Habari za Punde

Hutuba ya Ufunguzi wa Baraza la Kumi la Wawakilishi Zanzibar Wakati wa Ufunguzi huo Uliofanyika leo.

 
HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KATIKA UZINDUZI WA BARAZA LA KUMI LA WAWAKILISHITAREHE: 11 NOVEMBA, 2020

 

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,

 

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla;

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

 

Mheshimiwa Omar Othman Makungu;

Jaji Mkuu wa Zanzibar,

 

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi na Mama Siti Mwinyi,

 

Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk.  Amani Abeid Amani Karume na Mama Shadya Karume,

 

Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Mama Mwanamwema Shein,

 

Mheshimiwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaafu

Balozi Seif Ali Iddi na Mama Asha Suleiman Iddi,

 

Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,

 

Waheshimiwa Mabalozi Wadogo mliopo, Zanzibar,

 

Wawakilishi wa Mashirika mbali mbali ya Kimataifa mliopo,

 

Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya Siasa,

 

Ndugu Wageni Waalikwa,

 

Ndugu Wanahabari,

 

Mabibi na Mabwana,  

 

Assalam Aleikum.

 

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kutujaalia uhai na afya njema, na kutuwezesha kukutana katika siku hii ambayo ina nafasi yake katika historia ya nchi yetu.

 

Leo tumekutana hapa kuzindua rasmi Baraza la Kumi la Wawakilishi la Zanzibar ambalo linaambatana na kuanza kwa Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Kabla sijaendelea na hotuba yangu, nachukua fursa hii kutoa salamu za pole kwa uongozi na wanachama wa Chama cha ACT Wazalendo, Familia pamoja na Ndugu wa Marehemu Abubakar Khamis Bakar, aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Mteule wa Jimbo la Pandani.

Tutamkumbuka Marehemu Abubakar kwa mchango mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya Zanzibar katika nyadhifa zake mbali mbali za uongozi alizowahi kushika likiwemo suala la maridhiano ya kisiasa yenye lengo la kuleta Umoja wa Kitaifa hapa Zanzibar.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake na ailaze roho yake mahali Pema Peponi, Amina. Aidha, tunamuomba Mwenyezi Mungu awape wafiwa wote subira katika kipindi hiki cha msiba wa mwenzetu

 

SALAMU ZA PONGEZI

Mheshimiwa Spika,

Naomba uniruhusu kwanza nitoe pongezi zangu nyingi kwako kwa kuchaguliwa kwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi. Kuchaguliwa kwako kwa kura zote ni kielelezo cha Imani kubwa waliyonayo Waheshimiwa Wajumbe. Umefanya kazi nzuri ya kuliongoza Baraza la 9 na ndio sababu umeaminiwa kuliongoza Baraza hili la 10. Wahenga wamesema, Chanda chema huvikwa pete!

Ahadi yangu kwako ni kukupa kila aina ya ushirikiano utakaohitaji katika kutekeleza majukumu yako. Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya 8 ninayoiongoza yanategemea sana ufanisi wa Baraza la Wawakilishi. Chombo hiki ndio chombo cha uwakilishi wa wananchi. Ndio chombo  kilichopewa dhamana ya kuisimamia Serikali. Mimi naamini kuwa Baraza la Wawakilishi imara huzaa Serikali imara.

Mheshimiwa Spika,

Pamoja na salamu za pongezi kwako, niruhusu pia nimpongeze Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Nakutakieni kila la kheri katika kutekeleza majukumu yenu na katika kuitimiza dhima kubwa mliyopewa.

Kwa hakika, kuchaguliwa kwenu kwa kura zote kuongoza mhimili huu wa dola kunaashiria imani waliyonayo Waheshimiwa wajumbe wa Baraza hili kwenu kutokana na hekima, busara, uadilifu, taaluma na uzoefu mlionao. Hongereni sana.  Sisi katika Serikali tuko tayari kushirikiana nanyi katika kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Niwapongeze pia Wawakilishi wote kwa kuchaguliwa na wananchi kuwawakilisha katika Baraza hili tukufu. Mimi na ninyi tumeshirikiana katika uchaguzi na kufanya kampeni. Tumewasikia wananchi wetu na matarajio yao kwetu. Kote nilikopita mimi, na bila ya shaka ninyi, nimekutana na kiu kubwa ya wananchi wetu ya kutaka kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Wametuchagua kwa sababu tumeahidi kutimiza matarajio hayo. Aidha, Heshima yetu itatokana na sisi kutimiza matarajio yao. Heshima yetu itatokana na sisi kutimiza ahadi zetu, maana si tu kwamba ahadi ni deni, bali kutimiza ahadi ni kulinda heshima. Niwatakie kila la kheri katika kutimiza majukumu yenu. Niwahakikishie dhamira yangu na ya Serikali nitakayoiunda ni kushirikiana nanyi katika kufanikisha na kutimiza matarajio ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika,

Katika Baraza hili la 10, mbali na ninyi Wawakilishi wa kuchaguliwa, kwa mamlaka niliyopewa na Katiba ya Zanzibar ya 1984 toleo la 2020, nimefanya uteuzi pamoja na wengine wa Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Makamu wa Pili wa Rais na Mheshimiwa Dkt. Mwinyi Talib Haji kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Ninayo furaha kumtambulisha kwenu Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wangu wa Pili na kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi. Ni kiongozi kijana, mwenye ari na nguvu nyingi za kuwatumikia Wazanzibari. Ni kiongozi msikivu, mwenye huruma na mchapa kazi hodari. Nakuombeni sana mumpe ushirikiano wenu.

 

Pamoja naye, ninayo furaha kumtambulisha kwenu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Mwinyi Talib Haji. Ni kiongozi mnyenyekevu, muungwana na ni mtu makini sana. Ni msomi mzuri aliyebobea katika masuala ya sheria. Tumempa jukumu hili atusaidie ndani ya Serikali na katika Baraza lako Tukufu katika kutekeleza majukumu yake ya utungaji sheria. Nakuombeni naye mumpe ushirikiano wenu wote.

 

Mheshimiwa Spika,

Kadhalika, nakipongeza chama changu, Chama Cha Mapinduzi kwa kupata ushindi mkubwa wa asilimia 76.2 kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar, asilimia 92 ya majimbo kwa nafasi za ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na asilimia 93.6 kwa nafasi za Madiwani. Huu ni ushindi mkubwa na wa kihistoria ambao haujapata kutokea katika chaguzi zilizopita Zanzibar katika mfumo wa vyama vingi.

 

Kwa hakika, kura nyingi tulizopigiwa na wananchi ni ishara ya matumaini makubwa waliyonayo kwa uongozi mpya. Ushindi huu mkubwa tulioupata ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wananchi kwa  chama chetu na kwangu mimi binafsi. Hivyo ni wajibu  wetu sasa kukidhi matarajio ya wengi; ambalo ndilo jukumu kubwa lilio mbele yetu.


