Habari za Punde

Wananchi Wanaoishi Pembezoni Mwa Reli Kupewa Elimu ya Usalama wa Reli

Afisa usafirishaji wa kanda ya Tanga Rashid Juma akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana katika ofisi za reli jijini Tanga. 
Picha na Hamida Kamchalla -Tanga.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
TIMU ya wakurugenzi katika Shirika la Reli kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wameanza kazi ya uhamasishaji na utoaji wa elimu ya usalama wa reli kwa wananchi wanaoishi maeneo yaliyopo pembeni mwa reli ambayo imeanza kufanyiwa ukarabati kwa mikoa hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Afisa usafirishaji wa kanda ya Tanga Rashid Juma wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake katika jengo la reli jijini.

Alisema kuwa Shirika limefanya ukarabati wa reli kipande cha kutokea Moshi hadi Arusha kwa kuondoa miundombinu ya zamani na kuweka mipya zoezi ambalo litaendelea kwa kukarabati kipande kingine kutokea Tanga mjini hadi wilayani Korogwe.

"Tayari kuna timu yetu kutokea Kilimanjaro na Arusha wameshaanza kazi ya kuwapa elimu ya usalama wa reli wananchi wanaoishi au kufanya shuhuli zao za kibinadamu pembezoni mwa reli, hii ni kutokana na baadhi ya watu kulima na kufanya biashara pembezoni mwa reli" alisema.

"Bado tuna changamoto, hasa kwenye vivuko kwani sio vivuko vyote tumeweka alama (bendera) hivyo kusababisha hali hatarishi hasa kwa vyombo vingine vya usafiri, na nyinyi waandishi wa habari mtusaidie kuwajulisha watu juu ya suala hili" aliongeza.

Hata hivyo aliwaasa wananchi waliojenga makazi yao pembeni mwa reli kufanya usahihi wa kuondoa makazi hayo ambapo aliwataka kujiondoa kabla ya hatua za kisheria kufuatwa dhidi yao na kuongeza kuwa wakati huu wakijiandaa na ufufuaji wa reli kutoka Tanga kuelekea wilayani Korogwe tayari wakurugenzi wanaotoa elimu hiyo tayari wameshafika wilayani humo.

"Kuna baadhi ya wananchi ambao wamevamia na kujenga makazi yao pembezoni mwa reli, niwaase tu kwamba waanze kujiondoa wenyewe kabla hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao" alibainisha.

Aidha Juma alielezea ufufuliwaji wa mabehewa ya kubebea mizigo ambapo alisema kuwa wanayo kazi ya ziada kuanza upya kuwashawishi abiria ambao walikuwa wakitumia reli hiyo kabla haijafungwa mwaka juzi pamoja na wapya wajitokeze kusafirisha mizigo yao.

Alifafanua kwamba ana imani endapo reli hiyo itafunguliwa na kuanza kazi rasmi watahakikisha wateja wao wanapata hufuma sahihi na bora ili kuingia kwenye soko la ushindani na vyombo vingine vya usafiri ambavyo vinafanya biashara hiyo kwasasa.

"Kuingia kwenye hili soko kwa sasa tunajipanga kuwashawishi wateja wetu kurudi tena baada ya sisi kufungiwa njia na nina imani tutawahamasisha na watatuelewa, tunawaomba wateja wetu warudi tumesharudisha behewa zetu na hata bei zetu katika usafirishaji no nafuu zaidi" alisema Juma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.