Habari za Punde

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Wachangia Milioni 30 Ujenzi wa Msikiti Chamwino


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo akimkabidhi Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali  Charles Mbuge mchango wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma unaojengwa na SUMA  JKT ambaye ni mkandarasi wa mradi huo.


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo akisisitiza jambo wakati wa hafla ya kukabidhi mchango wa shilingi milioni 30 zilizotolewa na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na usalama kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma  
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali  Charles Mbuge akizungumza wakati wa hafla ya kupokea mchango wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama waliochangia milioni 30 na Wakuu wa Mikoa ambao wamechangia shilingi Milioni 26 katika ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma leo Agosti 27, 2020.Mkandarasi wa mradi huo ni SUMA  JKT.


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evaristi Ndikilo akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wakati wa hafla ya kuchangia ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma halfa hiyo imefanyika katika eneo la Chamwino utakapojengwa msikiti huo.


Sheikh wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Suleiman Matitu akitoa neno  la shukrani kwa Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Mikoa waliochangia katika ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino
Sehemu ya Wakuu wa Mikoa walishiriki katika hafla hiyo wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo kabla hajakabidhi mchango wa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwezesha ujenzi wa Msikiti wa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Sehemu ya malighafi za ujenzi wa msikiti wa Chamwino zikiwa tayari katika eneo la ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma kama zinavyoonekana pichani.


(Pichazotena MAELEZO)




Na Mwandishi Wetu- Dodoma                                                                                                                 
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamekabidhi Shilingi milioni 30  ujenzi wa msikiti wa kisasa wa  Wilaya ya Chamwino Mkoani  Dodoma.

Akikabidhi mchango huo leo Agosti 27, 2020 kwa niaba ya wakuu wengine wa vyombo hivyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa wameguswa na azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwawezesha wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo ya imani .

“Naamini kuwa michango zaidi itaendelea kutolewa ili azma ya kujenga msikiti huu ikamilike kwa wakati”, Alisisitiza Jenerali Mabeyo

Hafla ya Kukabidhi fedha hizo imefanyika pembezoni mwa msikiti wa zamani unapojengwa msikiti huo mpya ambapo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Venance Mabeyo amekabidhi fedha hizo kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali, Charles Mbuge, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Suma JKT, inayotekeleza mradi huo.

Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa  kiasi cha Shilingi milioni 142 zimeshachangwa na wadau mbalimbali ili kuwezesha ujenzi wa msikiti huo.

Alipongeza jitihada za kuwafanya watanzania kushikamana bila kujali imani zao kutokana na ushirikiano ulioneshwa na wadau mbalimbali katika kuchangia ujenzi wa msikiti huo.

Kwa upande  wa Wakuu wa Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara,nao pia wamekabidhi shilingi milioni 26 kwaajili ya Ujenzi huo.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Mikoa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evaristi Ndikilo amesema kuwa wanaunga mkono juhudi za ujenzi wa msikiti huo zilizoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

Aidha, Pamoja na Fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka,amekabidhi shilingi milioni mbili zilizochangwa na kanisa la AICC la mkoani humo.

Kwa upande wake, Sheikh mkuu wa Wilaya ya Chamwino Suleiman Matitu  amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuchangia ujenzi wa msikiti huo na kuhamasisha wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia.

Aidha, Shehe Matitu aliwashukuru Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na  Wakuu wa mikoa  kwa kuchangia ujenzi wa msikiti huo.

Azma ya kujenga msikiti mpya wa Wilaya ya Chamwino ilianzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni wakati wa ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Katoliki  la Mt. Immaculata Chamwino ambapo alizindua kanisa hilo  baada ya kuchangia ujenzi wake na ukarabati.

Katika kuendeleza azma hiyo alianzisha  harambee ya ujenzi wa msikiti huo ambapo hadi sasa kiasi cha Shilingi Milioni 142 zimeshapatikana.

Ujenzi wa Msikiti huo unatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni SUMA JKT na tayari vifaa na malighafi mbambali zimeanza kufikishwa  katika eneo la ujenzi ili kazi ya ujenzi iweze kuanza mara moja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.