Habari za Punde

Wadau wa Elimu Hadeni Waweka Mkakati Kuboresha Elimu.

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.
Wadau wa elimu wa Wilaya ya Handeni wameweka mkakati utakaohakikisha kero sugu zinazozorotesha maendeleo ya elimu kwa wanafunzi ikiwamo miundombinu duni  na raslimali fedha vinaboreshwa

Mkakati huo waliuweka jana wakati asasi isiyo ya kiserikali ya Tree of Hope ilipokuwa ikitambulisha mradi unaofadhiliwa na shirika la Foundation For Civil Society (FCS) wa ufuatiliaji wa uwajibikaji kwa jamii "SAM"sekta ya elimu utakaotekelezwa kwa miezi sita katika vijiji nane vilivyopo Wilayani hapa.

Wakizungumza katika mkutano uliofunguliwa na Afisa Tarafa ya Mzundu, Elizabeth Mponda kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni Toba Nguvila, wadau hao wakiwamo wajumbe wa SAM wa vijiji hivyo walisema katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo watahakikisha kero sugu katika elimu zinapatiwa ufumbuzi.

Afisa Mtendaji wa kata ya Kitumbi Hamis Kipanga alisema wajumbe wa kamati ya ufuatiliaji uwajibikaji kwa umma katika elimu, walimu, watendaji Serikalini na wazazi wanapaswa kuungana kuyatafutia ufumbuzi mambo yanayorejesha nyuma maendeleo ya elimu.

" Katika kipindi hiki cha miezi sita ya utekelezaji wa mradi huu, ni lazima tutafute ufumbuzi wa mimba kwa wanafunzi wasichana, utoro shuleni na kisha tuamshe ari ya kusoma ili idadi kubwa ya wanafunzi wa Wilaya ya Handeni wafikie kiwango cha elimu ya juu"alisema Kipanga.

Mratibu wa mradi huo kutoka asasi ya Tree of Hope, Goodluck Malilo alitaja mambo yatakayofanyika wakati wa utekelezaji wake ikiwamo mafunzo kwa wadau, ufuatiliaji uwajibikaji katika vijiji nane na kutathmini.

"Lengo la mradi ni kuhakikisha elimu katika Wilaya ya Handeni inatolewa kwa ubora unaohitajika,ufaulu unaongezeka na kila mmoja anatekeleza wajibu wake" alisema Malilo.

Afisa Tarafa ya Mzundu, Elizabeth alieleza kuridhishwa kwake na mkakati uliowekwa katika mkutano huo ikiwamo kuhakikisha wazazi wanachangia chakula mashuleni na kusisitiza kuwa Serikali itatoa msaada wa hali na mali ili utekelezaji huo usikwamishwe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.