Habari za Punde

Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Akizungumza na Wananchi Kuhusu Matokeo ya Utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar.

 

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN KATIKA HAFLA ZA KUZUNGUMZA NA WANANCHI KUHUSU MATOKEO YA UTAFITI WA MAFUTA NA GESI ASILIA,ZANZIBAR

TAREHE: 23 OKTOBA, 2020

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

 Assalam Aleikum

Awali ya yote naanza kuzungumza nanyi kwa kumshukuru Mola wetu Mtukufu, Subhanahu Wataala, Muumba wa Ulimwengu na vyote viliomo, kwa kutujaalia neema ya uhai na uzima wa afya tukaweza kukutana wakati huu kwa madhumuni ya kupeana taarifa kuhusu jambo maalum ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Jambo hilo, ambalo nimekuwa nikiahidi mara kadhaa kulizungumza ni maendeleo na matokeo ya utafiti wa mafuta na gesi asilia ambao ulifanywa kwa vipindi tafauti katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Kabla sijatoa taarifa za matokeo ya utafiti wa shughuli ya utafutaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia Zanzibar, napenda nikushukuruni sana ndugu wananchi kwa ustahamilivu mkubwa mliouonesha na ushirikiano wenu kwa Serikali pamoja na wataalamu wetu ambao walikuwa wakifanya utafiti huo. Nafahamu kuwa kulikuwa na maneno mengi kuhusu utekelezaji wa dhamira hii njema ya Serikali yenu, lakini kamwe hamkubabaika na mliendelea kuiamini Serikali yenu. Nakupongezeni sana.

Mtakumbuka kuwa katika hotuba zangu mbali mbali, nilikua nikikuahidini kwamba muda utakapofika, Serikali yenu itatoa taarifa rasmi zilizo sahihi kuhusu suala hili. Leo ndio siku yenyewe imefika.

Nachukua fursa hii kutoa shukurani kwa uongozi na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati pamoja na wataalamu wetu wote wazalendo kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kulishughulikia suala la utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Nakupeni hongera sana. Kadhalika, natoa shukurani kwa taasisi zote za nje ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo katika shughuli za utafiti na utafutaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia tangu tulipoanza shughuli hizi. Kwa hakika, kila mmoja ametimiza wajibu wake na hatimae tumeweza kufikia hatua nzuri ya matumaini, hata kama bado hatujafika mwisho wa safari yetu.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Mwaka 2011, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ilianza upya harakati za utafiti wa mafuta na gesi asilia kwa kufanya mazungumzo yaliyotokana na  safari yangu ya Ras Al Khaimah kutokana na mualiko wa Mtawala wa Ras Al Khaimah Sheikh Said Bin Saqir Al Qasimi juu ya namna ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakavyoshirikiana na Serikali ya Ras Al Khaimah. Mazungumzo hayo ndiyo hatimae yaliyopelekea kusainiwa kwa Hati ya Mashirikiano (Memorandum of Understanding – MoU), baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Ras Al Khaimah tarehe 12 Novemba 2011. Hati hio ya Makubaliano ilikuwa na mambo tisa. Jambo moja kati ya hayo ni kuanzisha na kuingia makubaliano ya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika eneo la mipaka ya Zanzibar.

Katika utekelezaji wa suala hilo, Serikali zetu mbili ziliunda Kamati maalum ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano yenye kazi ya kusimamia utekelezaji. Katika utekelezaji wa majukumu yao, Kamati hii ilifanya vikao saba (7) baina ya tarehe 31 Januari, 2012 na tarehe 22 Agosti, 2016. Vile vile, katika safari yangu niliyoifanya huko Uholanzi, tarehe 28 Agosti, 2013, nilifanya mazungumzo na Kampuni ya Shell kutokana na mualiko wao na hatimae yalipelekea kutia saini kwa Hati ya Maelewano baina Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar   na kampuni ya Shell. Hati hio ilikuwa na mambo 11. Katika utekelezaji wa makubaliano hayo iliundwa kamati ya pamoja ya kusimamia makubaliano hayo, ilikuwa na jumla ya wajumbe saba (7) wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sita (6) wa Kampuni ya Shell.

