kimataifa.
Kwa upande wa Zanzibar maadhimisho haya yanafanyika wakati taifa likiwa
katika kipindi cha matayarisho ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, ambapo vijana ni
sehemu kubwa ya wananchi wanaotarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo.
Hivyo, kutokana na kauli mbiu ya 2020 na hali ya Taifa kukabiliwa na
kipindi muhimu cha uchaguzi Mkuu, Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Vijana
kwa Zanzibar yamebeba kauli mbiu isemayo ‘ KIJANA! SHIRIKI UCHAGUZI, DUMISHA
AMANI’’ kwa ajili ya kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika hatua zote
za uchaguzi kwa njia ya amani.
No comments:
Post a Comment