Mheshimiwa Spika,

Natoa shukrani  kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi, kuyapokea matokeo na kuheshimu uamuzi wa wananchi katika uchaguzi huo. Napenda nisisitize kuwa naheshimu maridhiano na matakwa ya kikatiba ya kushirikiana na vyama vyengine vya siasa katika kuendesha Serikali kuwatumikia wananchi wa Zanzibar. Navihakikishia tena vyama hivyo kwamba niko tayari kuyatekeleza maridhiano kama Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza.

 

DHIMA YA SERIKALI YA AWAMU YA 8

Mheshimiwa Spika,

Nimekuja Barazani leo hii kutimiza takwa la Katiba yetu linalonitaka kulizindua rasmi Baraza la Wawakilishi. Nami ninayo furaha na fahari kubwa kutekeleza takwa hilo.

 

Hivyo napenda kuitumia fursa hii kuzungumza nanyi mambo muhimu yahusuyo ustawi wa nchi yetu, watu wetu na dhima ya Serikali ya Awamu ya 8. Lengo langu ni tuweze kufahamiana juu ya tulipo, tunapotaka kwenda na namna ambavyo sisi katika Serikali tumejipanga kutafsiri na kutekeleza Ilani ya CCM ya 2020-2025, ambayo Chama Cha Mapinduzi kinachounda Serikali kimetuelekeza tuitekeleze. Nafanya hivyo ili wenzetu katika Baraza mtufahamu na kuona namna bora ya kutusaidia kufanikisha azma hiyo.

 

Mheshimiwa Spika,

Ninaposimama mbele yenu leo, ninafarijika na mambo matatu makubwa. Kwanza, mimi ni Rais wa Awamu ya 8 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kabla yangu, kumekuwapo na Marais 7. Wote hawa wamefanya kazi kubwa sana ya kuitoa Zanzibar ilipokuwa kuifikisha ilipo leo ikiwa na mafanikio makubwa. Kutangulia kwao na kazi nzuri waliyoifanya, kunanifanya mimi kuanzia mahala pazuri zaidi kuliko pale walipopokea wao. Kipekee, nashukuru sana kuipokea nchi kutoka kwa Rais wa Awamu ya 7 na Mzee wangu Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein. Amefanya kazi kubwa sana yenye kustahili pongezi zetu nyingi. Jukumu lililo mbele yangu ni kumalizia pale ambapo hakukamilisha, kuendeleza mazuri aliyoyaacha na kufanya mengine mapya ya kuipeleka nchi yetu mbele.

 

Pili, Nimepata bahati na heshima kubwa ya kuwaongoza wananchi wa Zanzibar ambao Asilimia 93 kati yao, wamezaliwa baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya 1964 na Muungano wetu wa mwaka 1964. Najisikia fahari kuwa Rais wa kwanza kuiongoza Zanzibar ambaye amezaliwa baada ya matukio hayo mawili muhimu katika historia yetu.

 

Hii kwangu ina maana kubwa sana. Nayo ni kuyatafsiri upya Mapinduzi yetu Matukufu na Muungano wetu katika kizazi kipya. Tafsiri hiyo si nyengine bali ni kuijenga Zanzibar Mpya kwa kufanya Mapinduzi Mapya, ambayo ni Mapinduzi ya Kiuchumi. Ikumbukwe pia kuwa lengo la Mapinduzi halikuwa tu kuondosha Usultani, bali kuleta uhuru na ustawi kwa wananchi wa Zanzibar. Hilo la kwanza la uhuru tumefanikiwa. Hili la pili la ustawi bado tunayo safari ndefu. Ni matamanio yangu kuyadumisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kuyatafsiri katika muktadha wa mahitaji ya sasa ambayo ni ukombozi wa kiuchumi. Hiyo ndio itakuwa tafsiri yangu na ya Serikali nitakayoiunda ya ile kauli mbiu yetu tukufu “Mapinduzi … Daima”.

 

Tatu, kote nilikopita wakati wa kuomba ridhaa ya wananchi wa Zanzibar, nimekutana na ari, shauku na utayari wa hali ya juu ya wake kwa waume, vijana kwa wazee, wakulima kwa wavuvi, wafanyabiashara kwa wafanyakazi na makundi yote, ya kuyapokea Mapinduzi mapya ya kiuchumi na kujenga Zanzibar mpya. Wananchi wetu wamechoshwa na siasa za uhasama, kuhubiri chuki na visasi ambazo hazibadilishi hali ya maisha yao kuwa bora zaidi. Wanataka matunda ya Mapinduzi na si simulizi za Mapinduzi na Muungano. Wanachotaka ni kustawi na kufaidika na matunda ya mapinduzi kwa usawa, bila upendeleo wala ubaguzi. Mimi nakubaliana nao na ninasimama nao!  Nami nimewaahidi, “Yajayo ni neema tupu”.

Kwa mnasaba huu, nimedhamiria kuwaunganisha wananchi wote kuwa wamoja, bila ya kujali rangi, asili, jinsia, imani za kidini au itikadi za kisiasa, jambo ambalo tayari nimeanza kulitekeleza katika uteuzi wa viongozi ninaoendelea kuufanya. Ifahamike kwamba uteuzi wa viongozi na watendaji katika Serikali yangu utazingatia uwezo wa mtu kitaaluma, uwajibikaji na uaminifu.

 

MAPINDUZI YA UCHUMI

Mheshimiwa Spika,

Katika kuijenga Zanzibar mpya, moja ya ahadi yangu kubwa niliyoitoa kwa wananchi na ambayo imeelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni kujenga uchumi wa kisasa wa Bluu (Blue Economy). Uchumi wa Buluu, ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta  za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbali mbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

 

Zanzibar hatukujaaliwa ardhi kubwa. Nchi yetu ni visiwa. Idadi ya watu wetu imeongezeka mara tano katika kipindi cha miaka 56. Mwaka 1964 Wazanzibari tulikua laki 3 tu, leo tuko takribani milioni 1.6. Wakati huo huo Visiwa vyetu havipanuki wala kuongezeka. Ndio kusema, ardhi yetu inazidi kuwa finyu mwaka hadi mwaka. Ahueni tuliyonayo ni kuwa na eneo kubwa la bahari. Hivyo sisi Wazanzibari hatuna budi tuigeuze bahari hii kuwa ndio shamba letu. Huko ndiko fursa na ajira za Zanzibar mpya zilipo. Huu ndio msingi wa dhana nzima ya Uchumi wa Bluu.

 

UVUVI

Mheshimiwa Spika,

Uvuvi ni eneo ambalo hatujalitumia vyakutosha na linaweza kutuletea manufaa mengi. Serikali itaweka mkazo juu ya kuendeleza uvuvi wa bahari kuu kwa kununua vyombo vitavyoweza kutumika kwa aina hiyo ya uvuvi. Nitazitekeleza ahadi nilizozitoa wakati nilipokutana na wawakilishi wa wavuvi ikiwemo ahadi ya kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia vyombo vya kisasa na mikopo kwa ajili kuendeleza shughuli zao. Hili litakwenda sambamba na kuboresha masoko yaliyopo na kujenga masoko mapya ikiwa ni pamoja na viwanda vya usindikaji wa Samaki kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi. 