Jumla ya vikao vitano (5) vilifanyika baina ya tarehe 19 Januari, 2014 na tarehe 9 Aprili, 2015. Vikao vivyo, vilifanyika Zanzibar na The Hague, Uholanzi.

Hadi tarehe hio 9 Aprili, 2015 vikao hivyo, vilisita kufanyika na Kampuni ya Shell haikuleta taarifa yoyote; ingawa Wizara ya Ardhi, Nyumba maji na Nishati, iliwasiliana na ofisi ya Shell – Dar es Salaam zaidi ya mara 3.

Mwakilishi wa kampuni ya Shell iliopo Dar es Salaam alikuja kuonana nami mwaka 2016 na kunieleza kwamba kwa kipindi hiki hawatashughulikia suala hilo, labda hapo baadae. Kwa hivyo, jitihada zetu tuliziendeleza na Kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah. Tulitegemea Kampuni nyengine za nje zingejitokeza. Hata hivyo, hadi sasa hakuna Kampuni au nchi nyengine zilizojitokeza.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kukubaliana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipeleka muswada wa Sheria katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Sheria ya Mafuta  tarehe 5 Julai, 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kuipitisha Sheria ya Mafuta Namba 21 ya mwaka 2015 ambayo ilitiwa saini na Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 4 Agosti, 2015.  Pamoja na mambo mengine, sheria hio ilibainisha kwamba shughuli zote za mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Bara zitafanywa na Taasisi zilizoanzishwa ndani ya Sheria namba 21 ya mwaka 2015 na shughuli zote za mafuta gesi asilia kwa upande wa Zanzibar zitafanywa na Taasisi zitakazoanzishwa kwa mujibu wa Sehria za Zanzibar.

Kwa mara nyengine natoa shukurani nyingi kwa Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kiwete kwa hatua alizozichukua, ili kuhaikishaa kuwa kabla ya kustaafu kwake suala hili linapatiwa ufumbuzi na kuondoa kero ya muda mrefu. Kwa mujibu wa sheria hio, Zanzibar ilipewa uwezo na Mamlaka ya kuzishughulikia rasilimali za mafuta na gesi asilia wenyewe. Sijui wale wanaosema hatuna Mamlaka hayo, wanatumia sheria ipi. Kufuatia hatua hio, na kwa lengo la kuzidi kupata nguvu za kisheria, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitunga Sera ya Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016 pamoja na Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia Namba 6 ya mwaka 2016, niliyoitia saini hapa Ikulu kwa taadhima zote, tarehe 15 Novemba, 2016. Madhumuni ya Sera na Sheria  yalikuwa ni kwa ajili ya kusimamia shughuli za utafutaji,uchimbaji,uendelezaji na uzalishaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Napenda nirudie tena maneno niliyoyaeleza tarehe kama ya leo mwaka 2018, katika hafla ya Utiaji saini wa Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, hapa hapa Ikulu, kwamba suala la utafutaji wa mafuta na gesi asilia ni jambo linalohusu maendeleo yetu na kamwe halitakiwi lituletee mfarakano katika jamii yetu, badala yake inatakiwa lituunganishe. Tunapaswa tujiepushe na watu wachache ambao wameamua kulitumia jambo hili kuwa ajenda ya kuwagawa watu jambo ambalo ni kinyume na malengo ya Serikali ya kuzishughulikia rasilimali hizi. Malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa faida zitakazopatikana kutokana na rasilimali ya mafuta na gesi asilia zitachangia katika ukuaji wa uchumi wetu na zinawanufaisha wananchi wote bila ya kuwatenga na kuwabaga wengine.

