Habari za Punde

WANARUANGWA TUMCHAGUE MAGUFULI-MAJALIWA



MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi  (CCM ) Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  amewasihi wananchi wa Jimbo la Ruangwa kumpigia kura Rais Dkt. John Pombe Magulfuli ili aendelee kujenga na kuimarisha huduma mbalimbali za jamii nchini. 

Akizungumza wakati alipozindua kampeni za CCM katika jimbo la Ruangwa kwenye kijiji cha Chinongwe leo Septemba 11, 2020, Mheshimiwa Majaliwa  amesema maendeleo makubwa yaliyofanyika nchini katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Dtk. Magufuli kwa kiwango kikubwa yamebuniwa na kusimmiwa kwa karibu na Rais mwenyewe.

Amesema kwa kuwa bado ipo  miradi mingi mikubwa iliyoanzishwa na Rais Dkt. Magufuli  inayohitaji kukamilishwa ni   vyema Watanzania wakampigia kura za kishindo zitakazompa nafasi ya kuliongoza Taifa kwa kipindi cha pili ili aweze kumalizia miradi hiyo na kuanzisha mingine mingi kama ilivyoonyeshwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.

Aliitaja miradi inayotekelezwa ni ya ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme wa maji la Nyerere,  Reli ya Kiwango vya Kimataifa ya SGR, ujenzi na uboreshaji wa huduma za afya kama vile ujenzi wa Vituo vya afya, Hospitali za wilaya, Mikoa na Rufaa pamoja na ujenzi wa miradi ya maji kuwa ni baadhi ya miradi ambayo  inamfanya Rais Magufuli astahili kupewa kipindi kingine cha kuiongoza nchi.

Akizungumzia mipango ya serikali ya kuongeza ajira kwa Watanzania, Mheshimiwa Majaliwa amesema  msukumo mkubwa uliofanywa na serikali ya Awamu ya Tano katika kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi  kujenga viwanda vidodo, vya kati na vikubwa ni moja ya mikakati ya makusudi ya kuongeza ajira kwa Watanzania. 

“Kiwanda cha samani na kiwanda cha kubangua korosho vinavyojengwa katika kijiji cha Namkonjera  wilayani Ruangwa ni moja ya juhudi  zinazolenga kuwapatia ajira wananchi wa  wilaya hii na Watanzania kwa ujumla”

Kuhusu Vitambulisho vya Wajasiriamali   nchini, Mheshimiwa Majaliwa amevitaja kuwa chanzo kingine cha ajira hasa kwa vijana ambao hapo awali  walibugudhiwa kwa kuonekana kuwa hawana uhalali wa kufanya biashara katika baadhi ya maeneo hasa ya katikati ya miji na majiji . 

Mheshimiwa Majaliwa amesema bugudha kwa vijana hao hivi sasa imekwisha na  sasa wanafanya biashara zao  ambazo ni ajira halali inayotambuliwa na Serikali  ambayo inayowapa kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao .

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa aliwashukuru wanaRuangwa wananchama wa vyama vyote vya siasa kwa kumpitisha bila kupingwa katika jimbo hilo.

Naye mgombea ubungea wa Jimbo la Ndanda, Cecil Mwambe alipopewa nafasai ya  kuzungumza amesema  Ilani ya Uchanguzi ya CCM ya 2020-2025 imegusa maisha ya wananchi wa Ruangwa  kwani  imezungumzia maboresho ya zao la korosho  pamoja masoko yake.

Mheshimiwa Mwambe amewaomba wanaRuangwa wamchague Rais Dkt. Magufuli na Madiwani wa CCM  kwani Ilani ya CCM imezingatia maslahi yao hasa kilicho cha mazao ya Biashara na chakula.

Mbuge Mstaafu wa Viti Maalum, Riziki Lulida aliyerejea  CCM akutoka Chama cha CUF aliwaomba wanaRuangwa  kumuunga mkono Rais Dkt. Magufuli  kwa kumpa kura nyingi kwani kawafanyia mengi na makubwa wana Lindi

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 11, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.