 

Vile vile, katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba hasa yale yenye bahari zenye mikoko na yenye mazingira mazuri, tumedhamiria kuimarisha shughuli za ufugaji wa samaki, kama nilivyoahidi, katika kampeni. Serikali itazalisha na kusambaza kwa wananchi vifaranga vya samaki milioni 10 kila mwaka kwa watakaojishughulisha na ufugaji samaki.

Kwa upande wa zao la mwani, tutaongeza uzalishaji kwa kuwawezesha wakulima wa zao hilo. Kama nilivyoahidi wakati wa Kampeni, tutawapatia vifaa na mikopo nafuu wakulima wa mwani, tutajenga viwanda vya kusarifu mwani, tutawatafutia  masoko mapya ili zao hilo liwe na bei kubwa zaidi  itakayosaidia kuinua hali ya maisha na kipato chao,  hasa kina mama. Nawataka wajumbe wa Baraza hili la Kumi, muwe mstari wa mbele kuisimamia Serikali na kuishauri juu ya namna bora ya kutekeleza azma yetu hiyo.

 

UTALII

Mheshimiwa Spika,

Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kukuza na kuimarisha Sekta ya Utalii ambayo hivi sasa ndiyo muhimili mkuu wa uchumi wetu. Tutashirikiana kuitangaza Zanzibar katika masoko ya asili na masoko mapya; kuendelea na ujenzi wa hoteli za daraja la juu na miundombinu muhimu; kulinda na kuhifadhi vivutio vya utalii vilivyopo pamoja na kuanzisha vivutio vyengine vipya. Ninapata matumaini makubwa kuona kwamba licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa zilizosababishwa na maradhi ya COVID 19, bado kuna mashirika mengi ya ndege na yale yanayoshughulika na biashara ya utalii yanayotaka kufanya safari za kuja Zanzibar kwa ajili ya kuleta wageni. Tumepata taarifa ya ongezeko la wageni katika siku za karibuni.

Mheshimiwa Spika,

Kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii hivi sasa, kunanipa matumaini kwamba tutaweza kuyafikia malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya kuongeza idadi ya wageni wanaoitembelea Zanzibar kutoka 538,264 mwaka 2019 hadi kufikia wageni 850,000 mwaka 2025. Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili tukufu tuna kazi kubwa ya kushajiisha na kuendeleza Mpango wa Utalii kwa Wote yani “Tourism for All”, ulioanzishwa na Awamu iliyopita ili manufaa ya sekta hii yamguse kila mwananchi kama ilivyokusudiwa. Nimeahidi na nitaitekeleza ahadi ya kuongeza utalii katika kisiwa cha Pemba. Nina azma ya kukifanya kisiwa cha Pemba, eneo maalum la uwekezaji yaani Strategic Investment Area kwa kutoa vivutio mahsusi kwa wawekezaji ili maendeleo ya Unguja yaende sambamba na maendeleo ya Pemba.

 

Serikali ninayoiongoza  itahakikisha kwamba juhudi zetu za kukuza utalii zinakwenda sambamba na utekelezaji wa mipango yetu ya kuelimisha jamii umuhimu wa kuulinda na kuutangaza utamaduni wetu, kuyathamini mambo ya kale  pamoja na kuendeleza historia na urithi wa  Zanzibar, ukiwemo Mji Mkongwe ambao  umepata umaarufu mkubwa hivi sasa duniani kote.

 

MAFUTA NA GESI

Mheshimiwa Spika,

Sekta ya Mafuta na Gesi ni miongoni mwa maeneo makuu ya Uchumi wa Buluu. Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza juhudi za kushughulikia Sekta hii. Tarehe 23 Oktoba, 2020, Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba, Dk. Ali Mohamed Shein alitoa taarifa maalum kwa  waandishi wa habari,  kuhusu matokeo ya Awali ya tafiti zilizofanywa katika utafutaji na  uendelezaji wa rasilimali  hizo.  Ufupisho wa taarifa iliyotolewa ni kwamba tafiti zilizofanywa zimeonesha uwezekano mkubwa wa kuwepo miamba yenye kuhifadhi rasilimali za mafuta na gesi asilia. Utafiti umeonesha kuwepo kwa maumbile ya miamba (structures) yenye uwezo wa kuhifadhi rasilimali ya gesi asilia yenye ujazo wa futi trilioni 3.8.

 

Matokeo haya ya utafiti yanathibitisha ile kauli mbiu yetu kwamba “yajayo ni neema tupu”. Tumeshafikia makubaliano ya kindugu baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kulitoa suala la mafuta na gesi katika mambo ya Muungano; na hivi sasa sheria mbali mbali zimeshatungwa za kusimamia Sekta hiyo. Kwa hivyo, Zanzibar itanufaika moja kwa moja na mapato yote yanayotokana na rasilimali hizo wakati wowote kazi ya uchimbaji itakapoanza.

 

Kwa hivyo, Serikali ya Awamu ya  8 itaziimarisha na kuzijengea uwezo wa kitaaluma na nguvukazi Kampuni ya Mafuta Zanzibar (ZPDC) na Mamlaka ya  Usimamizi wa Mafuta na Gesi (ZPRA) ili ziweze kuiongoza sekta hii muhimu.  Vile vile, tutaendelea kushirikiana na kampuni mbali mbali zenye dhamira njema ya kuwekeza katika nchi yetu kwenye sekta hiyo.

 

BANDARI

Mheshimiwa Spika,

Serikali ya Awamu ya Nane ina malengo ya kujenga bandari kubwa katika maeneo ya Mangapwani. Bandari hiyo ya kisasa itakuwa kubwa yenye sehemu kadhaa za kutolea huduma zikiwemo sehemu za kuhudumia meli zitakazobeba mafuta na gesi, chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli, eneo la kuhudumia meli zinazobeba mizigo na makontena, bandari ya uvuvi na bandari ya meli za kitalii.

 

 

Mheshimiwa Spika,

Uchumi wa Bluu haukamiliki bila kuweko kwa Bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu. Kwa upande wa bandari, yamekuwepo malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kucheleweshewa mizigo yao bandarini na msongomano wa makontena katika bandari ya Malindi, vitendo vya rushwa na kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi wa bandari.

 

Kwa kutambua umuhimu wa Bandari kwa Zanzibar, sikukawia kuanza na jambo hili mara tu baada ya kuapishwa kwangu. Tarehe 3 Novemba, 2020 niliamua kutembelea Bandari ya Malindi, ili kuweza kufahamu kwa kina malalamiko ya wafanyabiashara na wananchi kuhusiana na utendaji kazi na utoaji wa huduma usioridhisha unaofanywa na wafanyakazi katika Bandari yetu hiyo.