Ni dhahiri kuwa suala la Mafuta na Gesi Asilia, ni sehemu ya Uchumi wa Buluu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, inafuata Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya 2015 -2020. Uchumi wa Buluu ni Ajenda iliyomo vile vile, katika Dira 2050, ambayo nimeizindua juzi tarehe 19 Oktoba, 2020. Viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Viongozi wa CCM wanaielewa vyema Dira 2050 na Ilani yetu ya Uchaguzi Mkuu ya 2020- 2025. Kwa msingi huo, ninaamini kwamba suala hili la utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia utaendelezwa vyema  na Serikali ya Awamu ya Nane na zitakazofuata hapo baadae.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Baada ya hatua hio, tukaanzisha taasisi maalum zitakazoshughulikia sekta hii ya mafuta na gesi asilia. Taasisi hizo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC). Malengo ya kuanzisha taasisi hizi yalikuwa ni kuimarisha usimamizi na udhibiti wa shughuli zote za utafutaji, uchimbaji, uendelezaji na uzalishaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia. Vile vile, hatua hii ina madhumuni ya kuweza kujiendesha kibiashara kupitia kampuni yetu ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia tuliyoianzisha, ambayo imeanza kazi vizuri.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Katika kufanikisha kuwepo kwa Mkataba wa Mgawanyo wa Mapato yanayotokana na Mafuta na Gesi Asilia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliunda Kamati Maalum ya majadiliano iliyoongozwa na Mheshimiwa Said Hassan Said; Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kamati hio ilifanya kazi nzuri ya majadiliano ya muda mrefu yaliyoanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2018 kuhusiana na kitalu cha Pemba – Zanzibar. Hatimae, tulikubaliana na ndipo Serikali ilipoingia Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia na Kampuni ya RAK Gas katika sherehe iliyofanyika hapa Ikulu tarehe 23 Oktoba, mwaka 2018.

Pamoja na makubaliana hayo, napenda mfahamu kwamba kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa kitalu cha Pemba – Zanzibar ilianza mwaka 2017 kabla ya kusainiwa kwa Mkataba wa PSA kwa makubaliano maalum baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya RAK Gas. Shuguhli kadhaa zilifanyika mwanzoni zikiwemo uchukuaji wa taarifa kwa njia ya anga (Full Tensor Gradiometric Survey).

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Tarehe 14 Machi, 2017 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilizindua rasmi shughuli ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya anga. Shughuli hio, ilifanywa na Kampuni ya BELL GEOSPACE ya Scotland katika eneo la Kitalu cha Pemba – Zanzibar lenye ukubwa wa kilomita za mraba 11,068. Kazi iliyokuwa ikifanywa ni kuangalia uwezekano wa kuwepo kwa miamba yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia. Taarifa zilizopatikana, zilitoa matokeo yaliyosababisha kufanywa kwa shughuli ya uchunguzi kwa njia ya mtetemo (2D Seismic Survey).

Shughuli ya uchukuaji wa taarifa kwa njia ya mtetemo ilianza mwezi Oktoba 2017 na kumalizika mwezi Machi, 2020. Shughuli hio, ilifanywa na Kampuni ya BGP ya Jamhuri ya Watu wa China. Shughuli iliyofanywa ilijumuisha uchukuaji wa taarifa kutoka baharini, nchi kavu na katika kina kifupi cha bahari. Kwa upande wa bahari, zoezi lilifanywa kwenye eneo lenye urefu wa kilomita 2,815.6, likijumuisha jumla ya mistari 66. Kwa upande wa nchi kavu, uchukuaji kwa njia ya mtetemo, ulifanywa katika jumla ya mistari 25 yenye urefu wa kilomita 717.1. Kadhalika, katika maeneo ya kina kifupi cha maji, zoezi lilifanywa kwenye mistari 10 yenye urefu wa kilomita 244.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Baada ya kukamilika shughuli hizo za ukusanyaji wa taarifa, hatua iliyofuata lilikuwa ni kwenda kuzifanyia uchambuzi taarifa hizo, kazi ambayo ilikwenda kufanywa na kampuni ya BGP katika kituo hio kilichoko Kuala Lumpa nchini Malaysia. Usafirishaji wa taarifa za baharini umechukua miezi 11 (Januari, 2018 hadi Disemba 2018). Usafirishaji wa taarifa za nchi kavu na kina kifupi cha maji kwa maeneo ya Unguja na Pemba ulichukua muda wa miezi minane (8) kuanzia mwezi Oktoba, 2018 hadi mwezi wa Julai, 2019.

Matokeo ya usafirishaji wa taarifa zilizokusanywa yameonesha kuwepo kwa sura mbili tafauti. Kwa upande wa Unguja, taarifa za mistari zimekua na ubora unaoridhisha na kuonesha maeneo ya miamba yenye maumbile yanayoweza kuhifadhi mafuta na gesi asilia. Kwa upande wa Pemba, imeonesha taarifa zenye kiwango kidogo cha ubora kutokana na maumbile ya kijiografia ya kisiwa hicho (Gegraphical Landscape).

