Habari za Punde

Mwanamke hajazuiwa kuwa kiongozi kwa misingi ya dini



Prf,Issa Haji Ziddy  wakati alipokua akaizungumza na viongozi wa dini mbali mbali na baadhi ya wawakilishi kutoka asasi za kiraia huko katika ukumbi wa Tamwa uliopo Tunguu Wilaya ya kati Unguja

Na Mwandishi wetu


Wakati Tanzania ikielekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu Jamii ya Wazanzibar imetakiwa kufahamu kuwa hakuna sehemu yoyote inayomkataza au kumzuia mwanamke kutokua kiongozi kwa misingi ya dini.

 

Kauli hio imetolewa na Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Prf,Issa Haji Ziddy  wakati alipokua akaizungumza na viongozi wa dini mbali mbali na baadhi ya wawakilishi kutoka asasi za kiraia huko katika ukumbi wa Tamwa uliopo Tunguu Wilaya ya kati Unguja kufuatia uwasilishwaji wa muongozo wa utowaji wa elimu dhidi ya nafasi ya mwanamke na uongozi katika Uislamu.

 

Alisema kwa miaka mingi wanawake  visiwani Zanzibar wamekua wakipoteza fursa za uongozi kutokana na baadhi ya watu kwenye jamii kuwa na dhana potofu ikiwemo kuamini kuwa mwanamke hapaswi kuwa kiongozi jambo ambalo halina mashiko.

 

Alisema  wapo baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao wanatumia baadhi ya aya za Quraan kuwakandamiza wanawake na kupelekea wanawake hao kupoteza fursa ambazo anaamini zingeweza kuwakomboa wao na familia zao.

 

‘’Hata mkataba wa hudaibiya ushauri wa makubaliano yale kwa mara ya kwanza ulitoka kwa mwanamke kwenda kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na wengi wa wanaume wakiwemo maswahaba walidhani wanakandamizwa lakini ulikua mwanzo wa kheri kwa  dini ya kiislamu.’’aliongezea.

 

Prf,Ziddy aliongezea kwa kusema kuwa hadi leo hii kuna kundi kubwa la wanajamii wanaendelea kuamini kuwa kazi za mwanamke na kutunza familia na wengine hawaruhusiwi hata kuwa viongozi kwenye mikutano ya familia zao.

 

Nae Mjumbe wa kamati ya Amani Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga alisema si sahihi wanawake kunyimwa fursa hizo na kuwa wanaofanya hivyo wanapaswa kutambua kuwa wanabeba dhima na wanapaswa kuacha mara moja.

 

Katika hatua nyengine  aliwataka wanawake visiwani hapa kubadilika na kukataa kabisa kujidhalilisha wenyewe na kusema kuwa ni chanzo kikubwa ambacho wanaume hukitumia kama fursa kuwakandamiza.

 

‘’Leo hii imekua kawaida kuona wanawake kwenye nyimbo wanacheza wakiwa na nguo za uchi kabisa na kuonekana kuwa suala la kawaida wakati wanaume wamevaa nguo nzuri zenye kuwasitiri jambo ambalo ni kujidhalilisha wenyewe’’aliongezea.

Kwa upande wake Father Stanley Nicholas kutoka kanisa la Angilaka Mkunazini mjini Unguja alisema yanayoendelea kutokea yote ni kwa sababu ya watu kutokua na elimu na kukosa utayari wa kujifunza.

 

Alisema watu wengi katika jamii wanaamini elimu ya dini ni hile walioikuta lakini wanashindwa kujiongeza kusoma zaidi ambapo anaamini wangeweza kupata mwanga na kuonga uhalisia ulivyo.

 

Nae Amina Salum Khalfan alisema inasikitisha sana kuona hata Baraza la Maulamaa kisiwani hapa kukosa ushiriki wa wanawake jambo ambalo anaamini ni kuendeleza mfumo dume na kwa kuwa Baraza hilo halifanyi kazi kuwahudumia wanaume pekee hivyo kuna kila sababu ya ushiriki wa wanawake ndani yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.