 

Bandari ni lango kuu la biashara duniani. Kwa hivyo kukosekana kwa ufanisi unaopelekea usumbufu kwa wafanyabishara katika Bandari yetu kuu ya Malindi kunazorotesha kasi ya ukuaji wa uchumi wetu; kwa sababu wafanyabiashara hao hulazimika kutumia bandari nyengine; hasa za Mombasa na Dar es Salaam.

 

Mheshimiwa Spika,

Katika uzinduzi wa Baraza  hili la Kumi  la Wawakilishi, nataka niwajulishe  viongozi na wafanyakazi  wote katika  bandari zetu kuu za  Unguja na Pemba pamoja na Viwanja vya ndege kwamba nitakuwa nikifuatilia kwa karibu utendaji wa taasisi hizo. Ieleweke bayana, kwamba sijaridhishwa  na  uendeshaji wa shughuli za  bandari na viwanja vyetu vya ndege, katika maeneo yote, hasa  utoaji wa huduma, uendeshaji, ukusanyaji na  udhibiti wa mapato,  kiwango cha faida kinachopelekwa Serikalini kila mwaka pamoja na mipango ya matumizi ya fedha za maendeleo. Nitahakikisha kwamba  wafanyakazi wa bandarini na viwanja vya ndege ni wale wanaopenda kazi  kuwatumikia watu, na sio wale wenye malengo binafsi ya kujinufaisha.

 

Napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kuwa tayari tumeshaanza kuzifanyia kazi changamoto hizo ikiwemo kujaza nafasi ya Mtendaji Mkuu katika mamlaka ya Bandari. Hili ni eneo ambalo nitalisimamia kwa nguvu zangu zote maana ni eneo lenye fursa ya kutupa mapato mengi ya kuendeleza Zanzibar yetu. Vile vile, tumedhamiria kuiimarisha bandari za Wete na Shumba Mjini. Kadhalika, tutaiimarisha bandari ya Mkoani ili iweze kuhudumia meli kubwa kutoka nje moja kwa moja kwa lengo la kunyanyua uchumi na biashara kwa kisiwa cha Pemba.

 

BIASHARA NA VIWANDA

Mheshimiwa Spika,

Serikali ya Awamu ya 8 itaendeleza dhamira njema ya kukuza Sekta za Biashara na Viwanda hapa Zanzibar, ili kuwaletea wananchi wake maendeleo zaidi ya kiuchumi. Katika kipindi changu cha uongozi nitahakikisha kwamba Sekta Binafsi inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mipango na mikakati iliyopo ya ujenzi wa viwanda vidogo vidogo, vya kati  na vikubwa vyenye kuzalisha  bidhaa bora,  zenye  viwango na vyenye kuhimili ushindani wa soko. Nitahakikisha  tunatekeleza ahadi niliyotoa katika Wilaya mbali mbali za Unguja na Pemba ya kujenga viwanda mbali mbali, vikiwemo viwanda  vya kusarifu mwani, kusindika samaki na mazao mengine, ili kuyaongezea thamani. Serikali itahakikisha inavilinda viwanda hivyo dhidi ya ushindani usio wa haki wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ambazo hazilipiwi kodi stahiki.

Serikali inatambua kwamba hii ndio njia ya uhakika ya kutengeneza ajira, kutoa soko kwa malighafi za ndani na kuongeza pato la Serikali linalotokana na kodi stahiki zitakazolipwa na viwanda hivyo.

 

MAKUSANYO YA KODI

Mheshimiwa Spika,

Ili tuweze kutekeleza kwa ufanisi ujenzi wa uchumi mpya, ni lazima tuongeze uwezo wetu wa kukusanya kodi. Serikali ya Awamu ya 8 itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Aidha, tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.

 

SEKTA BINAFSI

Mheshimiwa Spika.

Naamini kwamba ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi dhamira yetu ya kufanya mageuzi ya kiuchumi, lazima pawe na ushirikiano mzuri na wa kuaminiana baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Wakati wa Kampeni za Uchaguzi nilikutana na viongozi waliowakilisha Sekta Binafsi kwa lengo la kujadiliana, kubuni na kutafuta njia bora za kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuijenga nchi yetu.

 

Serikali ya Awamu ya 8, itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili sekta binafsi iwe na mchango mkubwa zaidi katika kukuza ajira na katika Pato la Taifa. Ushirikiano na umoja wetu ndio utakaotuwezesha kutekeleza  miradi yenye tija ikiwemo uendelezaji wa viwanda, utaliii na  uchumi wa buluu. Ili kufanikisha azma hii, serikali itaweka mifumo rafiki kwa sekta binafsi kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi. Kadhalika, Serikali itaweka mazingira rafiki kwa Wanadiaspora kuja kuwekeza nyumbani kwa lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi tunayokusudia kuyafanya. Nataka niwahakikishie wadau wa Sekta Binafsi kwamba Serikali yangu haitakua kikwazo kwa Sekta Binafsi bali tutakuwa wadau wezeshi. Kwa mnasaba huu, sitokubaliana na visingizio vya aina yoyote na uzembe wa watendaji vyenye kukwamisha azma yangu hii.

 

VIWANJA VYA NDEGE

Mheshimiwa Spika,

Mapinduzi makubwa ya uchumi tunayoyatarajia, yanahitaji kuwa na viwanja vya ndege vya kisasa vyenye ubora wa kimataifa. Tutaendeleza jitihada zilizofanywa za kuimarisha Kiwanja cha Ndege cha Abeid Amaan Karume hasa baada ya ujenzi wa jengo la Terminal Three. Hatua hiyo sio tu imeuongezea hadhi na haiba uwanja huo, bali pia itawezesha kuzihudumia ndege kubwa zaidi pamoja na idadi kubwa ya abiria, mizigo  na watalii wanaoitembelea Zanzibar. Aidha, tunathamini jitihada zilizofanywa katika kuimarisha miundombinu ya uwanja wa ndege wa Pemba, ikiwemo kuongezwa majengo ya kutolea huduma pamoja na kuwekwa taa za kuongozea ndege. Tutaendelea na juhudi za kuimarisha  viwanja hivyo pamoja na huduma zinazotolewa, ili viwe na mchango zaidi katika kuongeza ukusanyaji wa mapato na kukuza soko la ajira.

 

 

BARABARA

Mheshimiwa Spika,

Ujenzi wa barabara bora za kisasa ni muhimu katika kufikia mapinduzi ya uchumi mkubwa wa kisasa tunaoutarajia kuujenga. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, nimeahidi kuendeleza kazi za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa zaidi ya kilomita 197.6. Unguja na Pemba.

 

Miongoni mwa barabara zitakazojengwa kwa Unguja ni Tunguu-Jumbi (km9.3), Jozani-Charawe-Ukongoroni-Bwejuu (km23.3), Fumba-Kisauni (km 12), Kizimbani-Kiboje (km 7.2) na Kichwele-Pangeni (km 4.8). Nyengine ni barabara ya Umbuji- Uroa (km 6.9), Mkwajuni-Kijini (km 9.4) na Tunguu-Makunduchi (km48). Vile vile, kwa kuzingatia usumbufu wanaoupata wananchi wanaoishi vijiji vya Uzi na Ng’ambwa, Serikali itashughulikia ujenzi wa barabara na daraja kutoka Unguja ukuu hadi kisiwa cha Uzi.