Kutokana na matokeo hayo, Kampuni ya RAK Gas imeonesha nia ya kutaka kuifanyia usafishaji wa mara ya pili, mistari yote yenye kiwango kidogo cha ubora, ili kuongeza ubora wa taarifa hizo. Kufuatia uamuzi huo, Kampuni ya RAK Gas ilichukua hatua ya kuendelea na kazi ya kutafuta taarifa za mitetemo za mafuta na gesi asilia kwa kitalu cha Pemba – Zanzibar, kazi ambayo ilianza mwezi Agosti, 2019 na kukamilika mwezi Machi, 2020. Matokeo ya kazi waliyoifanya, yamepelekea Kampuni ya RAK Gas kuendelea na kazi ya kufanya uchunguzi kwa njia ya mtetemo katika kina kifupi cha maji, eneo ambalo linaonesha kuwa na viashiria vya kuwepo kwa gesi asilia.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Matokeo ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya Anga (Full Tensor Gradiometric Survey) na Mtetemo (2D Seismic Survey) yameonesha uwezekano mkubwa wa kuwepo miamba yenye uwezo wa kuhifadhi Mafuta na Gesi Asilia katika kitalu cha Pemba – Zanzibar. Hii ni kwa sababu, matokeo ya taarifa zote yameonesha kuwepo kwa viashiria vyote vya mfumo wa uhifadhi wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia (Petroleum System Elements (PSE). Kwa hakika hio ni taarifa njema na tumshukuru Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wa utafutaji kwa njia ya anga, imeonekana kuwepo kwa maeneo matatu (3) yenye uwezekano wa kuwepo kwa miamba inayoweza kuzihifadhi rasilimali ya mafuta na gesi asilia. Maeneo hayo ni kisiwa cha Makoongwe kilichopo kusini mwa kisiwa cha Pemba, Kisiwa cha Tumbatu kilichopo Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Unguja na katika upande wa bahari ya Mashariki mwa kisiwa cha Unguja.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Kwa upande wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya mitetemo, matokeo yameonesha kwamba yapo maeneo matano (5) yenye uwezekano wa kuwepo na rasilimali ya gesi asilia katika Kitalu cha Pemba – Zanzibar. Sehemu zenyewe ni eneo la bahari liliopo baina ya Kaskazini Mashariki mwa kisiwa cha Unguja na Kusini mwa kisiwa cha Pemba, eneo la Kaskazini, Kusini na Mashariki mwa kisiwa cha Unguja, eneo la bahari ya Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Unguja, eneo la bahari ya Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Pemba na eneo la Kusini mwa Kisiwa cha Pemba.

Kwa jumla, maeneo hayo yameonesha kuwepo kwa maumbile ya miamba (Structures) yenye uwezo wa kuhifadhi rasilimali ya gesi asilia yenye ujazo wa futi trilioni 3.8. Kwa mujibu wa tafsiri hio, uwezekano wa kufanikiwa kuigundua rasilimali ya gesi asilia wakati wa kisima ni asilimia Thalathini (30%) kiwango ambacho ni kikubwa kwa upande wa utafutaji  kwa nia ya mtetemo (2D Seismic). Aidha, kuna uwezekano wa kupanda kutoka asilimia thalathini (30%) hadi asilimia arubaini na tano (45%) baada ya kukamilika utafutaji wa kina kwa njia ya mtetemo kwa kutumia teknolojia ya 3D. 

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Baada ya kupata matokeo hayo ya utafutaji, kwa njia ya anga na mitetemo yenye kutia matumaini, kazi zinazoendelea hivi sasa ni kama zifuatazo:-

 i. kuzifanyia usafirishaji wa mara ya pili taarifa zilizoonekana kutokuwa na ubora wa kuridhisha katika zoezi la mtetemo lililokamilika.

 ii. kuendelea na utafutaji rasilimali hizi katika kina kifupi kwa njia ya mtetemo kwenye maeneo maalum yaliyogundulika kuwa na viashiria vya kuwepo kwa mafuta na gesi asilia.

 iii. kutambua eneo la kuchimba kisima cha utafutaji (Identification of well location)

iv. kuanza kazi ya kuchimba kisima cha kwanza cha utafutaji (Exploration Well Drilling).

