Habari za Punde

Redio Jamii Micheweni FM Inaomba Mashirikiano Zaidi na Wadau wa Maendeleo.

 Micheweni FM inaomba mashirikiano zaidi

Redio Jamii Micheweni ambayo iliongoza Nchini Tanzania mwaka 2019 kwa ubora wa maudhui ya Redio katika utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam imefanikiwa  zaidi katika uzalishaji wa maudhui bora ya vipindi vya redio licha ya kukabiliwa na changamoto  ya uwezo wa kifedha.

Meneja wa redio hiyo, Ali Masoud alisema, ni furaha kuona kwamba mafaniko yote yanatokana na uwezo waliojengewa na mashirika mbalimbali zaidi hasa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambao umewezesha kituo kukidhi mahitaji yake ikiwemo wafanyakazi pamoja na ujuzi wa kituo katika masuala ya kiutawala

Alisema kupitia maarifa ya uandaaji wa harambee waliyopata kupitia mpango huo iliwezesha kukiweka kituo karibu na jamii ya Micheweni katika shughuli zake zote ambapo kupitia hilo kilifanikiwa kufanya hafla za kukusanya fedha.

Alisema Micheweni FM imefanikiwa kuandaa hafla ya kutafuta fedha kwa uendelevu wa kituo mnamo Agosti 19, 2020 iliyohudhuriwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali aliyekusanya jumla ya shilingi milioni tano kwaajili ya ununuzi na ufungaji wa solar kwenye kituo hicho.

Pia kupitia mpango mkakati ulioandaliwa, kituo kiliweza kupata wadau wapya wa kushirikiana na kufanya nao kazi ambao ni (TAMWA ZNZ), ActionAid, na RTI ambapo kupitia wadau hao imesaidia kuongeza mapato ya kituo kwa kiwango cha shilingi milioni 11.

Alisema ujuzi wa ufuatiliaji na tathmini umekipa nguvu kituo hicho kukusanya taarifa kwa wakati kutoka kwenye vipindi vyake na kuziweka kwenye kumbukumbu kwaajili ya kuzishirikisha kwa wadau wengine, kuzichambua pamoja na kujibu maswala yaliyojitokeza iwe ya ndani au nje.

Aliongeza kuwa kituo hicho pia kimeimarisha utumiaji wa teknolojia kwa kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii ikiwamo Facebook, Twitter na Instagram ambayo inasikika hadi nje ya  mipaka ya  eneo la redio jamii ya Micheweni.

"Zamani hatukujua umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii lakini kupitia programu hii, tumewekeza nguvu zaidi katika mitandao hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa wadau wetu kutoa maoni yao moja kwa moja kupitia mitandao hiyo,” alisema Meneja Ali Kombo.

Meneja huyo alisema kuwa changamoto pekee ambayo kituo kinakabiliwa nayo kwasasa ni ukosefu wa fedha za kutekeleza mipango yake kabambe ambayo inahusu kuandika na kufuatilia maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyofikiwa na jamii ya Micheweni sambamba na kubaini changamoto zilizojitokeza.

Akiongea na waandishi wa habari, Dk Mzuri Issa ambaye ni mmoja wa washauri waelekezi alisema Redio ya Jamii Micheweni imepiga hatua kubwa sana katika eneo la uendelevu wa kitaasisi tangu UNESCO ilipozindua mpango wa mafunzo ya kukuza uwezo wa vituo hivyo mapema mwaka 2019.

Alisema kituo kimeweza kuweka miundo na mifumo yote muhimu ikiwa ni pamoja na sera, mpango mkakati ya kudumu na ya mara kwa mara.

Pia alisema kuwa kimefanikiwa kujipambanua kama redio ya kijamii kwa kuifanya jamii ya Micheweni kuwa sehemu ya juu ya kufanya maamuzi katika safu ya uongozi wa kituo hicho, kuwa na bodi huru yenye kuishirikisha jamii pamoja na ushiriki wa jamii katika kuandaa habari, vipindi, mijadala, sherehe na harambee.

Safia Mohamed Mzirai mmoja wa wadau wa kituo hicho alisema, “kwa sasa tunaona redio jamii imebadilika sana kwani sisi wasikilizaji tunapata kile tunachohitaji kwa wakati kutokana na mfumo ambao wameuweka hivi sasa wa kutushirikisha katika kila kitu wanachofanya, hii imesaidia sana."

Aliongeza kuwa, kulingana na uwezo na juhudi za redio kushughulikia maswala ya kijamii na kiuchumi yanayojitokeza kwa kuishirikisha jamii yenyewe hali hiyo imewafanya kuendelea kujivunia uwepo wa kituo hicho ndani ya jamii yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.