 

Kwa upande wa Pemba, tutazijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Chake chake – Wete (km 22.1), Mkoani-Chake chake kupitia Chanjaani (km 29) na barabara ya Finya – Kicha (km 8.8). Vile vile, tutazitengeneza barabara za ndani za Unguja na Pemba ili zipitike kwa urahisi wakati wote.

 

NISHATI YA UMEME

Mheshimiwa Spika,

Uchumi mkubwa wa kisasa tunaoukusudia, unahitaji kupatikana kwa nishati ya umeme wa kutosha wenye uhakika. Dhamira yetu ya kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Viwanda inahitaji kuwa na umeme wa kiwango kikubwa. Kwa upande wa Unguja, mahitaji ya umeme hivi sasa yameshafikia megawati 80, ambapo laini mpya ya umeme tuliyo nayo ina uwezo wa kuchukua megawati 100; na ile ya zamani ina uwezo wa kuchukua megawati 40.

 

Kwa mantiki hii, baada ya kipindi kifupi kijacho, kiwango cha umeme tulichonacho kitakua ni changamoto katika kufikia dhamira yetu ya kujenga uchumi mpya wa kisasa. Hali hii, inatulazimisha kuanza kuendeleza suala la kutafuta vyanzo vipya vya umeme, ikiwemo nishati mbadala ili nchi yetu iwe na umeme wa uhakika.

 

HUDUMA ZA FEDHA

Mheshmiwa Spika,

Sambamba na miongozo ya Ilani ya Uchaguzi, Serikali ya Awamu ya 8, itaweka mkazo mkubwa katika kuimarisha Sekta ya Huduma za Fedha kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za benki, mashirika ya bima na taasisi nyengine za fedha. Dhamira yetu ni kuona kwamba huduma za fedha zinazotolewa na taasisi binafsi na Serikali zinakidhi wiwango na mahitaji halisi ya wawekezaji, watalii, wageni wanaotumbelea pamoja na wananchi kwa jumla. Serikali itasimamia utendaji wa mashirika yake kwa lengo la kuhakikisha kwamba taasisi hizo zinatoa huduma bora zenye kuaminika kwa wateja wote.

 

TEKNOLOJIA

Mheshmiwa Spika,

Matumizi bora ya teknolojia ni msingi muhimu katika juhudi zetu za kuendeleza viwanda, biashara, utalii, huduma za fedha na shughuli mbali mbali za kijamii. Kwa msingi huo, Serikali ya Awamu ya 8 ina lengo la kuendesha shughuli zake katika mifumo ya kisasa ya kidigitali. Tutaweka mifumo ya kidijitali katika ukusanyaji wa kodi za Serikali, manunuzi ya umma na uendeshaji wa Serikali kwa ujumla. Aidha, Serikali  itaimarisha  mitaala ya masomo ya sayansi katika skuli, vituo na taasisi za ufundi pamoja na vyuo vikuu  ili kuwaandaa vizuri vijana wetu na hatimae  kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia katika sekta zote.

 

KILIMO

Mheshimiwa Spika,

Serikali ya Awamu ya 8 itaendeleza mipango na mikakati iliyoanzishwa na Serikali ya Saba katika kuendeleza Sekta ya Kilimo ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inajitosheleza kwa mahitaji ya chakula. Tutaendeleza mpango mkuu wa umwagiliaji maji Zanzibar (Zanzibar Irrigation Master Plan) ambao umebainisha kuwa zipo hekta 8,521 zinazofaa kujengwa miundombinu ya umwagiliaji maji. Hivi sasa, jumla ya hekta 2,527 tayari zinaendelea kujengwa miundombinu ya umwagiliaji maji kutoka hekta 700 za mwaka 2010. Ujenzi huo unaendelezwa katika mabonde ya Cheju, Kilombero, Chaani, Kibokwa, Kinyasini kwa Unguja na Mlemele na Mkwararani kwa upande wa Pemba. Halikadhalika, Serikali itahakikisha inaendeleza huduma za ugani kwa kuajiri wataalamu wa kutosha na kutoa vifaa vinavyohitajika.

Kadhalika, tutaendelea kuhimiza kilimo cha kisasa katika uzalishaji wa mazao mengine ya chakula kwa kuwawezesha vijana kuendeleza kilimo kwa ujenzi wa vitalu nyumba (green houses) na matumizi ya mbegu bora za kilimo. Vile vile, tutaweka mkazo katika kununua pembejeo za kilimo, dawa za kuulia magugu pamoja na kuwapatia wakulima huduma bora za matrekta. Watu wengi duniani hivi sasa wanapendelea kula vyakula vinavyotokana na kilimo hai yaani “Organic Farming” kutokana na ladha ya asili ya vyakula hivyo pamoja na uwezekano wa kuwa vinapunguza athari za kemikali. Ni jambo muhimu kwa Taasisi itakayohusika na Kilimo kulifanyia utafiti suala la kukiendeleza kilimo hai nchini mwetu na upatikanaji wa masoko ya mazao yanayopatikana kutokana na kilimo hicho.

 

Mheshimiwa Spika,

Kwa kutambua umuhimu wa zao la karafuu na uhusiano wake katika historia na maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar, Serikali ya Awamu ya Nane itaendeleza juhudi zilizopo za kuliimarisha zao hilo kwa kutoa mikopo na kuwatafutia masoko wakulima. Kadhalika, kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa nazi unaopelekea kupanda bei ya zao hilo kila uchao, Serikali itaimarisha upandaji wa miche ya minazi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo. Serikali itasimamia na kuendeleza programu ya kufufua zao la minazi  iliyoanzishwa mwaka 2019; lengo likiwa ni kuotesha miche ya minazi 1,200,000 (Unguja minazi 720,000 na Pemba minazi 480,000); ambapo asilimia  17  itakuwa ni minazi ya madafu naasilimia   83 itakuwa ni minazi yetu ya asili  (East African tall).

 

UFUGAJI

Mheshimiwa Spika,

Serikali ya Awamu ya 8, itaweka mkazo katika kuendeleza shughuli za ufugaji wa njia za kisasa, ili sekta hiyo iwe na tija zaidi kwa wakulima na kuongeza mchango wake katika upatikanaji wa chakula na kuimarisha Pato la Taifa.

Tutahakikisha panakuwa na matumizi mazuri ya pembejeo za mifugo, dawa za chanjo na kutoa elimu juu ya matumizi ya mbegu bora za mifugo. Serikali itabuni na kutekeleza mikakati madhubuti ya kukomesha wizi wa mifugo na mazao.  Katika kuitekeleza mikakati hiyo, tuzingatie sheria za nchi yetu na Waheshimiwa Wawakilishi muwashirikishe wananchi majimboni mwenu katika kupambana na wizi wa mifugo na mazao ya kilimo ambao hivi sasa umekithiri katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

 

Ninaamini kwamba kwa juhudi za pamoja tunaweza kukomesha vitendo hivi viovu vinavyorejesha nyuma maendeleo ya wakulima na wafugaji. Katika kuiendeleza sekta ya mifugo, serikali itakaribisha wawekezaji wakubwa wa ufugaji hasa wa ng’ombe na mbuzi wa maziwa ambao wataweza kuwasaidia wafugaji wetu wa dogo wadogo kuzalisha bidhaa nyingine zinazotokana na mifugo.

 

MAZINGIRA NA TABIANCHI

Mheshimiwa Spika,

Utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo utazingatia sana kuwepo kwa mipango mizuri ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Tutahakikisha kwamba tuna matumizi mazuri ya rasilimali zisizorejesheka, utunzaji wa maliasili na misitu, fukwe pamoja na bahari.

Kadhalika, tutaweka mkazo katika kuhakikisha kwamba Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri zetu zinasimamia vyema jukumu lao la usafi wa miji. Nataka niweke wazi kwamba kiwango cha usafi katika miji yetu hakiridhishi. Naamini kwamba Waheshimiwa Wajumbe mtaungana na mimi nikisema kwamba hakuna sababu ya kuifanya miji yetu isiwe safi na salama. Kwa hivyo, Serikali itahakikisha kwamba miji yetu inakuwa safi wakati wote kwa ajili ya kulinda afya za wananchi na kuvutia wageni wanaokuja kututembelea.

 

HUDUMA ZA JAMII

Mheshimiwa Spika,

Serikali ya Awam ya 8, itaweka kipaumbele katika kuziimarisha huduma za elimu, afya na maji safi na salama kwa kuzigatia umuhimu wake kwa ustawi wa maendeleo ya jamii.

 

ELIMU

Mheshimiwa Spika,

Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya elimu kama ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Serikali itachukua hatua za kuimarisha ubora wa elimu ambayo ni haki ya msingi kwa kila mwananchi. Katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu hivi sasa, Serikali itaelekeza juhudi katika kuimarisha miundombinu ya elimu, ikiwemo, ujenzi wa skuli za kisasa na kuzikarabati skuli za zamani, kuzipatia skuli vifaa vya kufundishia na kusomea pamoja na madawati, kupitia upya mitaala ya elimu na kupunguza tatizo la walimu hasa wa masomo ya Sayansi.

 

Kadhalika, tutaimarisha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya Taifa, kuendeleza masomo ya ufundi katika vyuo vya amali na vituo mbali mbali. Ili kufikia dhamira hiyo, Serikali itaongeza bajeti ya sekta ya elimu ili iweze kugharamia vyema huduma za elimu katika ngazi zote kwa kuendeleza sera ya elimu pamoja na kuongeza fursa za mikopo ya wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu.

 

Pamoja na hatua hizo, tutayaimarisha maslahi ya walimu ili kuwapa motisha ya kufundisha na tutaendeleza sera ya elimu bure kwa lengo la kuwaondolea wazazi mzigo wa kuchangia elimu ya watoto wao.

 

Mheshimiwa Spika,

Nikiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), nitahakikisha kwamba tunakiendeleza Chuo hiki kwa kuanzisha programu mpya kutegemea mahitaji halisi ya nchi yetu, sambamba na kujenga majengo mapya pamoja na kukipatia vifaa vya kisasa vya kufundishia vinavyohitajika ili kuweza kutoa elimu bora kwa wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho. Tutaweka mkazo katika kufanya tafiti kwenye maeneo muhimu kwa kuzingatia ajenda za maendeleo ya kiuchumi na kijamii za nchi yetu.

 

Tutahakikisha kwamba SUZA inaendelea kuwa na uhusiano mwema na vyuo na taasisi za elimu ya juu zilizopo Zanzibar na sehemu mbali mbali za dunia. Tutaendelea kuweka mkazo maalum katika kufundisha Kiswahili ili kutekeleza dhamira yetu ya kuifanya Zanzibar kuwa chimbuko la Kiswahili sanifu na fasaha. Tutahakikisha kwamba wahitimu wa chuo chetu hiki katika fani zote tunazofundisha wanabobea kitaaluma na wanajengeka kiushindani katika soko la ajira popote wanapokwenda.

 

AFYA

Mheshimiwa Spika,

Kwa upande wa Sekta ya Afya, Serikali itandelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa huko Binguni Wilaya ya Kati ambayo itakuwa na huduma zote za kibingwa. Mpango wake upo na lazima tuusimamie utekelezaji wake kwa nguvu zetu zote. Hatua hiyo, itatuwezesha kupunguza na hatimae kuondoa kabisa tatizo la kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Sambamba na juhudi hizo, tutaendelea kuimarisha miundombinu ya afya, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, kuongeza idadi ya madaktari bingwa wa fani mbali mbali na wataalamu wengine wa afya. Tutaongeza bajeti ya kununulia dawa na vifaa vyengine vya huduma za afya. Vile vile, tutaongeza nyumba za madaktari na kujenga vituo vya afya ili kuondoa usumbufu wanaoupata baadhi ya wananchi kufuata huduma za afya katika maeneo ya mbali.

Aidha, tutaimarisha Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na hospitali za wilaya za Makunduchi na Kivunge. Tutazijengea uwezo Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, Hospitali ya Chake Chake na Wete pamoja na kuipandisha hadhi hospitali ya Micheweni. Lengo letu ni kuona kwamba huduma zote za kibingwa zinapatikana katika Kisiwa cha Pemba. Katika kufikia dhamira zetu hizo, tutawashajiisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya afya. Vile vile, tutaangalia uwezekano wa kuanzisha bima ya afya kwa wenye uwezo na kwa wale wasio na uwezo Serikali itaendelea kuwapatia huduma za afya bure.

 

MAJI SAFI NA SALAMA

Mheshimiwa Spika,

Upatikanaji wa huduma za maji bado ni changamoto katika baadhi ya  maeneo ya mjini na vijijini.  Hali ya upatikanaji wa maji hivi sasa imefikia  wastani wa asilimia  83 katika mwaka 2020.  Kwa kuzingatia kuwa maji ni uhai, Serikali ya Awamu ya 8 itamalizia kazi iliyobaki ya kuiboresha miundo mbinu ya maji na kuongeza upatikanaji wake. Kazi hiyo, ni pamoja na kujenga matangi mapya ya kuhifadhia maji, uchimbaji wa visima vipya vya maji na kuendelea kuifanyia matengenezo miundombinu ya zamani, ikiwemo kuvitengeneza visima vya zamani na kuviwekea pampu zenye nguvu zaidi. Vile vile, tutayabadilisha mabomba ya zamani na kukabiliana na tatizo la uvujaji wa maji.

 

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

Mheshimiwa Spika,

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni miongoni mwa malengo ya Serikali ya Awamu ya 8 katika kukabiliana na tatizo la umaskini wa kipato unaosababishwa na ukosefu wa ajira. Tunaelewa kuwa bado kuna changamoto zinazowakabili wananchi katika kuendesha shughuli za ujasiriamali, ambazo zinahusiana na ukosefu wa mitaji, vifaa, utaalamu wa kutosha wa kuendesha biashara na utafutaji wa masoko ya uhakika ya kuuzia biashara hizo. Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali itauimarisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kuuongezea uwezo wa kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wengi zaidi.

 

Kadhalika, tutawasajili wajasiriamali wote na kuwapatia vitambulisho. Pia, tutatoa mafunzo ya namna bora ya kuitumia mitaji na mikopo hiyo katika kupata vifaa na zana za kisasa na kuendesha shughuli za ujasiriamali kitaalamu zaidi, kulingana na mahitaji ya masoko ya wakati tulio nao.

 

Aidha, tutawajengea wajasiriamali sehemu maalum za kufanyia biashara zao zitakazojengwa vizuri, ili waondokane na usumbufu wa kuhamahama huku na kule. Pamoja na jitihada hizi, Serikali itawawekea mfumo na utaratibu bora wa kulipa kodi mara moja tu kwa mwaka na kuondosha ile kero ya utitiri wa kodi.

Katika kuhakikisha kwamba mkakati huu unaleta ufanisi tunaoutarajia, tutakuwa tunafuatilia kwa karibu na kufanya tathmini ya mikopo tunayoitoa kwa vikundi hivyo, ili kujiridhisha endapo inawafikia walengwa na kwamba hakuna matumizi mabaya ya fedha hizo yanayofanywa na watumishi wa Serikali wasio waaminifu. Tusitosheke tu kutoa mikopo na mitaji na baadae kuripoti takwimu za vikundi vilivyopokea mikopo hiyo, na kuirejesha au kutoirejesha. Ni lazima tujue mikopo hio imeleta faida gani kwa wananchi.

 

UTAWALA BORA

Mheshimiwa Spika,

Maendeleo, amani na utulivu ni dhana zenye maana zinazotegemeana. Ili kuwe na maendeleo kunahitajika kuwe na amani na utulivu na kwa upande mwengine, amani na utulivu haiwezi kupatikana ikiwa hakuna maendeleo; ni kama uhusiano wa kuku na yai. Maendeleo katika nyanja mbali mbali za maisha ndiyo yanayowaletea wananchi utulivu, na utulivu ndio unaoleta amani. Wananchi wanaokabiliana na dhiki za maisha hasa katika kupata huduma muhimu za kuyamudu maisha yao, mwishowe hujenga hasira, hasira ambayo huzaa chuki miongoni mwao na kusababisha matendo maovu yanayopelekea kuvunjika kwa amani.

Ili uwiano mzuri upatikane baina ya amani, utulivu na maendeleo ni lazima tuhakikishe kwamba Serikali inaongozwa katika misingi ya utawala bora.

 

Mheshimiwa Spika,

Miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni  vitendo vya rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji, kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili. Serikali ya Awamu ya 8 itakabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Najua wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo. Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali. Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Baraza lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi wala kuoneana muhali. Ninaomba Waheshimiwa Wawakilishi na Wananchi wote mniunge mkono wakati wa mapambano haya.

 

Tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina shaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya. Ni matumaini yangu pia vyombo husika katika jambo hili vitatekeleza wajibu wao.  Nataka niweke wazi kuwa kiongozi yoyote nitayemteua kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, nitamuwajibisha mara moja pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.

 

UTUMISHI WA UMMA

Mheshimiwa Spika,

Mafanikio katika utendaji wa Serikali yanategemea jinsi Sekta ya Umma inavyotekeleza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi kwa misingi ya uwajibikaji, usawa na haki. Utendaji katika Sekta yoyote unategemea kuwepo kwa haki na utekelezaji wa wajibu. Kwa maana nyengine, haki na wajibu ni watoto pacha. Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Kwa upande mwengine, wafanyakazi nao wana wajibu wa kutekeleza kwa bidii na nidhamu kubwa majukumu ya kazi zao kwa mujibu wa sheria za utumishi, kwa maslahi ya jamii na taifa kwa jumla.

 

Kwa hivyo, Serikali ya Awamu ya 8 itasimamia kwa umakini sana nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma. Serikali haitakuwa na muhali kwa mtendaji yoyote ambae hatowajibika katika utekelezaji wa majukumu yake. Atakayeshindwa kuwajibika aelewe kuwa atawajibishwa. Uzembe na ukosefu wa nidhamu kazini huzorotesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwa hivyo, tabia hii sitoivumilia. Kadhalika, tunahitaji ubunifu wa kitaalamu katika kufanya kazi zetu na tuondokane na mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea.

 

Napenda viongozi wote nitakaowateuwa katika nafasi mbali mbali walizingatie jambo hili. Ni lazima wawe wabunifu na waweze kuishauri Serikali juu ya masuala mbali mbali yanayohusu fani na utaalamu wao. Serikali haitowavumilia viongozi wenye kusubiri kuambiwa kutoka kwangu au Serikalini nini wafanye katika kutekeleza majukumu yao. Tutaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na sheria ya hifadhi ya jamii kwa manufaa ya wanachama wote; wafanyakazi na wastaafu. Tutafungua Ofisi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii katika mikoa ya Zanzibar ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama wake.

 

IDARA MAALUM

Mheshimiwa Spika,

Serikali itaziendeleza Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili ziendelee  kutoa  huduma bora za ulinzi na usalama  kwa  wananchi na  kutekeleza majukumu yao mengine kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria zinazoongoza Idara zetu hizo.

 

Tutaendeleza miradi ya ujenzi wa  majengo ya ofisi, mahanga na nyumba za maofisa, sambamba  na kuyaimarisha mazingira ya kambi mbali mbali za Idara zetu maalumu. Vile vile,  tutaendelea kuwajengea uwezo maofisa na  wapiganaji  kwa kuwapatia  vifaa na mafunzo ya kisasa katika vyuo vya ndani na nje ya nchi. Kadhalika, tutaendelea kuimarisha maslahi yao  kwa kadri hali ya uchumi wetu itakavyoruhusu.

 

AJIRA KWA VIJANA

Mheshimiwa Spika,

Mapinduzi makubwa ya Uchumi tunayokusudia kuyafanya yatatupelekea kuwa na uchumi mpya wa kisasa, ambao utaongeza fursa nyingi za ajira kwa vijana wetu. Kwa hivyo, ni wajibu wa vijana wetu kuwa tayari kufanyakazi. Serikali itawajengea uwezo kwa kuwapatia mafunzo maalumu ya ufundi wa fani mbali mbali katika vyuo vya ufundi na vituo vya amali. Vile vile, vijana watawezeshwa kwa kupatiwa mitaji ili waweze kujiajiri wenyewe na kuondokana na tatizo la kutegemea ajira chache kutoka Serikalini. Serikali itaandaa sera nzuri za ajira na kuwashajiisha wawekezaji kuweka kipaumbele katika kuajiri vijana wa Zanzibar.

 

USTAWI WA WAZEE, WANAWAKE NA WATOTO

Mheshimiwa Spika,

Wazee ni hazina kubwa kwa nchi yetu, na kwa kutambua hilo, Serikali itaendelea kuwatunza wazee. Kwa wazee wanaoishi kwenye nyumba za wazee za Sebleni, Welezo na Limbani, huduma za kuwapatia makaazi bora, chakula na matibabu zitaendelea. Vile vile, huduma ya pensheni jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70 na zaidi zitatolewa. Hapo baadae, Serikali itaangalia uwezekano wa kushusha umri na kuongeza kiwango cha pensheni inayotolewa sasa kwa mwezi.

 

Kwa upande wa wanawake na watoto, Serikali imeazimia kuwasaidia wanawake wajane ambao tayari wameshaunda rasmi jumuia yao. Wanawake hao watasaidiwa kwa kuwezeshwa kiuchumi na kusimamia haki zao ikiwemo mirathi. Kadhalika, Serikali itaendeleza juhudi zilizotangulia za kuwapatia wanawake na watoto haki zao zote za msingi ili waishi vizuri katika jamii. Katika kulinda haki zao, Serikali itaendeleza mapambano ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia kwa nguvu zetu zote na kuhakikisha kwamba sheria zilizotungwa na kupitishwa zinazolinda usalama na maslahi ya wanawake na watoto zinatumika ipasavyo, na haki inatendeka.

 

 

WATU WENYE ULEMAVU

Mheshimiwa Spika,

Kama ilivyosisitizwa na kuelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali itaweka kipaumbele maalum katika kuwashirikisha watu wenye ulemavu kwenye shughuli mbali mbali za kiuchumi pamoja na kuzilinda na kuziimarisha haki zao. Tutawawezesha kwa kuwapatia mitaji na mafunzo mbali mbali ya ujasiriamali bila ya kuwabagua kijinsia au aina ya ulemavu walionao.

 

MAENEO MENGINE MTAMBUKA

Sanaa, Burudani na Michezo

Mheshimiwa Spika,

Eneo jengine ambalo tutalishughulikia ni sanaa, burudani na michezo. Mambo haya matatu yana nafasi ya kipekee katika kuwaunganisha Wazanzibari, kuwatambulisha Wazanzibari duniani na kukuza uchumi na kutoa ajira. Muziki wa Taarab, muziki wa kizazi kipya na sanaa ya filamu kupita matamasha ya ZIFF na ‘Sauti ya Busara’ yameitangaza sana Zanzibar na kuwa na mchango wa kipekee. Naahidi kuyalea na kuyakuza matamasha haya na mengine ili kutangaza hazina ya utamaduni na ustaarabu wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii, kipato na ajira.

 

Kwa upande wa michezo, tutafanya mengi. Lakini kubwa sana na ambalo linalifadhaisha moyo ni kupotea kwa msisimko wa Ligi ya Soka ya Zanzibar. Siku za nyuma, timu za Zanzibar za Small Simba, Malindi, Mlandege na KMKM zilikuwa ni timu zenye sifa na kuchachafya timu za Bara na Afrika Mashariki. Tutawekeza kwenye michezo katika kuibua, kulea na kuendeleza vipaji vya vijana. Hii itakwenda sambamba na kukaa na wadau wa soka kutafuta jawabu la kuamsha msisimko wa Ligi yetu ya Zanzibar. Azma yetu ni kuona Timu ya Taifa ya Zanzibar inakwenda mbali katika kushiriki michuano ya Afrika ili kutumia vizuri fursa ya uanachama wetu katika Shirikisho la Michezo la Afrika (CAF) ambayo tumeipigania kwa miaka mingi.

 

Natambua kua maendeleo ya michezo yanahitaji udhamini kutoka kwa wadau wa michezo. Naahidi kujadiliana nao ili waweze kutoa udhamini kwa michezo yetu mbali mbali.

 

AMANI NA UTULIVU

Mheshimiwa Spika,

Mafanikio ya utekelezaji wa mipango na ahadi tulizozitoa, hayawezi kupatikana bila ya kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini. Jukumu la kulinda na kudumisha amani tuliyo nayo sio la vyombo vya ulinzi na usalama peke yake. Huo ni wajibu wa kila mmoja wetu. Kuiharibu amani ni jambo jepesi na la mara moja, ila kuirudisha ni vigumu na tujifunze kwa wengine walioichezea tunu hii. Kwa hivyo, sote tuwe walinzi wa amani kwa kutambua kuwa bila ya amani hakuna maendeleo. Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya 8 itashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha kuwa amani na usalama wa Watanzania na mali zao pamoja na wageni wote wanaotutembelea nchini vinadumishwa na kulindwa.

 

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,

Kabla sijamaliza hotuba yangu, nawashukuru tena wananchi wa Zanzibar kwa kutupa dhima hii ya kuongoza nchi na Serikali. Tunatambua uzito wa dhamana tuliyoibeba kwa wananchi ya kuwatumikia watu wote kwa misingi ya usawa. Nakuahidini kuwa Serikali nitayoiunda itasimamia kwa weledi na umahiri mkubwa utekelezaji wa ahadi zote tulizozitoa wakati wa kampeni kwa ufanisi huku tukizingatia kuwa ahadi ni deni na wananchi wametuchagua kwa matumaini. Ni matarajio yangu kuwa na nyinyi Waheshimiwa Wawakilishi mtazingatia wajibu wetu huu na Madiwani wetu nao watazingatia kuwa uongozi tuliopewa ni dhamana ya kuwatumikia watu na sio kwa maslahi yetu binafsi.

 

Kwa mara nyengine, nakupongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, na Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi la Kumi la Zanzibar kwa heshima kubwa mliyopewa na wananchi ya kuchaguliwa kuingia katika chombo hiki muhimu cha kutunga sheria ili muwawakilishe. Matumaini yangu, mtaitumia vyema fursa hii kwa lengo la kuchangia mipango ya maendeleo na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi wetu kwa kusaidiana na Serikali yenu.

 

Namalizia hotuba yangu kwa kuvishukuru vyombo vya habari vinavyowatangazia wananchi tukio hili la uzinduzi wa Baraza. Kadhalika, nawashukuru wananchi wote wanaofuatilia uzinduzi huu kupitia vyombo vya habari. Tumuombe Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na mshikamamo. Mola atuwezeshe kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi. Nakutakieni nyote kila la heri na mafanikio.

 

Baada ya kusema hayo, na kwa mamlaka niliyo nayo ya kikatiba kama yalivyoainishwa katika Ibara ya 91 kifungu (1), sasa natamka kuwa Baraza la Kumi la Wawakilishi la Zanzibar limezinduliwa Rasmi leo tarehe 11 Novemba, 2020.

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR,

 

MUNGU IBARIKI TANZANIA,

MUNGU IBARIKI AFRIKA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.