MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye
pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaletea kiongozi mchapakazi na mwenye uwezo kuwa kuwa Rais wa Zanzibar ambaye ni Dk
Hussein Ali Hassan Mwinyi.
Dk.
Shein aliyasema hayo leo katika mkutano wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM)
huko Gando, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambao ulihudhuriwa na maelfu
ya wanaCCM.
Alisema sifa za Dk. Mwinyi za nidhamu, uhodari wa kazi, kuwajali watu wote na ubobevu wa uongozi sifa hizo hanazo mgombea mwengine yeyote kwa nafasi yoyote kutoka vyama upinzani.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa, Dk. Mwinyi ni kiongozi
anaejali shida za watu na ambaye ameweza kushika nafasi mbali mbali katika Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
‘’Kazi iliyofanywa na mikutano yote ya CCM na kisha
kupatikana kwa mgombea huyo Dk. Hussien Mwinyi haikukosea, maana uchapakazi
wake unaonekana kila pale anapokabidhiwa
madaraka,’’alieleza.
Hata hivyo, Rais Dk. Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti
wa CCM Zanzibar alisema kuwa yeye anayajua vyema majukumu ya urais kutokana na
ugumu wake, na jinsi anavyomfahamu Dk. Mwinyi, basi anauweza kuifanya kazi hiyo
bila ya wasi wasi.
“Urais sio asali kama kila mtu airambe, Urais ni kazi na
Dk. Mwinyi kazi hiyo anaiweza”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, alieleza kuwa, Dk. Mwinyi ndio mgombea pekee ambae
anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais wa Zanzibar, hasa kwa busara zake na utii wa
kazi.
‘’Dk. Mwinyi anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais, maana mimi
nauwelewa sana na sijaona kiongozi mwengine anaeuweza baada ya mgombea
aliyetuliwa na CCM,’’alifafanua.
Hivyo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi na WanaCCM
kumpigia kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mgombea wake
Mwenza, Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Wabunge, Wawakilishi na
Madiwani wote wa CCM.
Alifahamisha kuwa, dhamira ya CCM kila siku ni kuona
wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, hivyo ili hilo litekelezeke ni
kuwapigia kura wagombea wa chama hicho cha CCM.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Dk. Hussein
Mwinyi ndie kiongozio pekee anayegombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kuwa Rais wa
Zanzibar anaeweza kuyalinda, kuyatetea na kuyadumisha Mapinduzi ya Januari 12,
1964 pamoja na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Siku ya tarehe 28, Oktoba mwaka huu, siku hiyo ya kupiga
kura ikifika, muhakikishe hamfanyi makosa, na muwapigie kura rais John Pombe
Magufuli, Dk. Hussein Mwinyi, wabunge, wawakilishi na madiwani wetu wote,’’alisisitiza.
Nae Mgombea Urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema iwapo
wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kushika nafasi hiyo, atahakikisha,
anasimamia uwajibikaji na watakoshindwa atawawajibisha, ili mafanikio ya kweli
yapatikane.
Dk. Mwinyi alisema, hayo ndio kipaumbele chake cha kwanza
mara atapomaliza kuapishwa, kwani mambo hayo ni miongoni mwa yanadhoofisha kwa
kiasi kikubwa maendeleo ya jamii.
Mgombea huyo wa urais, aliyasema hayo Jimbo la Gando
wilaya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, alipokuwa akizugumza na mamia ya wanaccm
na wananchi wengine, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni wa chama hicho.
Aliongeza kuwa, serikali atakayoiongoza hatopenda hata
kidogo kuona ndani yake, mna watendaji wasiopenda kuwajibika, kwani wanakuwa
kikwazo kufikia maendeleo yaliokusudiwa.
Alisema kuwa jambo hilo ni adui mkubwa wakufikia maendeleo
ya Zanzibar, na kuendelea kudumaa kwa baadhi ya sekta, jambo ambalo
halikubaliki na atalisimamia kwa dhati.
“Mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, pamoja na mambo kadhaa
ambayo ntawafanyia, lakini suala la uwajibikaji ndio kipaumbele cha kwanza, na
akitokezea mtendaji kushindwa kuwajibika, ntamuwajibisha,’’alisisitiza.
Aidha, Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM
Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaahidi wananchi wa Zanzibar kama akipata ridhaa,
atahakikisha anaimarisha miundombinu ya barabara, ili iwe ya kisasa zaidi.
Alisema, bara bara ambazo ataanza nazo kwa kisiwani Pemba,
ni ile ya Chake Chake - Wete yenye urefu wa kilomita 21, Finya- Kicha yenye
urefu wa kilomita 8.8 na zile ndani ya mji wa Wete zenye urefu wa kilomita 9.
