Habari za Punde

Jumla ya Ajali 11 Zimeripotia Mwenzi Septemba Mwaka Huu.

Na Mwashungi Tahir     Maelezo      15-10-2020.

JUMLA ya ajali 11 zimeripotiwa mwezi wa Septemba nwaka huu ambapo kulikuwa na waathirika 28 kati ya hao  27 ni wanaume sawa na asilimia 96.4 na 1 ni mwanamke  sawa na asilimia 3.6.

Akizungumza na waandishi wa habari huko katika ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali uliopo Mazizini Mtakwimu kutoka kitengo cha Makosa ya Jinai, Madai na Jinsia Asha Mussa Mahfoudh wakati alipokuwa akiwasilisha takwimu za ajali na makosa ya barabarani.

Amesema Wilaya ya kati na Magharibi ‘A’ zimeripotiwa kuwa na ajali nyingi  ambazo ni tatu (3) kwa kila Wilaya  ikifuatiwa na Wilaya ya Wete kuwa na ajali mbili ambapo Wilaya ya kati imeripotiwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya waliyoathirika ambao ni kumi na mbili  sawa na asilimia 42.9.

Amesema jumla ya waathirika wa ajali za barabarani kwa waliojeruhiwa na waliokufa wapanda baskeli na piki piki 15, abiria 13, waendao kwa miguu na dereva walioathirika hakuna walioripotiwa kwa mwezi huo.

“Jumla ya makosa 1,406 ya barabarani yameripotiwa kwa  mwezi wa Septemba 2020 ambapo makosa yote yamefanywa na wanaume ikiwemo kutofuata muongozo na kanuni za usalama barabarani ambapo ajali nyingi hutokea kunzia saa kumi na mbili jioni hadi saa sita usiku”, alieleza Mtakwimu huyo.

Amesema miongoni mwa makosa hayo ni pamoja kuzidisha abiria na idadi ya mizigo, kushindwa kuvaa sare na beji kwa utingo na dereva kwa gari za abiria na mizigo na kuendesha chombo cha moto bila ya leseni, bima na leseni ya njia.

Amefahamisha kuwa Wilaya ya Mjini ina idadi kubwa ya makosa ya barabarani, ambapo jumla ya makosa 351 sawa na asilimia 24.9 kati ya makosa yote yaliyoripotiwa, kwa Wilaya ya Micheweni  ina idadi ndogo ya makosa ya barabarani yaliyoripotiwa ambayo ni makosa 29 sawa na asilimia 2.1.

Nae Koplo Ali Abdullah wa Jeshi la Polisi Usalama wa Barabarani amesema mafanikio ya kupungua kwa ajali za barabarani imetokana kwa kufuata miongozo na sheria.

Koplo Ali ametaka jamii kufuata sheria za barabarani kama walivofuata sheria za  kujikinga na corona na kutii masharti hadi maradhi hayo kumalizika.

Afisa wa leseni kutoka Mamlaka ya Usafiri naUsalama Barabarani Nassor Mwinyi Mzale ametoa tahadhari kwa wapanda pikipiki kuepuka kwenda mwendo wa kasi ili kujikinga na ajali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.