Hizo ndizo shughuli kubwa zinazotaka kutekelezwa katika jitihada za Serikali yenu za kushughulikia rasililmali za mafuta na gesi asilia.

Kwa hakika, dhamira njema ya Serikali yenu ya kulishughulikia suala la utafutaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia inazidi kuonekana,  kwani matokeo ya kazi ya utafutaji  na uchambuzi wa taarifa za anga na mtetemo yanazidi kuleta matumaini ya kuwepo kwa uwezekano wa kugundulika kwa rasilimali hizo hapa Zanzibar. Viashiria vilivyobainika katika tafiti zilizokwishafanywa, vimeonesha matumaini ya kuwa na rasilimali hizo. Hata hivyo, katika utafiti uliofanywa, Kampuni ya RAK Gas imevutiwa  kuvutiwa zaidi kuendeleza shughuli zake kwenye rasilimali ya gesi asilia katika maeneo ya baharini. Pamoja na hayo, juhudi kubwa zinazohitajika katika kusimamia, kudhibiti na kuendeleza sekta ya mafuta ya gesi asilia kutokana na kuwa kazi hii huchukua muda usiopungua miaka sita (6) hadi minane tangu pale utafiti ulipoanza kufanywa; kabla ya kunufaika na rasilimali hizo.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Kwa mara nyengine, napenda nikuelezeni kuwa shughuli hii si ya kukamilika na kuanza kunufaika kwa leo na kesho. Shughuli hio, bado itachukua muda usiopungua miaka sita mpaka minane tangu kuanza utafiti, kabla ya kuanza kunufaika na rasilimali hizi. Hata hivyo, hatupaswi kuvunjika moyo. Kwa hivyo, tuendelee kuwa na subira kwani wazee walisema, “Subira huvuta kheri.” Nina mategemeo makubwa kwamba huko mbele tutaweza kufaidika na rasilimali hizi kwa vile, tumefikia hatua nzuri  ambapo tayari tumeandaa sera, Sheria na tumeanzisha taasisi za kushughulikia rasilimali hizi  kufikia hatua nzuri za utafiti pamoja na kufanya maandalizi ya ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,

Ninapomalizia kipindi changu cha Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, nimeridhika sana na hatua tulizozifikia katika kuishughulikia rasilimali ya mafuta na gesi asilia kama ilivyobainishwa kwenye Ilani ya uchaguzi Mkuuwa CCM ya mwaka 2015 na kwenye Ibara ya 96(b) ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020. Kwa mara nyengine, natoa shukurani zangu kwa Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa namna tulivyoshirikiana na tukahakikisha kuwa suala la Zanzibar kulishughulikia rasilimali ya mafuta na gesi asilia, linapata ufumbuzi  kutokana na hatua tulizozichukua. Kadhalika, natoa shukurani za pekee kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali yake kwa namna tulivyoshirikiana kwamba Zanzibar tunafanikiwa katika malengo yetu ya kulishughulikia rasilimali ya mafuta na gesi asilia.  vile vile shukurani zangu za dhati naendelea kuzitoa kwa Mtawala wa Ras Al Khaimah Sheikh Saud Bin Saqri Al Qasimi, pamoja na  uongozi wa Kampuni ya Rak Gas  kwa hatua kubwa tuliyoifikia kwa kuzingatia MoU ya tarehe 12 Novemba, 2011 na Mkataba wa mgawanyo wa Mafuta na Gesi asilia (PSA) uliotiwa saini tarehe 23 Oktoba, 2018; miaka 2 iliyopita

Namalizia hotuba yangu kwa kukushukuruni tena ndugu wananchi na ndugu waandishi wa habari kwa kuipokea taarifa yangu hii. Namuomba Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na mshikamano.  Atupe uwezo zaidi wa kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi. Mola wetu atuwezeshe kuzitumia vyema rasilimali zetu kwa faida ya watu wote wa Zanzibar.

 Ahsanteni kwa kunisikiliza

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.