Alisema kuwa, ili Zanzibar ipige hatua kubwa kwenye
maendeleo ya sekta ya utalii, viwanda, uvuvi inategemea sana uwepo wa barabara
za kisasa, katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.
Alisema, ingawa tayari Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed
Shein anaemaliza muda wake, ameitekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015/2020 ambapo nay eye ameahidi kuitekeleza vyema ile ya
2020-2025.
“Kila mmoja ni shahidi kuwa, Inali ya CCM ya mwaka
2015/2020 Dk. Shein, ameitekeleza kwa asilimia 100, karibu kila sekta na mimi
mkinichagua, nitazidi kuziimarisha na kuendeleza,’’alifafanua.
Pia, Mgombea huyo aliwaahidi wananchi kuwa atawafanyia, ni
kupiga vita suala la udhalilishaji pamoja na dawa za kulevya, ambapo alisema matatizo
hayo amekuwa akilielezwa kila anapopita katika kapeni zake za urais nazozifanya
wakati akiwatembelea wananchi mbali mbali Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa, tatizo hilo linamnyima usingizi na ndio
maana mara akichaguliwa. atahakikisha anafanya kila mbinu kuona udhalilishaji
na dawa za kulevya, zinakuwa historia Zanzibar.
Aidha, mgombea huyo wa urais alisema, kutokana na mengi
ambayo aliyafanya rais anayemaliza muda wake, kazi yake itakuwa ndogo mara
akiingia madarakani ambapo alieleza kuwa tayari Dk. Shein ameliimarisha zao la
karafuu na kusababisha kuvunwa kwa tani 3,321 mwaka 2015 na kufikia tani 8,277
ambazo ni nyingi mno.
Aidha, alisema, eneo jengine ambalo limefanikiwa kwa kiasi
kikubwa ni sekta ya elimu , kwa kujengwa skuli za ghorofa za Kizimbani, Limbani
na ile Chasasa pamoja na chuo cha amali kilichopo Daya wilaya ya Wete.
Kuhusu kuliimarisha zao la mwani, Dk. Mwinyi alisema,
tayari Serikali ya Awamu ya Saba, imeshaanza ujenzi wa kiwanda ya kusarifia
mwani, eneo la Chamanangwe sambamba na kuwakabidhi vihori 80 wakulima wa
mwani wa Wilaya ya Wete.
‘’Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, lazima nikiri kuwa
ilipata msimamizi Dk. Shein, maana hata sekta ya utalii imeimarika kwa kuongeza
watalii kufikia laki tano kutoka watalii
37,900 mwaka 2015,’’alisisitiza.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya CCM, amewataka wananchi wa Zanzibar kuhakikisha kura zao
hawazipotezi, kwa kuvipa vyama ambayo havina muelekeo.
Alisema CCM ndio chama kinachojali maisha ya watu wote
wakiwemo wanyonge, wakulima na wakwezi hivyo, dhamira hiyo haiwezi kuendelezwa
na kiongozi yeyote, isipokuwa anaetoka CCM.
‘’Tupeni ridhaa sisi wagombea wote wa CCM, ili tuendelee
dhamira na ari ya kweli ya kuwatumikia, pasi na kujali maeneo mnayotoka wala
rangi, na hii ndio shabaha ya waasisi wa taifa hili,’’alieleza Dk. Mwinyi.
Mapema Naibu Katibu mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma
Mabodi, alisema, ushindi wa CCM hauna shaka, kutokana na kuitekeleza vyema
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2015/2020.
‘’Leo kutoka mjini Wete hadi kijiji cha Gando, unatumia
dakika zisizozidi 20, maana barabara imejengwa tena kwa kiwango cha lami, hayo
ndio mambo ya CCM,’’alisema Dk. Mabodi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad
Mberwa alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa maendelea makubwa yaliyopelekwa na
katika Mkoa huo na Serikali anayoiongoza Dk. Shein.
Nao wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Wilaya ya
Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba walitambulishwa na Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM
Zanzibar ambapo walitumia fursa ahiyo kuomba kura na kuwataka wananchi na
wanaCCM wote kuwachagua ili wazidi kupeleka maendeleo katika maeneo yao.
Viongozi
mbali mbali wa CCM walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha pamoja na
viongozi wengine wa CCM.
Mkutano huo wa Kampeni ulikwenda sambamba na burudani kadhaa zilizotolewa na wasanii mbali mbali wakiwemo wale wa kizazi kipya pamoja na wagongwe kama vile Bi Fatma Issa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment